Thursday, June 18, 2009

Kikwete azingirwa

• Hoja za maaskofu, wabunge zamuelemea


na Waandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete, sasa anaonekana kuzingirwa kila upande na makundi mbalimbali ya kijamii, ambayo hayaridhishwi na mwenendo wa mambo katika serikali anayoiongoza kiasi cha kuanza kutilia shaka maamuzi mazito yaliyofikiwa.

Hali hiyo ya manung’uniko, kuinyoshea serikali kidole na kumlenga Kikwete binafsi pasipo kumtaja moja kwa moja, imedhihirika tangu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo, asome hotuba yake ya Bajeti ya Serikali ya mwaka wa Fedha wa 2009/2010, Alhamisi, wiki iliyopita.

Hotuba hiyo ya bajeti ambayo inapingwa na wabunge wengi waliokwishaijadili, viongozi wa dini, viongozi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NG’Os), pamoja na wanaharakati, inamuweka Rais Kikwete katikati ya upinzani mkali kutoka kwa watu anaowaongoza na inatoa ishara ya kuwapo mtikisiko mwingine mkubwa serikalini.

Katika hali inayoonyesha kuishiwa uvumilivu kwa baadhi ya wabunge wa CCM, ambao hawako karibu na wateule wa Kikwete serikalini, sasa wameanza kuhoji miradi tata inayotekelezwa kinyume cha taratibu na wasaidizi wake.

Moja ya miradi tata inayotekelezwa kinyume cha taratibu za serikali uliotajwa bungeni juzi, ambao unamgusa moja kwa moja Rais Kikwete, ni ule wa ujenzi wa barabara ya Chalinze – Segera, unaodaiwa kuanza kutekelezwa kabla ya kuidhinishiwa fedha katika bajeti ya serikali. Mradi huo unapita katika eneo ambalo ni nyumbani kwao na Rais Kikwete.

Mradi huo ambao unaonyesha dalili za kuwapo upendeleo katika usambazaji huduma za maendeleo hapa nchini, iwapo utathibitika kuwa unatekelezwa kinyume cha taratibu, unaweza kumchafua Rais Kikwete kiasi cha kumfanya aonekane kuwa miongoni mwa viongozi wanaopendelea maeneo ya kwao katika utoaji huduma za jamii na maendeleo.

Tayari Spika wa Bunge, Samuel Sitta, juzi aliitaka serikali kutoa maelezo ya suala aliloliita zito sana la kuanza kutekelezwa kwa mradi huo ambao utakuwa unatumia fedha za bajeti ambayo haijapitishwa wala kujadiliwa.

Spika Sitta alitoa agizo hilo kwa serikali baada ya Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM) kutaka mwongozo wake kuhusu mahali ambako serikali imepata mamlaka ya kuanza kutumia fedha za bajeti kabla hazijapitishwa.

Selelii, mmoja wa wabunge ambao wamekuwa wakilalamika kuandamwa na mafisadi majimboni kutokana na harakati zao za kupambana nao, alikwenda mbali zaidi kwa kulishambulia Baraza la Mawaziri kuwa limejaa watu wabinafsi, wenye roho mbaya, wenye lengo la kutaka kukwamisha baadhi ya wabunge na akamuomba Mungu awalaani.

Mbunge huyo, alikuwa miongoni mwa wabunge wa mwanzo kuichangia hotuba hiyo huku akionekana kuwa mwiba mkali zaidi kwa serikali na Baraza la Mawaziri, jambo linalotafasiriwa na baadhi ya wachambuzi wa mambo kuwa ni mwanzo wa vita ya wazi ya kuhakikisha anapambana kubaki kwenye kiti chake cha ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwakani.

Baadhi ya wadadisi wa mambo waliozungumza na Tanzania Daima Jumatano, wanaielezea kauli ya Selelii dhidi ya mawaziri kuwa iliyokuwa ikimgusa moja kwa moja Rais Kikwete, ambaye kikatiba ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri.

Hoja hizo za awali bungeni zilikuja siku chache tu baada ya maaskofu kadhaa wa makanisa makubwa nchini ya Katoliki, Anglikana na Lutheran kuelezwa kusikitishwa na hatua ya Serikali ya Kikwete kufuta misamaha ya kodi kwa mashirika ya dini.

Baadhi ya maaskofu hao, akiwamo Benson Bagonza wa Kanisa la Kilutheri, Karagwe walifikia hatua ya kusema kuwa walikuwa wakikusudia kuishitaki serikali kwa waumini wao katika mimbari, hatua ambayo iwapo itatekelezwa inaweza kusababisha athari za kisiasa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwakani.

Mwenendo huo wa kutoridhishwa na bajeti hiyo ya serikali, uliendelea kuonekana hata jana wakati Bunge lilipokuwa likiendelea kuijadili, huku wabunge wakionyesha dhahiri kuweka kando itikadi za vyama vyao.

Akichangia hotuba ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mkulo bungeni jana, Mbunge wa Kishapu, Fred Mpendazoe (CCM), alisema kukosa umakini kwa viongozi kumeisababishia nchi matatizo makubwa na kuwafanya wananchi wake kuwa masikini.

“Ashakum si matusi, lakini mawe yaliyo baharini hayawezi kusikia kilio cha mtende ulio jangwani, wakati watu wanapiga vita ufisadi, wengine wanakejeli,” alisema Mpendazoe.

Alihoji inakuwaje mpaka sasa watu waliohusika katika kuingiza nchi katika mikataba mibovu, ukiwamo wa Kampuni ya Richmond hawachukuliwi hatua za kisheria na serikali inaendela kuwatengea bajeti kila mwaka.

“Watendaji wa serikali ambao wameiingiza nchi katika mikataba mibovu, ikiwamo ya Richmond, reli na Kiwira kwa nini hawachukuliwi hatua mpaka sasa? Wananchi wanataka kufahamu. Kutochukua hatua dhidi ya uovu maana yake ni kuubariki, hivyo serikali inapokuwa haichukui hatua dhidi ya ufisadi na mafisadi maana yake inabariki,” alisema Mpendazoe.

Pia aligusia suala la kampuni ya upatu ya DECI kwa kueleza kuwa wananchi walijiunga katika kampuni hiyo baada ya kutokuwa na mbadala na kuongeza kuwa, riba za mikopo katika benki zimekuwa kubwa na serikali imekuwa haifanyi jitihada za kuwasaidia wananchi.

Aidha, mbunge huyo alishangazwa na kuwapo kwa utiriri wa Wachina na Wakorea jijini Dar es Salaam, ambao wanafanya kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania huku wenyewe wakibaki bila ajira.

Mbunge wa Maswa, John Shibuda (CCM), yeye alihoji ni lini Watanzania watashika hatamu ya kuendesha mashirika mbalimbali yaliyopo nchini.

Alitoa mfano wa Shirika la Reli kwa kueleza kuwa awali lilipokuwa likiendeshwa na Watanzania, lilikuwa likifanya vizuri, lakini tangu wamepewa wawekezaji wa kutoka India, limekuwa na matatizo.

“Naomba mawaziri mtueleze hivi mnatupeleka wapi Watanzania? Mkataba wa TRL, TICTS… uzalendo wenu utapimwa vipi? Tumechoka, tunataka mtekeleze ilani ya chama vizuri,” alisema Shibuda.

Alimgeukia pia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kumtaka kuondoa shughuli za kutengeneza vitambulisho vya taifa katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa vile hakuna kinachoendelea katika utekelezaji wa kazi hiyo bali malumbano.

“Vitambulisho hivi vinaweza kuliingizia taifa mapato makubwa, kwani kuna watu wanaostahili kulipa kodi karibu milioni 18, tukivitumia vizuri vitatusaidia…lakini imeshindikana, wakati wa kubebana umepita, vitambulisho hivyo viondolewe,” alisema Shibuda.

Aidha, aliwatahadharisha vingozi kuhusu ugawanyaji sawa na ‘keki ya taifa’ na kutaka kutokuwapo kwa upendeleo katika maeneo wanayotoka viongozi, na akahitimisha hoja yake kwa kusema alikuwa ameahirisha kuiunga au kuipinga bajeti hiyo akisubiri majibu kutoka kwa Waziri Mkulo.

Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Mnyaa (CUF), aliwamtaka Waziri wa Fedha na manaibu wake kujiuzulu kutokana na tamwimu za hasara iliyopata serikali kutokana na rasilimali za nchi kunufaisha nchi nyingine. Alitoa mfano wa rasilimali ambazo zinanufaisha nchi za jirani kuwa ni magogo, ng’ombe na alizeti.

“Juzi, Mheshimiwa Sakaya (Magdalena) alipouliza swali hili, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi alisema hana takwimu. Je, kwa hii nilivyotaja serikali haijapata hasara? Naomba waziri na manaibu wake wajiuzulu kama hawana takwimu... huu si wakati wa kuoneana haya,” alisema Mnyaa.

Aidha, alisema pamoja na serikali kusema katika bejeti hiyo kuwa ‘kilimo kwanza’, lakini mafanikio katika sekta hiyo hayatapatikana bila ya kuwapo kwa umeme katika maeneo mengi nchini.

Alihoji kitendo cha serikali kupunguza bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini huku safari za ndani na nje ya nchi zikitengewa sh bilioni 34.6.

Mbunge wa Arumeru Mashariki, Elisa Mollel (CCM), alisema ubaguzi unaoendelea wa kupeleka maendeleo kwa baadhi ya maeneo nchini si mzuri. Alisema wananchi wa jimbo lake mpaka sasa hawana maji, lakini mabomba ya maji yamepita katika jimbo hilo na kupeleka huduma hiyo katika Jimbo la Monduli.

“Sina ugomvi wa watu wa Monduli, lakini si vema inavyofanyika, wananchi wa Arumeru Mashariki mpaka sasa hawana huduma ya maji,” alisema.

Naye Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (CHADEMA), alisema Rais Kikwete amepotoshwa kwa kuelezwa kuwa visa ya watalii imepunguzwa kutoka dola 100 hadi dola 50 na kusema kilichopunguzwa ni kiingilio cha watalii.

Alisema mgeni yeyote anayeingia nchini hutozwa visa ya dola 50 na kuongeza kuwa hata kama serikali imepunguza kiingilio cha watalii bado havivutii, kwani Kenya wanatoza dola 25.

Pia aliomba serikali kutafakari upya kufuta msamaha wa kodi kwa mashirika ya dini na kusema kama kweli kuna watu waliotumia vibaya misamaha hiyo serikali iwashitaki.

“Lakini kwa kuwa mpaka sasa hakuna mtu aliyeshitakiwa, naamini hakuna aliyetumia vibaya misamaha hiyo,” alisema Ndesamburo na kuongeza kuwa, huduma inayotolewa na mashirika ya dini katika jamii ni muhimu.

Kwa upande mwingine, viongozi wa dini nao wamekwishaeleza kutokubaliana na uamuzi wa serikali wa kutaka kulipia kodi baadhi ya vifaa vya kibiashara wanavyopatiwa kama msaada au wanavyonunua kutoka nje ya nchi.

Msimamo huo unawajumuisha viongozi wa dini zote kubwa hapa nchini na baadhi yao wamekwishaeleza kuwa iwapo serikali haitawasilikiza na kubadili uamuzi wake huo, basi hukumu yake itapatikana katika uchaguzi mkuu wa mwakani.

Viongozi hao wa dini wamekwishaeleza kuwa wanaandaa waraka wa kupinga uamuzi huo wa serikali na baadhi wamekwishaanza kutoa elimu kwa waumini ya jinsi ya kuchagua viongozi wanaofaa, jambo linaloashiria kuwa ni maandalizi ya mapema ya kuwaandaa waumini kutofanya makosa katika uchaguzi ujao.

No comments: