Saturday, November 21, 2009

Majambazi Wateka Basi Kigoma, Wapora Mamilioni


Majambazi wawili wenye silaha za moto aina ya SMG, jana waliteka basi la abiria katikati ya kijiji cha Muyama na Mnyegera wilayani Kasulu mkoani Kigoma na kisha kupora vitu mbali mbali zikiwemo fedha na simu.

Taarifa za jeshi la polisi mkoani Kigoma zimelitaja gari lililotekwa kuwa ni Toyota Costa lenye namba za usajili T 248 AHA mali ya Lojin Msama Zihuye mkazi wa Kasulu mjini lililokuwa likitokea Muyama kwenda Kasulu.

Imebainishwa kuwa tukio hilo limetokea majira ya saa mbili asubuhi katika mlima Kabuye ambapo dereva wa gari hilo Bw. James Ngirante alilazimishwa kusimamisha gari akitishiwa kupigwa risasi.

Jeshi la polisi limeeleza kuwa katika tukio hilo majambazi wamefanikiwa kupora simu za mkononi zenye thamani ya shilingi laki nne na elfu kumi pamoja na pesa taslimu shilingi milioni 2.4 wakati thamani za mali zingine za watu zilizoibwa shilingi 2.8.

Katika ujambazi huo wahusika wanauhusisha na uwepo wa wakimbizi katika wilaya ya kasulu ambapo majambazi walidaiwa kuongea kwa lafudhi ya Kirundi na hivyo kupelekea kuwepo kwa hisia kuwa raia wa Burundi ndio wanaendesha uhalifu mpakani mwa Tanzania.

Aidha hakuna mtu aliyejeruhiwa, ingawa inatajwa kuwa huenda tukio hilo lilipangwa kutokana na majambazi hao kuwataja baadhi ya abiria kwa majina wakiwataka kutoa fedha.

Hadi sasa hakuna anayeshikiliwa kutokana na ujambazi huo na jeshi la polisi limepeleka kikosi maalumu katika tarafa ya Muyama kufanya uchunguzi utakaowezesha wahusika kukamatwa.

No comments: