Friday, October 30, 2009

Spika Sitta afyatuka

SPIKA wa Bunge Samuel Sitta amesema, fedha wanazolipwa wabunge wanapohudhuria mikutano au kutembelea maeneo mbalimbali ni takrima na si posho.

Amehoji kwa nini wabunge wanasakamwa kwa sababu wanalipwa takrima wakati ni jambo la kawaida ukienda kwa mtu akakukirimu kwa chakula, chai na hata nauli.

Sitta amesema, kama takrima kwa wabunge inawakera watu, wahusika wasubiri hadi mwakani majimbo yatakuwa wazi. Amesema, wabunge wanalipwa fedha hizo kutokana na utashi wa wahusika na ni utaratibu wa kawaida.

“Hivi unapokwenda kwa mtu ukakuta umeandaliwa au akakuandalia hata chai, chakula, na wakati mwingine anakupa nauli, si jambo la kawaida? sasa kwa nini wabunge wanasakamwa, tushughulikie mambo ya msingi kama vile kilimo kwanza na elimu ”, amesema Sitta.

Amewaeleza wabunge leo kuwa, Bunge limewaruhusu wachukue takrima hiyo na kwamba leo kuna semina inafanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa (ukumbi wa Bunge wa zamani) na itifaki imezingatiwa.

“Waheshimiwa wabunge kabla sijafunga kipindi cha maswali na majibu kuna matangazo machache, kwanza kutakuwa na semina kuhusu Muswada wa Mtoto leo mchana saa saba, mnaombwa kuhudhuria, kwani itifaki imezingatiwa” amesema Sitta na kusababisha wabunge wacheke.

Sitta amesema, fedha wanazopewa wabunge si posho, ni takrima kama wanavyopewa watu wengine wanapohudhuria mikutano, wakiwemo waandishi wa habari, na kwamba, ni jambo la uungwana kumpa takrima unayemualika.


“Kama wanaona wabunge wanafaidi sana, wasubiri mwakani sio mbali majimbo yatakuwa wazi, tukutane huko”, amesema Sitta huku akinesha kukerwa.

Baada ya kuyasema hayo, wabunge walipiga makofi huku wakicheka wakiashiria kumuunga mkono Spika Sitta.

Katika siku za karibuni kumekuwa na mvutano kati ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na wabunge baada ya taasisi hiyo ya Serikali kutaka kuwahoji kuhusu suala la kuchukua posho kwenye mikutano na ziara.

Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe amekataa kuhojiwa kwa madai kuwa, Takukuru inataka kuwafunga midomo wabunge.

No comments: