Friday, April 17, 2009

Kikwete awajia juu mawaziri watukanao

Imeandikwa na Maulid Ahmed, Saudi Arabia; Tarehe: 17th April 2009 @ 10:34

Rais Jakaya Kikwete ameelezea kukerwa na vitendo vya baadhi ya mawaziri wa nchi za Afrika Mashariki kutumia lugha za matusi na kuikejeli Tanzania kutokana na msimamo wake wa kutokubali suala la ardhi na ajira liwe la Afrika Mashariki kwa sasa. Rais Kikwete alielezea masikitiko yake hayo juzi wakati akijibu maswali ya Watanzania waishio hapa wakati alipokutana nao katika Hoteli ya Riyadh Palace.

Ingawa Rais Kikwete hakutaja mawaziri hao ni wa nchi gani, lakini hivi karibuni zimekuwapo taarifa kuwa baadhi ya mawaziri wa Kenya wamekuwa wakiikejeli na kupingana na Tanzania kwa msimamo wake wa kutaka suala la ugawaji ardhi kwa wananchi wa Afrika Mashariki lisiingizwe kwenye masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, bali nchi husika iwe na mamlaka juu ya umilikishwaji huo wa ardhi. Rais Kikwete alisema: “kinachonisumbua sasa juu ya suala hili ni jinsi linavyojadiliwa kwa kejeli, waziri tu anatukana nchi nyingine, lugha zinazotumiwa hazitasaidia kujenga Afrika Mashariki, silifurahii hili la kutukana nchi nyingine.

“Kama hili la ardhi sasa haliwezekani tusigeuze kuwa kama hilo haliwezekani basi Jumuiya ya Afrika Mashariki haiwezekani, kama kwa sasa suala la ardhi ni gumu liachwe yafanywe mengine yanayowezekana na wakati ukifika litajadiliwa”. Mbali na hilo, Rais Kikwete ambaye alimaliza ziara yake jana, aliwambia Watanzania hao kuwa kutokana na hali ya mvua mwaka huu kutokuwa nzuri nchini, kutakuwa na upungufu wa chakula.

Alisema uhaba wa mvua upo katika mikoa ya Pwani, Tanga, Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Morogoro na kuongeza: “Lakini tutajitahidi kukabiliana na uhaba huo”. Aliwaasa Watanzania hao kukumbuka nyumbani kwa kupeleka maendeleo na kuwasaidia ndugu zao na si kujisahau na wanaporejea nyumbani wanajikuta wakiwa na maisha magumu. Aliwataka waishi hapa kwa kuzingatia sheria za nchi na kuongeza: “Huwezi kuishi hapa kwa sheria zako, watakushughulikia, ukifanya makusudi kuvunja sheria hutatunyima usingizi, lakini ukionewa ubalozi utakusaidia”.

Akijibu swali la Mtanzania aliyetaka kuanzishwe shule ya Afrika Mashariki ili watoto wasome kwa kufuata mtaala wa Afrika Mashariki, Rais Kikwete aliwataka mabalozi wa nchi za Afrika Mashariki kukaa na kuanzisha shule hiyo na serikali zao zitasaidia kupeleka mitaala ya kufundishia. Kuhusu uraia wa nchi mbili, alisema Watanzania wengi waishio nje wanalitaka hilo, na kwa sasa suala linafanyiwa kazi.

Katika hatua nyingine, mke wa Rais, Salma Kikwete, aliwambia wanawake Watanzania wanaoishi hapa, kuwafundisha watoto wao utamaduni wa Kitanzania na lugha ya Kiswahili. “Asiyekuwa na utamaduni ni mtumwa, wafundisheni watoto utamaduni wa nyumbani na nyinyi kumbukeni kusaidia nyumbani,” aliwambia. Wakati huohuo, Rais amesema kuanzia sasa Tanzania itaanza kupata mikopo yenye masharti nafuu kutoka taasisi za fedha duniani kutokana na utendaji wake kuwa mzuri.

Tanzania ni miongoni mwa nchi tano za Afrika zilizofanya vizuri kiutendaji ambapo Rais Kikwete alisema: "Kutokana na utendaji wetu mzuri mlango wa kupata mikopo sasa utafunguliwa na tutafanya maendeleo zaidi." Akifanya majumuisho ya ziara yake mjini hapa, Rais aliwataka wafanyabiashara wa Tanzania kujitayarisha kuchangamkia uwekezaji kutoka Saudi Arabia.

"Tujitayarishe katika maeneo ambayo wafanyabiashara wa Saudi Arabia wameonyesha nia, mfano katika kilimo, ili wakija wakute watu wako tayari kushirikiana nao… wamesema wana dola trilioni 1.6 na kati ya hizo dola bilioni 60 wamezitenga kwa utalii nasi tutumie nafasi hiyo," alisema. Akijibu swali aliloulizwa sababu za utawala wake kupata misaada mingi kuliko mikopo, alisema: "Kila kitu kina wakati wake na kukaa kwangu miaka 10 nikiwa Waziri wa Mambo ya Nje, kumenisaidia kupata marafiki wengi ambao sasa wananisaidia kupata misaada katika nchi zao kama Marekani, Uingereza, Japan na Ufaransa".

Alisema licha ya Tanzania kupata misaada kutoka Saudi Arabia kama kusaidia ujenzi wa daraja la Mkapa lakini bado haijatumia sawasawa fursa za kupata misaada hiyo na kuongeza kuwa sasa itaitumia nafasi hiyo. Alisema ziara hiyo ya kikazi ya siku tatu imekuwa na mafanikio na sasa Tanzania ina matumaini ya kuuza bidhaa zake Saudi Arabia.

No comments: