Friday, October 30, 2009

Tanzania yawaonya mabalozi, wahisani

SERIKALI ya Tanzania itamfukuza nchini Balozi au ofisa yeyote wa kibalozi atakayebainika kushirikiana na vyama vya upinzani kuking’oa chama tawala madarakani.

Serikali imesema, nchi zinazotoa misaada kwa Tanzania hazina mamlaka ya kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, ametoa msimamo huo bungeni leo na kubainisha kwamba, mabalozi au ofisi za mabalozi wanaruhusiwa kushirikiana au kuvisaidia vyama vya siasa lakini si kwa lengo la kukingoa chama tawala madarakani.

Waziri Membe amesema, Balozi au ofisa wa kibalozi atayeshirikiana na vyama vya siasa kuking’oa chama tawala madarakani watakuwa wanaingilia mambo ya ndani ya nchi mwenyeji, kuvunja itifaki na sheria za kimataifa.

Kwa mujibu wa Waziri Membe, kifungu cha tisa cha Mkataba wa Vienna kinairuhusu Serikali kuwafukuza nchini bila hata kutoa sababu yoyote ya kufanya hivyo.

“Mheshimiwa Spika, tabia ya nchi za nje kuingilia mambo ya ndani ya nchi huweza kuhatarisha uhuru na usalama wa nchi. Njia kubwa na ya kudumu ya kuepukana na tatizo hili sio tu kutoa adhabu ya kuwafukuza watu hawa bali pia kuchukua hatua katika kuimarisha uchumi wa nchi” amesema Waziri Membe wakati anajibu swali la Mbunge wa Matemwe, Kheri Khatib Ameir.

Membe amelieleza Bunge kuwa Serikali itachukua hatua hizo “ ili tujiepushe na nchi ambazo hudhani kuwa kwa kuipa Tanzania misaada ya kiuchumi/ kifedha au kutoa misaada ya fedha kwa Tume za uchaguzi au viongozi wa vyama vya kisiasa inawapa mamlaka ya ya kutuingilia mpaka jikoni”

Kiongozi huyo wa Serikali amesema, shughuli za mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini na mabalozi wa Tanzania nje ya nchi zinaongozwa na Mkataba wa Mahusiano ya Kidiplomasia wa Vienna wa mwaka 1961.

“Bila kuathiri haki na kinga zao za kibalozi, ni wajibu wa watu wote wenye haki na kinga hizo kuheshimu sheria na taratibu za nchi wenyeji. Pia wanao wajibu wa kutoingilia masuala ya ndani ya nchi hizo” amesema Waziri Membe wakati anajibu swali la Mbunge huyo.

Ameir amedai kuwa, imekuwa ni kawaida kwa baadhi ya mabalozi wa nchi za nje kuwa karibu na vyama vya upinzani uchaguzi unapokaribia hivyo akaiuliza Serikali kama hali hiyo haihatarishi uhuru na usalama wa nchi, na kwamba Serikali inachukua hatua gani.

No comments: