Friday, July 24, 2009

Serikali yamsafisha rasmi Mkapa

Yaahidi kurejesha gharama zote alizotumia kuwekeza Kiwira


na Hellen Ngoromera, Dodoma




HATIMAYE serikali imetimiza azma yake ya kuurejesha mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira ambao kwa muda mrefu umekuwa ukihusishwa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa.

Hata hivyo, wakati uamuzi huo ukitangazwa bungeni jana na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, imebainika kwamba, Kampuni ya ANBEN Ltd inayomilikiwa na Mkapa na mkewe Anna, tayari ilikuwa imeshapoteza dhamana ya umiliki wa mradi huo tangu Januari mwaka 2005 kutokana na kushindwa kulipia fedha za hisa katika Kampuni ya TanPower Resources Company (TPR).

Akitoa tamko hilo bungeni jana, Ngeleja, alisema ANBEN ilinyang’anywa hisa zake katika mgodi huo, tangu Januari 10, 2005 baada ya kushindwa kulipia hisa ilizokuwa imezichukua wakati wa usajili wa TPR ambayo ilikuwa na hisa katika Kampuni ya Kiwira Coal Mines Limited (KCML) inayoendesha mradi huo wa makaa ya mawe hadi wakati huu.

“Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Kampuni ya TPR inaanzishwa, wanahisa wake na hisa zao zikiwa kwenye mabano, walikuwa ANBEN Limited (200,000), DevConsult International Ltd (200,000), Universal Technologies Ltd (200,000), Choice Industries Ltd (200,000) na Fosnik Enterprises Ltd (200,000).

“Januari mwaka 2005 (siku 13 tangu kuanzishwa kwa TPR), ANBEN iliondolewa kuwa miongoni mwa wamiliki wa hisa kwa vile haikuweza kulipia hisa ilizokuwa imechukua wakati wa usajili wa TPR, hivyo wamiliki wa TPR waliobaki walikuwa wanne,” alisema Waziri Ngeleja.

Alibainisha kuwa, mkataba wa kuendeleza mradi wa Kiwira kati ya serikali na Kampuni ya KCML, uliingiwa Machi 24, 2006 kwa kutia saini makubaliano ya makusudio (Agreement of Intent-Aol) na mikataba ya Power Purchase Agreement (PPA), Implementation Agreement (IA), Escrow Agreement (EA), Transmission Line Facilities Agreement (TLFA) na Facility Transer Agreement (FTS), ilitiwa saini Agosti 2006.

Akitangaza uamuzi huo wa serikali jana bungeni, Waziri Ngeleja alisema serikali imeamua kuurudisha mgodi huo na mradi wa kuchimba makaa ya mawe mikononi mwake kwa makubaliano ya kurudisha gharama zote zilizotumiwa na KCML, endapo itathibitika kuwa za kweli.

“Kwa kuwa kumekuwepo na kasoro katika uendeshaji wa mradi huu, zilizosababisha hisia mbalimbali miongoni mwa wananchi na kwa kuwa hisia zilizoibuka kuhusu ubinafsishaji wa Kampuni ya KCML zimeathiri sana mazingira ya kampuni kuweza kutekeleza na kutimiza malengo yake kama yalivyoainishwa kwenye mkataba, na hivyo kuiathiri nchi, ikiwa ni pamoja na kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi 500 kwa zaidi ya mwaka sasa inayofikia sh bilioni 1.5, serikali imeona bora ifanye hivyo,” alisema Waziri Ngeleja.

Alisema serikali imeanza mchakato wa kupata utaratibu muafaka wa kuendesha mradi kama ilivyokusudiwa kwa kuangalia fursa mbalimbali, mojawapo ikiwa kuingia mkataba wa uendeshaji (Management Contract) na kampuni itakayopewa mamlaka ya kujenga na kuendesha mradi huo chini ya mkataba wa uendeshaji na mkandarasi atapewa jukumu la kujenga uwezo wa mashirika ya Stamico na TANESCO ili kuyawezesha kumiliki na kusimamia mradi.

Akizungumzia historia ya mgodi huo, alisema ujenzi wake ulianza mwaka 1983 na kukamilika mwaka 1988 kwa ushirikiano kati ya Serikali ya China na Tanzania ambapo gharama halisi za ujenzi wake wakati unakamilika zilikuwa sh bilioni 4.29.

Aliongeza kuwa, pamoja na mambo mengine, uchimbaji wa makaa ya mawe na uzalishaji wa umeme ulianza rasmi Novemba 1988 ambapo makaa yaliyochimbwa, yalitumika kuzalisha umeme kwa ajili ya matumizi ya mgodi wenyewe na ziada iliyopatikana ya makaa ya mawe, iliuzwa kwa kiwanda cha kutengenezea saruji cha Mbeya.

“KCML kama mashirika mengine ya umma, iliwekwa kwenye mchakato wa kubinafsishwa kupitia GN Na. 543 ya tarehe 22 Agosti 1997 kwa kuzingatia kifungu Na 48 cha The Public Corporation Act 1922. Hadi KCML inabinafsishwa, ilikuwa inajiendesha kwa hasara,” alisema Waziri Ngeleja.

Alisema kutokana na msimamo wa serikali kuwa miradi yote iliyokuwa inapata msaada kutoka Serikali ya China, kipaumbele kipewe kampuni za Kichina pale inapobinafsishwa, ndipo Aprili mwaka 1999 katika jitihada za kufufua mgodi huo, serikali iliingia makubaliano na kampuni ya Kichina, Hunan International Economic and Techinical Cooperation (CHITEC) na katika makubaliano, ingemiliki hisa asilimia 62 na serikali 38 kwenye mgodi huo.

Alibainisha kuwa, baada ya CHITEC kufanya uchambuzi wa kina kuhusu mradi wa makaa ya mawe wa Kiwira na soko lake, walibaini kuwa mradi huo pekee haukuwa na manufaa kibiashara, hivyo walilazimika kuunganisha na mradi wa kuzalisha umeme.

“Hata hivyo, mradi ulishindwa kusonga mbele kutokana na kukatishwa tamaa na TANESCO ambao inasemekana wakati huo walisema walikuwa na umeme wa ziada (excess power) na hawakuhitaji umeme kutoka mradi wa CHITEC na kusababisha kampuni hiyo kujitoa na baadaye serikali iliamua kuubinafsisha kwa wawekezaji binafsi katika mkakati wa kuukwamua,” alisema Ngeleja.

Alibainisha kuwa, wakati Kampuni ya KCML inasajiliwa, ilikuwa na mtaji wa sh milioni 30 (hisa 30,000, zenye thamani ya sh 1,000 kila moja).

Alisema kampuni hiyo ilimilikiwa na serikali kwa asilimia 100, kupitia STAMICO na baadaye mwaka 1997, ilihamia kwa msajili wa hazina na kupata namba GN. Na 647/1997.

Kuhusu uamuzi wa serikali kuibinafsisha KCML, kwa Kampuni ya Tan-Power Resouces Company Limited, alisema kampuni hiyo ambayo ilikuwa chini ya Stamico, ilishindwa kujiendesha kwa faida kwa sababu ya uzalishaji wa chini wa makaa ya mawe kati ya tani 20,000 na 80,000 badala ya tani 150,000 na 200,000 kwa mwaka.

Alibainisha kuwa mwaka 2005, Kampuni ya TPR, ilinunua hisa 700,000 za KCML kwa bei ya sh 1,000 kwa kila hisa moja, sawa na asilimia 70 ya hisa zote na serikali ilibakia na hisa 300,000 ikiwa ni asilimia 30 ya hisa zote.

Alisema malipo hayo, yaligawanywa katika awamu mbili, yaani kwa sh milioni 70, baada ya kusaini mkataba na salio la sh 630,000,0000, lingelipwa baada ya TPR kuanza kuendesha mgodi chini ya jina la Kiwira Coal and Power Limited (KCPL).

Kwa mujibu wa waziri huyo Kampuni ya TanPower Resources Company ilisajiliwa na Msajili wa Makampuni Desemba 29, 2004 na kupewa hati ya usajili namba 51080.

“Mtaji wake wakati wa kampuni inaanzishwa, ilikuwa sh bilioni 2, hisa za kampuni milioni 2 za sh 1,000 kwa kila hisa. Julai 9 2008, Kampuni ya TPR iliongeza mtaji na kufikia sh bilioni 15 na kuwa na hisa 15,000,000 za sh 1,000 kila moja,” alisema.

Uamuzi wa serikali kutaka kuutwaa mgodi huo, mara ya kwanza ulitangazwa bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati akijibu maswali ya papo kwa papo kutoka kwa wabunge.

Alisema serikali ingetwaa mgodi huo kwani umekuwa chanzo cha kusakamwa kwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa, akihusishwa na ufisadi wa kujitwalia kienyeji rasilimali hiyo ya taifa kwa bei ya kutupa.

Huku akijenga hoja kwamba Mkapa si fisadi, Waziri Mkuu, aliliambia Bunge kuwa kiongozi huyo mstaafu, anayeheshimika kimataifa ni msafi na alilitumikia taifa kwa uadilifu mkubwa.

Akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia mjadala wa makadirio ya matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2009/10, Pinda alisema hasemi hayo kwa nia ya kumtetea Mkapa, ila anazungumza kwa kuangalia kazi aliyofanya akiwa madarakani.

Huku akitoa changamoto kwa wanaomwita Mkapa fisadi, wautaje kwa kuonyesha wazi na kuuliza kama kuna ndege zinazoruka, zenye jina la Mkapa, Pinda alisema kama ni hisa za mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira ulioko mkoani Mbeya, ameamua zirejeshwe serikalini ili Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Madini Tanzania (Stamico) yatafute mwekezaji wa uhakika.

“Rais Mkapa kama kweli ni fisadi baba huyu sijui, tuone ufisadi ameuweka wapi? Ana maakaunti nje ya nchi? Ana mandege makubwa yanayoruka yameandikwa kwa jina la Mkapa?...Nasema bado ni mtu safi,” alisema Pinda na kuongeza:

“Lipo hili la Kiwira sawa. Tutalitolea maelezo, lakini suala alilofanya kwa jinsi gani aliingizwa huko ndiyo la kuangalia, inawezekana aliburuzwa tu.”

Pinda alisema nchi haiwezi kufika kokote kama marais watakuwa wanashambuliwa na kwamba, kila mtu ana uhuru wa mtizamo wake kuhusu suala lolote, lakini hawatakiwi kuanza kushambulia viongozi hao kiasi hicho.

Alisema kiongozi wa Tanzania hawezi kufikia kiwango cha ufisadi wa kutisha na kutoa mfano wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambayo Rais wake (bila kumtaja) alifikia kiwango cha juu cha ufisadi.

Pinda alisema ili kiongozi awe fisadi ni lazima awe dikteta wa kutisha mambo ambayo hayawezi kutokea Tanzania.

Alisema kimsingi matatizo ya Kiwira hayakuanza leo bali ni ya enzi za kale na kubainisha kuwa kama Mkapa angekuwa fisadi, mgodi huo usingefikia hatua ya kushindwa kuwalipa wafanyakazi wake mishahara kwa miezi 10 sasa.

Hii ni kauli ya kwanza ya serikali kutolewa hadharani juu ya mgodi wa Kiwira ambao umemweka Mkapa katika wakati mgumu kutokana na kutuhumiwa kwamba akiwa madarakani akishirikiana na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona, walijiuzia mgodi huo kwa bei ya kutupa.

Yona na Mkapa kupitia Kampuni ya TanPower Resources wanadaiwa kujiuzia mgodi huo wenye thamani ya sh bilioni 4 kwa sh milioni 700 tu, lakini kibaya zaidi wakatoa sh milioni 70 tu kisha wakakabidhiwa mgodi huo.

No comments: