Friday, July 24, 2009

Maalim Seif: Waraka wa Wakatoliki hatari

• Ahoji nguvu inayotumika kuutetea waraka


na Waandishi Wetu
MALUMBANO dhidi ya waraka uliotolewa na Kanisa Katoliki yamezidi kushika kasi baada ya Chama cha Wananchi (CUF), kuupinga na kumtetea mkongwe wa siasa nchini, Kingunge Ngombare-Mwiru (CCM) kwamba anaonewa kwani waraka huo ni hatari na unaweza kuigawa nchi katika misingi ya dini.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa hapa nchini, makao makuu ya chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam.

Hamad alisema waraka huo una kipengele kinachosema kinawaandaa na kuwadhibiti viongozi wa kisiasa, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linachanganya masuala ya dini na siasa.

Alibainisha kuwa, hivi sasa kumekuwa na jitihada kubwa za watu mbalimbali kuhakikisha waraka huo unakubalika kwa kila Mtanzania, na baadhi ya waandishi wa habari wamejikuta ama kwa kujua au kutokujua wakifanya kazi hiyo aliyoita kuwa ni ya hatari kwa taifa.

Aliongeza kuwa, watu wanaofanya jitihada hizo, wana ajenda zao nyuma ya pazia na hawapaswi kupewa nafasi kwa kuwa waraka huo una upungufu na ukiachiwa usambae, unaweza kuiingiza nchi katika misingi ya kidini ambayo waasisi wa taifa waliikataa.

“Nimeusoma waraka ule na nimeona una upungufu, hasa katika kile kipengele kinachosema kuwaandaa na kuwadhibiti viongozi wa kisiasa, sasa inawezekana vipi kwa viongozi wa dini kuwadhibiti viongozi wa kisiasa?” alihoji Hamad.

Aidha, alisema anashangazwa na baadhi ya watu kuanza kumshambulia Kigunge kuwa ametumwa na mafisadi kwa kutoa maoni yake kuhusu waraka huo ambao aliuelezea kuwa umedhamiria kuwapendelea zaidi Wakristo.

Alisema alichokisema Kingunge kinatakiwa kipingwe kwa hoja na wala si kumhusisha na kuwatetea mafisadi, kwani kwa kufanya hivyo ni kukwepa kujadili upungufu wa waraka ambao unalenga kuigawa nchi kwa misingi ya dini.

“Kwa nini wana dini waanze kumsakama Kingunge kwa kutoa maoni yake kuhusu waraka wao? Tunapaswa kuwa makini na viongozi wa dini wasije kuipeleka nchi kusikostahili,” alisema Hamad.

Aidha, alisema tatizo kubwa linaloonekana hivi sasa ni kutokuwapo kwa uongozi imara wa nchi, jambo linalowafanya baadhi ya watu kila kukicha kujiamulia mambo yao bila kuhofu athari wanayoitoa katika jamii.

Alisema kitendo cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuingiza suala la Mahakama ya Kadhi katika ilani yao ya uchaguzi wa mwaka 2005 na hivi sasa kushindwa kuitekeleza, ni ushahidi tosha wa kukosekana kwa viongozi ndani na nje ya chama hicho.

Aliongeza kuwa, tatizo hilo la CCM ndilo linalowafanya hivi sasa wahangaike huku na huko kuhakikisha wanapata uungwaji mkono na makundi ambayo waliyapa ahadi, lakini wameshindwa kuzitekeleza mpaka hivi sasa.

“Wacha CCM watafune kokoto zao, Mahakama ya Kadhi ni mtoto wao, wacha wamlee, kwa nini wanatafuta mtu wa kumlea wakati wao ndio wanaohusika?” alihoji Hamad.

Aidha, alisema kuwa ni vema Watanzania wakawa macho, kwani kuna baadhi ya watu wameanza kuififisha vita ya ufisadi kwa kuingiza hoja ya kidini, hasa kwa kutumia waraka wa Kanisa Katoliki.

Alisema kama Watanzania watahadaika na mbinu chafu hizo, kuna kila dalili kila siku nchi kuendelea kudorora na viongozi wa CCM kutawala kwa hila mbalimbali.

“Tunapaswa tuwe makini, hawa jamaa wanataka kutuingizia misingi ya udini ili tusahau vita dhidi ya ufisadi, tuna wajibu wa kuzuia jambo hili lisiendelee,” alisema Hamad.

Naye Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba amesema hakuunga mkono na wala hatounga mkono waraka huo, uliobarikiwa na Baraza la Maaskofu Tanzania kwa kile anachodai kuwa, utakuwa wa kibaguzi na unaweza kuigawa nchi na kuleta mgawanyiko wa kisiasa.

Akizungumza mjini Bukoba alipokuwa kwenye ziara ya Operesheni Zinduka inayoendelea mkoani humo, Profesa Lipumba alisema waraka huo ambao ni mpango wa kichungaji wa kuhamasisha jamii kuelekea katika uchaguzi, ni wa kibaguzi na kwamba unaweza kuwagawa Watanzania katika makundi na kusababisha ghasia nchini.

Aidha, alisisitiza kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi kwa kuwa itaweza kurahisisha na kutatua matatizo mengi na kuongeza kuwa, katika nchi ambazo zimeanzisha mahakama hiyo, hakuna matatizo yaliyotokea kwa kuanzishwa kwake.

Alisema alishangazwa na kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa Mahakama ya Kadhi ianzishwe lakini iwe nje ya serikali kwa kujiendesha yenyewe bila kuegemea dola.

Lipumba alisema mahakama hiyo, inatakiwa kuanzishwa ikiwa ndani ya serikali chini ya uangalizi wa serikali ili kuwe na utaratibu mzuri usiokuwa na migongano.

“Hakutakuwa na fujo yoyote ile, na mfano mzuri ni katika nchi ya Kenya ambayo kuna kadhi 17, lakini hadi leo hakuna matatizo ya kidini ambayo yametokea kwa kusababishwa na kadhi,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema ni vyema serikali ikaruhusu kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu (OIC) ambayo itakuwa ikisaidia katika mambo mengi ambayo ni pamoja na kupata misaada mbalimbali ya kiuchumi.

1 comment:

Binomutonzi said...

Seif na Lipumba wanachanganya maana na lengo la waraka. Hauna misingi yoyote ya dini. Unalenga ktk kuelimisha umma kuhusu kuitendea haki nchi yao.

Seif asipinge ukweli kwamba dini ina wajibu wa kuwaandaa na kuwathibiti viongozi. Ni wajibu wao kufanya hivyo na uwezo wanao maana hata serikali ni mamlaka iliyotoka kwa Mungu, hivyo watu wa Mungu wana nafasi ya kuwaandaa. Hawaoni jinsi viongozi wa dini walivyomwandaa na kumthibiti Nyerere mpaka kifo chake hajawahi kuiibia nchi, wakati angetaka angeamua kuiuza nchi hakuna ambaye angemzuilia. Hakuna mamlaka nyingine iliyomdhibiti bali viongozi wa dini. Alifundwa na kanisa kuhusu haki na utawala bora. Dini lazima ishirikiane na serikali ktk kuutawala umma. Hao watu waambie wasitupotoshe. Amina