Monday, June 15, 2009

Viongozi wa dini wazidi kumkalia kooni Mkulo

Exuper Kachenje na Salim Said


VIONGOZI wa dini za Kiislamu na Kikristo jana waliendelea kumkalia kooni Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, licha ya kueleza kuwa ufisadi katika baadhi ya taasisi hizo ndio uliofanya serikali itangaze katika bajeti yake kuwa inazifutia msamaha wa kodi.


Akijaribu kutuliza viongozi wa dini waliokasirishwa na kitendo cha serikali kufuta misamaha ya kodi kwa taasisi za dini na mashirika yasiyo ya kiserikali, Waziri Mkulo alisema baadhi ya vyombo hivyo vimekuwa vikitumia vibaya misamaha hiyo na kwamba ameiagiza Mamlaka ya Mapato (TRA) kutoa orodha ya vitu ambavyo vitasamehewa kodi.


Aidha alisema vitu vyote vya huduma, ikiwa ni pamoja na vya hospitali na shule havitatozwa kodi na kwamba tayari ameiagiza TRA, kuandaa orodha ya vitu vyote vitakavyotozwa na vitakavyosamehewa ushuru. Katika hotuba yake ya Alhamisi, Mkulo alisema vitu ambavyo havitatozwa kodi ni vile vya huduma za kiroho tu.


Lakini viongozi wa dini walielezea kauli hiyo ya Mkulo kuwa haina msingi na kwamba angekutana kwanza na wadau kabla ya kutangaza kufuta misamaha hiyo kwenye bajeti yake ya mwaka 2009/10 aliyoisoma bungeni mjini Dodoma Alhamisi iliyopita.


Wakizungumza na gazeti hili jana, viongozi hao wa dini walisema uchafu na ukosefu wa maadili upo takriban katika kila sekta, lakini wakasema hiyo haifanyi wahusika wote wastahili kuadhibiwa na kufafanua kuwa Mkulo anaweza kutangaza taasisi za dini ambazo zimedanganya katika kupata misamaha ya kodi.


Askofu Msaidizi wa Kanisa Katokili Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Method Kilaini aliiambia Mwananchi jana kuwa kitu ambacho Mkulo na serikali yake walitakiwa kufanya ni kukutana na wadau na kuwaeleza uamuzi wao; mapungufu waliyoyaona pia kusikia maoni ya taasisi za dini.


"Kama kutangazwa majina ya wanaotumia vibaya misamaha, sisi hatuna shida atangaze tu," alisema.


Kilaini alisema: "Mkulo anapaswa kukutana na wadau na kuwafafanulia kuhusu hatua hiyo kabla ya TRA haijataja wale anaodai Mkulo wanaotumia vibaya misamaha hiyo.


Kama wabunge wamemwelewa kama sisi tulivyoelewa anategemea sisi tumwelewe vipi? Awaite wadau awafafanulie.


"Bado nasisitiza kuwa hatua hiyo si sahihi. Wabaya wapo kila mahali, lakini huwezi kutupa mtoto kwa sababu mkono wake umeingia maji machafu.


"Wanaovunja sheria wapo kila mahali huwezi kuhukumu wote kwa kosa la wachache. Katika taasisi za dini wapo wanaovunja sheria. Zipo taasisi hata makanisa yanayoanzishwa kwa lengo la kupata msamaha wa kodi na ilitakiwa serikali idhibiti hilo si kufuta kodi kwa wote."


Aliongeza kuwa ndani ya mfumo wa serikali kuna mapungufu na matatatizo mengi, akiyataja baadhi kuwa ni wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), majina ya walimu hewa na mengineyo.


"Ikiwa kasoro ya wachache, inahusisha wote basi walimu wangefutwa wote na pia serikali isingerudisha ruzuku kwa wafanyabiashara," alisema.


Kaimu mufti wa Tanzania, Sheikh Suleiman Gorogosi alisema kwa sasa hawawezi kuzungumza lolote hadi hapo waziri huyo atakapotoa orodha hiyo na baada ya wao kuichambua, ili kuona ni kwa kiasi gani imetoa nafuu kwa taasisi hizo au imezidi kuzikandamiza.


"Haya unauliza wakati orodha yenyewe haijatolewa; yeye si kafafanua; si kasema ameiagiza TRA kuandaa orodha hiyo na kuichapisha magazetini? Sisi tunaisubiri kwa hamu hiyo orodha yake," alisema Sheikh Gorogosi.


Alifafanua kuwa iwapo orodha hiyo itatoa unafuu kwa taasisi za dini, wao hawana tatizo. Lakini akaongeza kuwa ikiwa itazidi kuwakandamiza kwa kulazimisha ushuru hata kwa vitu vya huduma katika taasisi na mashirika ya dini, hawataikubali.


Naye Mchungaji John Magafu wa idara ya habari ya Jumuia ya Makanisa Tanzania (CCT) alisema kuwa taasisi za dini zinafanya kazi kwa uwazi, hivyo ni bora Mkulo akaweka wazi taasisi zinazotumia vibaya msamaha wa kodi kwa majina.


"Sisi tunafanya mambo kwa uwazi. Ili kuondoa utata unaotumika kuzikandamiza taasisi zote za dini, ataje wahusika wala si jambo la kututia hofu," alisema Mchungaji Magafu.


Alisema kimsingi kama Waziri Mkulo ana ushahidi, yupo huru kutangaza wale wanaotumia vibaya misamaha hiyo. Serikali isifanye kiini macho na kuaminisha wananchi kuwa mapato yake yanategemea zaidi taasisi na mashirika ya dini.


Katibu mkuu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda alisema hawataikubali orodha yoyote ambayo itataka vitu vya kutolea huduma katika taasisi na mashirika ya dini kutozwa ushuru.


Alisema Waislamu wanasikitika kuona hata misikiti inatozwa kodi wakati hakuna biashara yoyote inayofanyika ndani zaidi ya watu kuingia kufanya ibada na kusoma na baadaye kutoka.


Alisema suala la kutotozwa kodi kwa bidhaa na vitu vya huduma hususan vya kiroho, kiibada, hospitali na hata mashuleni ni haki ya waumini kwa sababu serikali imeshindwa kuwatosheleza katika huduma hizo.


"Kwa miaka mingi serikali imekuwa ikitunyanyasa kwa kututoza kodi katika vitu vya kiibada, kiroho na huduma, lakini kwa sasa hatutakubali kwa sababu ni haki yetu na tutaidai," alisema Sheikh Ponda.


Kauli za viongozi hao wa dini ni mwendelezo wa mjadala mkali ulioibuka hata kabla ya hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2009/10 iliyotolewa bungeni Alhamisi iliyopita baada ya kubainika kuwa taasisi za dini na zile zisizo za kiserikali zinafutiwa kodi.


Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alisema: "Serikali imeonyesha udhaifu mkubwa katika msamaha wa kodi ya mafuta kwa kampuni za madini, kwani inataka kushauriana nao kwanza. Sasa ni kwanini haikushauriana na vingozi wa dini kabla ya uamuzi huo kama inavyotaka kwa makampuni ya madini?


"Ina maana kuwa serikali inathamini uwekezaji kuliko dini na shughuli za dini? Natambua kuna taasisi za dini zinatumia vibaya misamaha hii, lakini kwa nini serikali itoe adhabu kwa taasisi zote? Ni jukumu la serikali kudhibiti abuse (matumizi mabaya) hiyo."


Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, alielezea msamaha wa kodi ya mafuta ya petroli kwa kampuni za madini nchini umelikosesha taifa Sh181 bilioni toka uanze mwaka 2005.


"Msamaha huo ulitolewa wakati kampuni zote zikiwa tayari zina mikataba, hivyo kimsingi msamaha huo haupo kwenye mikataba ya madini ambayo serikali imeingia nayo," alisema Zitto.

No comments: