Tuesday, May 26, 2009

Richmond, TICTS, TRL kutikisa Bunge

• Karamagi, Msabaha, Hosea, Mwanyika roho juu


na Deogratius Temba




HATIMA ya baadhi ya watuhumiwa waliohusishwa na kashfa ya kutoa zabuni kwa Kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond inatarajiwa kujulikana katika mkutano wa Bunge la bajeti unaotarajiwa kuanza Juni 9 mwaka huu.

Kashfa ya zabuni ya Richmond ndiyo iliyomfanya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ibrahim Msabaha, kujiuzulu, jambo lililosababisha kuvunjwa na kuundwa upya kwa baraza la mawaziri.

Tangu kutokea kwa kashfa hiyo hadi sasa, hali ya upepo si salama ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hasa baada ya kuibuka makundi mawili makubwa, moja likijinasibu linapinga ufisadi huku jingine likidaiwa kupambana na wale wote wanaoendesha vita dhidi ya ufisadi.

Miongoni mwa watuhumiwa waliotakiwa kuwajibishwa na serikali ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Johnson Mwanyika, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Edward Hosea, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ibrahim Msabaha.

Hatima ya watu hao itajulikana baada ya Bunge kupokea taarifa ya serikali kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge kutokana na hoja binafsi ya uuzaji wa nyumba za serikali, iliyowasilishwa bungeni na Mbunge wa Vunjo (CCM), Aloyce Kimaro na taarifa ya uamuzi wa serikali kuhusu mkataba wa Kampuni ya kimataifa ya kupakua na kupakia makontena bandarini (TICTS).

Aidha, pia Bunge litapokea utekelezaji wa serikali juu ya maazimio ya Bunge kuhusu Kampuni ya Richmond, taarifa ya serikali kuhusu uendeshaji wa Shirika la Reli nchini (TRL), na utaratibu wa ugawaji wa vitalu vya kuwindia na bei zake, ambao kisheria muda wake unaisha mwaka huu.

Mbali na taarifa hizo, pia serikali inatarajiwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo ya kamati maalumu ya rais, ya Nishati na Madini iliyokuwa chini ya Jaji mstaafu, Mark Bomani, na serikali itatoa taarifa juu ya ripoti ya hesabu za mashirika ya umma ambayo iliwasilishwa hivi karibuni.

Taarifa ya Bunge kupokea utekelezaji wa maazimio hayo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu shughuli zinazolikabili Bunge.

“Tunategemea baada ya kipindi cha maswali na majibu, na mjadala wa bajeti kumalizika, Bunge litapokea taarifa ya maazimio 23, ya Richmond, kuhusu uendeshaji wa Shirika la Reli (TRL) na TICTS,” alisema.

Alisema siku ya kwanza ya mkutano huo utafuatwa utaratibu wa kawaida wa kula kiapo cha uaminifu kutoka kwa mbunge wa Jimbo la Busanda, atakayechanguliwa leo, kufuatiwa na kipindi cha kawaida cha maswali na majibu, ambapo Juni 11, Waziri wa Fedha na Uchumi, atawasilisha taarifa rasmi ya hali ya uchumi nchini, na kufuatiwa na kuwasilishwa kwa hotuba ya bajeti siku hiyo jioni.

Alisema kwa mujibu wa kanuni ya Bunge namba 96(2), makadirio ya fedha za matumizi yatawasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Uchumi kwa hotuba ambayo hutolewa kabla ya Juni 20 kila mwaka.

“Kwa kuzingatia makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, bajeti za nchi wanachama kwa mwaka wa fedha wa 2009/10, zitasomwa siku ya Alhamisi Juni 11, 2009,” alisema Dk. Kashililah.

Pia alisema kwa mujibu wa kanuni 96(6), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Fedha na Uchumi pamoja na Kiongozi wa upinzani Bungeni, watapewa muda wa saa moja kila mmoja kuwasilisha maoni yao kuhusu hotuba ya bajeti na maelezo kuhusu hali ya uchumi kwa ujumla.

Alisema mara baada ya Bunge kukamilisha kazi ya kujadili na kupitisha makadirio ya matumizi ya wizara zote, muswada wa fedha za matumizi utawasilishwa bungeni na kupitishwa mfululizo katika hatua zote kwa mujibu wa kanuni namba 105.

Alisema muswada huo hautajadiliwa bungeni kama ilivyo miswada mingine, utasomwa na kupitishwa moja kwa moja maana unahitimisha mjadala wa jumla kwa kutaja jumla ya fedha zote za matumizi ya serikali zilizopitishwa na Bunge kwa mwaka huo wa fedha.

Kiu kubwa ya baadhi ya watu ni kuona hatua zipi zimechukuliwa na serikali dhidi ya watu waliotakiwa kuwajibishwa baada ya kamati teule ya Bunge iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, kubaini ukiukwaji wa sheria ya manunuzi ya umma, ambako kulifanya Kampuni ya Richmond kupewa zabuni ya kuzalisha umeme.

Ripoti ya kamati teule iliwasilishwa katika mkutano wa 10 wa Bunge na tangu wakati huo serikali imekuwa ikitoa sababu kadhaa za kutokamilisha utekelezaji wa maazimio hayo, kwa madai kuwa mambo mengine yalihitaji kuangalia sheria zaidi, huku mengine yakihitaji kufika kwa rais ili yatolewe uamuzi.

Wakati baadhi ya watuhumiwa wakiendelea kuwajibika katika ofisi za umma, mmoja wa watuhumiwa hao, Gray Mgonja, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, amefikishwa mahakamani akikabiliwa na makosa 10 ya kutumia vibaya madaraka yake, kwa kutoa msamaha kwa Kampuni ya Alex Stewart ambayo iliisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.

No comments: