Tuesday, September 1, 2009

Makachero Uingereza wawasilisha tuhuma za Chenge

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema makachero wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) cha nchini Uingereza, wamewasilisha serikalini taarifa za uchunguzi kuhusu tuhuma za kusaini mikataba ya kifisadi zinazomkabili Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge ).

Profesa Lipumba alisema anasikitishwa kuona hadi sasa Serikali bado haijamshughulikia Chenge kwa tuhuma zinazomkabili.

Alitoa madai hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuwasilisha mada katika semina ya kujadili “Dira ya Maendeleo ya Tanzania Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010”, iliyofanyika katika Ukumbi wa jengo la Mayfair Plaza, jijini Dar es Salaam jana.

Semina hiyo iliyovishirikisha vyama 17 vya siasa nchini, iliandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Lipumba alisema licha ya SFO kupeleka kwa serikali taarifa kuhusu uchunguzi wa mikataba hiyo katika sekta ya madini na ule wa mwaka 1999 uliohusu ununuzi wa rada kutoka Kampuni ya British Aerospace (BAE Systems) ya Uingereza, unaodaiwa kuwa na harufu ya rushwa, hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na Serikali dhidi ya Chenge.

Alisema mikataba hiyo ilitiwa saini na Chenge alipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mfanyabiashara aliyetumika kama wakala katika biashara hiyo, Sailesh Vithlan alikiri mbele ya makachero wa SFO kwamba, aliingiziwa kwenye akaunti moja Uswisi Sh bilioni 12 kwa ajili ya kamisheni.

Malipo hayo ya ‘mlango wa nyuma’, yanadaiwa kufanywa katika mazingira ya kuichagiza serikali kununua rada hiyo.

“Nasikitika kwa Serikali haijamshughulikia Mheshimiwa Chenge kwa kushiriki kusaini mikataba ya kifisadi wakati SFO wameileta yote serikalini,” alisema Profesa Lipumba.

Rada hiyo ya kijeshi iliyonunuliwa na Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa mwaka 2002, iliigharimu serikali ya Tanzania Pauni za Uingereza milioni 28 (Sh. bilioni 50).

Waziri Mkuu wa Uingereza wa wakati huo, Tony Blair, aliunga mkono ununuzi wa rada hiyo ingawa aliyekuwa Waziri wake wa Maendeleo ya Kimataifa, Clare Short aliupinga, baadaye alijiuzulu wadhifa wake.

Aprili 12, mwaka jana, gazeti la The Guardian la Uingereza liliandika kuwa, katika uchunguzi wa SFO iligundulika akaunti moja inayohusishwa na Chenge ikiwa na zaidi ya dola za Marekani milioni moja (Sh. bilioni 1.2) iliyopo kwenye Kisiwa cha Jersey.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, SFO ilimchukulia Chenge kuwa mtu anayeweza kuwa shahidi muhimu katika uchunguzi wa zabuni ya ununuzi wa rada hiyo.

Gazeti hilo liliandika kwamba, SFO ingeanza upya kufanya uchunguzi kuhusu fedha hizo ili kuangalia iwapo zina uhusiano na zile zinazoaminika kutolewa kwa njia ya rushwa wakati Tanzania iliponunua rada hiyo.

Uchunguzi wa SFO ulianza Mei, mwaka jana ingawa wa awali ulionyesha kuwa moja ya mambo yaliyokuwa yakifuatiliwa ni kujua iwapo fedha zinazoaminika kuwa za Chenge zina uhusiano na zile zilizotoka katika Kampuni ya BAE Systems inayotuhumiwa kuinyonya Tanzania kwa kuiuzia rada mbovu kwa bei kubwa kuliko ilivyotakiwa. The Guardian katika habari yake hiyo iliyowekwa katika mtandao wa intaneti, liliripoti kuwa, taarifa hizo zilikuja ikiwa ni miaka minne tangu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kwa kushirikiana na SFO na taasisi za uchunguzi za Uswisi na Jersey zilipoanza kuchunguza kuhusu kashfa nzima ya ununuzi wa rada.

Gazeti hilo lilimkariri Chenge akikiri kwamba, fedha hizo ni zake na akatumia fursa hiyo kukanusha kuwapo kwa uhusiano wowote kati ya fedha hizo na kashfa nzima ya ununuzi wa rada, uliofanywa wakati yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Jambo la wazi linalotaka kuonekana hapa ni kwamba mimi nilipokea kwa lengo la kujinufaisha mwenyewe fedha za rushwa kutoka BAE. Huu ni uongo,” alisema Chenge, ambaye aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari vya hapa nchini akiziita fedha hizo kuwa ni "Vijisenti".

Aidha, gazeti hilo lilimkariri Chenge akisema kuwa, wakati rada hiyo ilipokuwa ikinunuliwa, yeye alihusika kwa kiwango kidogo sana katika mchakato mzima, kwani jambo hilo lilishughulikiwa na wizara nyingine na uamuzi ukaidhinishwa na Baraza la Mawaziri.

Mbali ya hilo, gazeti hilo kumkariri Mwanasheria wa Chenge anayeishi Cleveland, Ohio, nchini Marekani, J Lewis Madorsky, akikanusha kwa niaba ya mteja wake huyo, kuwapo kwa uhusiano wowote kati ya fedha zake na tuhuma zozote.

“Wakati tukitambua kuwa masuala hayo yalitokea muda mrefu uliopita, tunaweza tu tukathibitisha kuwa, tuhuma zozote za ukiukwaji wa sheria, ukiukwaji wa maadili, kutenda isivyo sawa na mambo mengine ya hivyo dhidi ya mteja wetu ni mambo ambayo kimsingi tunayakanusha kwa nguvu kubwa,” alisema mwanasheria huyo wa Chenge.

Hata hivyo, gazeti hilo liliandika uchunguzi huo dhidi ya Chenge unamfanya yeye kuwa tu shahidi muhimu, kwani wanailenga zaidi BAE, ambayo inadaiwa ilimlipa wakala mmoja wa Tanzania mamilioni ya fedha ili kujenga ushawishi wa rada iliyokuwa ikiiuza kununuliwa.

Wakala huyo ambaye amekuwa akitajwa kwa muda mrefu na ambaye sasa anaaminika kukimbia nchini na kutafutwa na polisi wa kimataifa ni, Shailesh Vithlani.

Nipashe iliwasiliana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba ili kuzungumzia suala hilo, hakupatikana na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi, ilipokelewa na mtu aliyejitambulisha kuwa mwanaye, ambaye alisema mama yake yuko nje ya nchi na anatarajiwa kurejea nchini kesho.

Vilevile, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe naye alipotafutwa jana hakupatikana na hata alipopigiwa simu yake mkononi, mara zote ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

Vilevile Mkurugenzi wa Mashtaka wa Serikali (DPP), Eliazer Felesh alipotafutwa jana hakupatikana na alipopigiwa simu yake ya mkononi, ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

Awali, akizungumzia “Dira ya Maendeleo ya Tanzania Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010”, Profesa Lipumba alimshauri Rais Jakaya Kikwete kuanzisha mazungumzo na wadau ili kujadili suala hilo.

No comments: