Monday, November 23, 2009

Duka la Kwanza la Bangi Lafunguliwa Marekani


Duka la bangi linalojulikana kama "The Cannabis Cafe" limefunguliwa mjini Portland katika jimbo la Oregon nchini Marekani na limekuwa duka la kwanza katika historia ya Marekani kuanza kuwauzia bangi watu walioruhusiwa na madaktari kuvuta bangi kama tiba ya magonjwa yao.

Ingawa wagonjwa waliopewa ruhusa na madaktari zao kuvuta bangi wataweza kununua bangi katika duka hilo wakati wowote, bado hawaruhusiwi kuvuta bangi mbele ya hadhara.

Kabla ya kufunguliwa kwa duka hilo, wagonjwa waliopewa ruhusa ya kuvuta bangi walikuwa wakinunua bangi toka kwenye maduka maalumu ya madawa yaliyopewa idhini maalumu ya kuuza bangi.

Katika jimbo la Oregon kuna jumla ya wagonjwa 21,000 walioruhusiwa kununua na kuvuta bangi.

Madaktari nchini Marekani huwaandikia tiba ya bangi wagonjwa wa kisukari, Alzheimer, multiple sclerosis na Tourette.

Kufunguliwa kwa duka hilo la bangi kumekuja mwezi mmoja baada ya rais Obama kuwaagiza waendesha mashtaka katika majimbo yaliyoruhusu matumizi ya bangi kama tiba kutowahukumu wagonjwa ambao wanavuta bangi kama tiba ya magonjwa yao.

Takribani majimbo 12 ya Marekani likiwemo jimbo la Oregon, yamefuata hatua ya mwaka 1996 ya jimbo la California kuruhusu ulimaji na uuzaji wa bangi kama dawa.

No comments: