Friday, April 17, 2009

Ngassa ngoma nzito ughaibuni


Winga wa Yanga ya Dar es Salaam na timu ya soka ya taifa 'Taifa Stars', Mrisho Ngassa ameanza majaribio katika timu ya West Ham United ya nchini Uingereza, lakini kukiwa na wachezaji wengi wanaowania pia kusajiliwa na timu hiyo.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Mohammed Sadick, ambaye ni Mtanzania anayeishi nchini humo, alisema pamoja na kuwa na matumaini huenda Ngassa akafanikiwa, lakini kazi ya ziada itabidi aifanye ili kuipata nafasi hiyo. "Niliposikia kuwa Ngassa anakuja huku, nilifuatilia mambo mbalimbali ndani ya timu anayokuja, nikagundua anatakiwa aongeze juhudi za ziada uwanjani ili kuwashawishi wamchukue.

"Namfahamu Ngassa ana uwezo mkubwa, kinachotakiwa apambane, maana vijana wanaotakiwa ni wachache, wakati wao wapo wengi, huku wengine wakitoka nchi zenye majina makubwa kisoka Afrika na hata hapa Uingereza," alisema Sadick. Hata hivyo alisema katika siku mbili za mazoezi, ameonyesha mwelekeo, ingawa idadi kubwa ya wachezaji waliopo katika majaribio ambao wanazidi 20, huku wakitakiwa watatu inamtisha.

Naye mchezaji mmoja wa Yanga, ambaye ni rafiki wa karibu wa Ngassa, alilieleza gazeti hili jana kuwa amezungumza na mchezaji huyo juzi na kumwambia ameanza vizuri, lakini idadi ya wanaotakiwa inamwogopesha. "Amenambia wapo wachezaji 20 wengine wanatoka Nigeria, Senegal, Afrika Kusini na sehemu nyingine, lakini wanatakiwa watatu, sasa nimemweleza asife moyo ndio mapambano yenyewe hayo, aongeze juhudi uwanjani.

"Amenielewa, tunamtakia heri, huku pia wadau wengine naamini nao wanamtakia mafanikio mazuri, hakuna kisichowezekana chini ya jua, " alisema mchezaji huyo. Ngassa ambaye ni mtoto wa kiungo wa zamani wa Pamba, Simba na timu ya taifa 'Taifa Stars', Khalfan Ngassa 'Babu', aliondoka Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki kwenda nchini Uingereza kufanya majaribio ya kucheza soka katika kikosi cha vijana cha timu ya West Ham ya huko inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

No comments: