Thursday, October 15, 2009

CHADEMA wamkanya Mwakyembe

• Wafananisha malumbano yake na kundi la Ze Komedi


na Gordon Kalulunga, Kyela




CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Mbeya, kimemtaka Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe kuacha mara moja kulumbana na wale anaowaona ni kikwazo kwake badala yake akae na wananchi waliomchagua kupanga mipango ya maendeleo.

Ushauri huo ulitolewa na viongozi wa chama hicho mkoani Mbeya katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Soko Jipya mjini hapa, baada ya kufungua tawi la chama hicho eneo la Ndandalo, Kata ya Mpakani.

Wakizungumza na wananchi wa mji mdogo wa Kyela, viongozi hao wa CHADEMA walioongozwa na mjumbe wa mkutano mkuu wa taifa, Edo Makata, walisema inashangaza kuona jimbo hilo linajipatia umaarufu kutokana na viongozi wao kulumbana kwenye vyombo vya habari, huku wakisahau majukumu waliyokabidhiwa na wananchi waliowachagua.

Makata alisema Jimbo la Kyela lina rasilimali nyingi ikiwa ni pamoja na Ziwa Nyasa ambalo lingeweza kuwanufaisha wananchi, lakini kutokana na viongozi waliopo kutojali maendeleo na mustakabali wa jimbo hilo, wamebakiwa na kazi ya kulumbana kwenye vyombo vya habari.

“Viongozi mliowapa dhamana ili mshirikiane nao kwa ajili ya mustakabali wa Wilaya ya Kyela, wamebakiwa na kazi ya kulumbana kwenye vyombo vya habari badala ya kukaa nanyi kujadili maendeleo, hivyo mnapaswa kuwakataa wakija tena kuomba kura kwenu maana wanaoufanya ni utoto.

“Tulikuwa tunawategemea kuwa tumewachagua kwa ajili ya kuzungumzia maendeleo ya Wilaya ya Kyela, lakini wamebaki kusingiziana utoto na huu ni msiba kwa wana Kyela, na hatupaswi kulishangilia hili, kwani watoto wetu hawana hata madawati na mipango ya maendeleo ya wilaya ikiendelea kuzorota,” alisema Makata.

Sanjari na hayo, alisema Dk. Mwakyembe hapaswi kuendelea kuongoza jimbo hilo kutokana na kushindwa kutekeleza ahadi zake na kuimba pambio za ufisadi huku akishindwa kuwataja kwa majina mafisadi hao, jambo ambalo linaonekana kuwa kama mchezo wa kuigiza wa kundi la Ze Orijino Komedi.

Makata alisema CHADEMA haina ubaguzi wowote, lakini hali inayoonyeshwa na watu walioko ndani ya CCM kuwa wanapambana na ufisadi si kweli na kwamba kama kweli wao si washiriki wa ufisadi huo, wanapaswa kuwataja kwa majina kuliko kuendelea kulalamika kwenye majukwaa huku wakiwa wamesahau majukumu yao.

Naye mwanachama wa CHADEMA aliyewahi kulitikisa Jimbo la Mbeya Vijijini, Sambwee Shitambala, ambaye pia ni wakili wa kujitegemea jijini Mbeya, alisema umefika wakati wa wananchi wa Kyela kukasirika kwa kuchezewa na viongozi wao ambao wameshindwa kujadili nao masuala ya maendeleo.

“Mahitaji muhimu ya nchi ni pamoja na uongozi bora, lakini viongozi wenu wanashindwa kujadili nanyi maendeleo kwa sababu si viongozi bora, na Kyela imekuwa maarufu sana na viongozi wenu ni maarufu kuliko hata Rais Obama (Rais wa Marekani), lakini umaarufu wao ni mabishano na kusemana, si maendeleo,” alisema Shitambala.

Aidha, alieleza kuwa kila kukicha viongozi waliowachagua wanawaza kujitafutia umaarufu wao binafsi badala ya kushirikiana na wananchi waliowachagua kujiletea maendeleo na badala yake wamekuwa mabingwa wa kusemana.

“Viongozi wenu wamekuwa bize kusingiziana kwa kusema huyu anajipendekeza kwa mafisadi na wengine wanasema huyu anajipendekeza kwa CHADEMA, maana hoja ya kukemea ufisadi ni yetu CHADEMA, hivyo mnatakiwa kukasirika wananchi wa Kyela na kuwakataa wakati wa uchaguzi.

“Wale mliowachagua hawasimamii maendeleo mliyowaambia kuwa mnayahitaji katika wilaya yenu ya Kyela, bali wamebaki kusimamia mambo yao, na ujumbe huu muufikishe kuwa waache kutangatanga huko Arusha, Singida na kwingineko, wanapaswa kuwa Kyela na kujadili masuala ya maendeleo ya Kyela,” aliongeza Shitambala.

Huku akishangiliwa na wananchi waliokuwa wamehudhuria mkutano huo, Shitambala aliendelea kuwa, umefika wakati wa kuwakataa viongozi hao kwa sababu tayari wamewasaliti kwa kutotimiza ahadi zao na kubaki kujitafutia umaarufu wakati maendeleo jimboni kwao yakibaki kudidimia.

“Mmekuwa mkihongwa mashati ya kijani na kofia kwenye chaguzi mbalimbali jambo ambalo linatia hasira sana, yaani mnaambiwa kuwa hamna uwezo wa kujinunulia nguo jambo ambalo linatia hasira sana, hivyo wananchi mnapaswa kuwachukia viongozi hawa na kuwakasirikia, na hili ni onyo la mwisho wasipojirekebisha wakataeni na hapa sichochei vurugu maana tumechoshwa kuona wananchi wa Kyela wakiendelea kuchezewa,” alisema Shitambala.

Mkutano huo umefanyika wiki moja baada ya viongozi hao kuimarisha chama chao katika Wilaya ya Mbozi, eneo la mji mdogo wa Tunduma ambako walivuna wanachama wapya 175 na sasa viongozi hao wanatarajia kwenda kuhutubia katika mikoa ya Mara, Singida na kwingineko kwa ajili ya kuimarisha chama chao.

Naye Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Kyela, Erick Sata, alisema chama chake kinazidi kuimarika kutokana na wananchi wengi kuchoshwa na ubabaishaji unaofanywa na viongozi waliopewa dhamana ya kuwaongoza.

No comments: