Tuesday, September 1, 2009

Kompyuta 32 zaibwa Muhimbili


Muhimbili.



Watu wasiojulikana wameiba kompyuta 32 katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili (MUHAS) cha jijini Dar es Salaam.

Kuibwa kwa kompyuta hizo kumekuja siku kadhaa baada ya majambazi kuvamia ofisi ya Taasisi ya Elimu Nchini (TIE) jijini Dar es Salaam na kuiba kompyuta zaidi ya sabini na magari mawili.

Mapema Agosti 6 mwaka huu, kundi la majambazi lilivamia ofisi za TIE usiku wa manane na kupora mali hizo zenye thamani ya mamilioni ya fedha.

Watu watano waliokuwa wakituhumiwa kwa ujambazi na uporaji huo akiwemo mwanamke alikamatwa na polisi na baadaye kufikishwa mahakamani.

Akizungumzia tukio la wizi hapo Muhimbili, Ofisa Habari wa chuo hicho, Hellen Mtui, alisema tukio hilo limeripotiwa Kituo cha Polisi Salenda Bridge na kwamba baadhi ya wafanyakazi wa maktaba hiyo wanaendelea kuhojiwa kuhusiana na wizi huo. Alisema watumishi kadhaa wamekwishahojiwa na polisi na kwamba polisi wanaendelea kuwahoji wengine pia.

Aliwataja waliokwishahojiwa kuwa ni Mkurugenzi wa Maktaba hiyo, Msaidizi wake na baadhi ya walinzi.

Mtui, alisema kompyuta zilizoibwa zilikuwa mpya baada ya kununuliwa kwa matumizi ya Kitengo cha Kompyuta (ICT) katika maktaba hiyo, na kuwasaidia wanafunzi wa chuo hicho kusoma vitabu mbalimbali kwa kutumia kompyuta. Mtui, alisema baada ya wizi huo uliotokea wiki iliyopita walitoa taarifa polisi na ndipo walipofika kwa ajili ya upelelezi na kuanza kuwahoji baadhi ya wafanyakazi wa maktaba hiyo. Alisema hakuna hata mfanyakazi anayeshikiliwa na polisi kwa tuhuma za wizi huo kwa kuwa wamekuwa wakiitwa polisi na kuhojiwa kisha kuachiwa.

"Polisi wamekuwa wakimwita mfanyakazi wanayeona wanahitaji kupata maelezo yake na kisha wanamwachia na hadi sasa hatujui upelelezi wao umefikia wapi," alisema.

Aliongeza kuwa inahisiwa wizi huo ulitokea usiku wa manane kutokana na madirisha ya maktaba kukutwa wazi majira ya asubuhi. "Hakuna mlango hata mmoja uliovunjwa na wezi hao," alisema. Alisema wezi hao walichukua kompyuta mpya tu na kuziacha za zamani zilizokuwepo katika maktaba hiyo.

Alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alielekeza aulizwe Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala.

Kamanda wa Ilala, Faustine Shilogile, alipoulizwa aliahidi kuzungumzia tukio hilo leo kwa kuwa hadi jana alikuwa mgonjwa.

No comments: