Friday, July 24, 2009

Pinda ahofia muungano kuvunjika

na Hellen Ngoromera, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, ameonya kuwa suala la Muungano likiendelea kujadiliwa kwa mitazamo ya ubinafsi hasa na upande wa Zanzibar, linaweza kusababisha serikali ya Tanzania na ile ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kufarakana.

Alitoa kauli hiyo jana bungeni, alipokuwa akijibu maswali ya papo kwa papo.

Akijibu swali la Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM), aliyetaka kujua msimamo wa serikali kuhusu kauli za viongozi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuhusu Muungano, Pinda alisema msingi wa maneno yote hayo yanayohatarisha Muungano ni mafuta na gesi ambayo hata Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake hivi karibuni, aliwahi kusema suala hilo linazungumzika kwani mafuta yenyewe hayajapatikana.

“Nilidhani swali hili litatoka kwa wenzetu wakina Mnyaa, lakini kwa sasa yeye na wenzake wapo kimya, hiyo inaashiria kuwa walishirikiana kututupia maneno, mambo haya hayana sababu ya kujitokeza, kwa nini tutupiane maneno katika hili.

“Mi huwa najiuliza, ipo siku pande hizi mbili zitafarakana, tuuvunje Muungano halafu tuone nani atakayeumia au kufaidika,” alisema Pinda.

Huku akionyeshwa kukerwa na maswali ya mara kwa mara kuhusu Muungano, Pinda alisema baadhi ya maneno ya Wazanzibari yanatia simanzi, hivyo wanatakiwa kujiuliza ni upande gani utaathirika iwapo Muungano utavunjika.

Kwa mujibu wa Pinda baada ya mambo hayo, kuna kamati iliundwa ili kuzungumzia suala hilo na Juni 23, mwaka huu, iliwasilisha ripoti, lakini badala ya kusubiri hali itakavyokuwa kuhusu suala hilo la mafuta, watu wengi wa Zanzibar wameamua mambo mengi.

“Kama alivyoshangaa Selelii, mimi pia nimeshangaa kuhusu suala hili, pamoja na mambo yote ni imani yangu kuwa Watanzania tutaendelea kuuenzi Muungano,” alisema Waziri Mkuu.

Aliongeza kuwa, kama kuna matatizo yaliyopo katika suala hilo, kinachohitajika ni kukaa na kuzungumza ili suluhisho lipatikane.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje itaendelea kusimamia masuala yote yanayohusu Tanzania katika masuala ya kimataifa.

Alitoa msimamo huo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chwaka, Yahya Kassim Issa (CCM) aliyetaka kujua ni kwa nini wizara hiyo inaiwakilisha Zanzibar katika masuala ya nje wakati katiba haionyeshi hivyo.

Alibainisha kuwa, suala hilo litaendelea kuwa katika chini ya wizara hiyo na kwamba iwapo SMZ inataka ijitegemee katika masuala ya kimataifa, inaweza kujaribu ili ione kama itafanikiwa.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Pinda, hafahamu mbunge huyo alikuwa na maana gani kuzungumza hilo na kusisitiza kuwa kama Zanzibar inataka kujaribu, ifanye hivyo ili Watanzania waone kama watafanikiwa.

No comments: