Friday, April 17, 2009

DECI sasa kizaazaa

• Watangaza kufunga ofisi zao nchi nzima


na Ratifa Baranyikwa na Lucy Ngowi




SIKU moja baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutangaza msimamo wa serikali wa kutounga mkono shughuli zinazofanywa na Kampuni ya Development of Entrepreneurship for Community Initiative (DECI), viongozi waasisi wa kampuni hiyo wamejitokeza hadharani na kupinga msimamo huo wa serikali.

Mbali ya kutangaza msimamo huo, DECI imetangaza kufunga ofisi za matawi yake yote 36 nchi nzima ili kupisha majadiliano yanayoendelea kati yake na serikali.

Waaasisi hao wa DECI ambao walijitokeza kwa mara ya kwanza jana na kujitambulisha kwa majina na vyeo vyao, walikanusha vikali kauli ya Waziri Mkuu Pinda aliyeuelezea mchezo wao kuwa ni upatu na ujanja ujanja wenye mwisho mbaya.

Wakizungumza kwa kupokezana, waasisi hao, Timoth Ole Loeiting’ye, Meneja Ufundi na Ushauri, Arbogast Kipilimba na Mwenyekiti wa Bodi, Jackson Mtaresi, walirejea hoja waliyopata kuieleza siku zilizopita kwamba, DECI ni matokeo ya maono na ufunuo walioupata kutoka kwa Mungu kwa njia ya sala kabla ya kuianzisha.

Waasisi hao ambao walikuwa wakizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam, jana, waliwahimiza washiriki wa mchezo huo kuendelea kupanda na kuvuna, wakisisitiza kuwa, kampuni haitakufa kamwe.

Huku wakisema kuwa walikuwa wakimshukuru Waziri Mkuu kwa kauli yake, viongozi hao wa DECI walipinga msimamo wa Pinda wa kuuita mchezo wao kuwa ni upatu na uliotawaliwa na ujanja ujanja ambao mwisho wake ni kuwaliza washiriki wake.

Viongozi hao ambao ni wachungaji wa Kanisa la Jesus Trust for Deliverance waliendelea kusisitiza kwamba, DECI ni maono na ufunuo.

“DECI ilianzishwa na kusajiliwa mwaka 2007 kwa kufuata taratibu zote chini ya uasisi wa kanisa hilo…waasisi walikuwa wamepata mzigo na maono ya kushirikiana na serikali katika kupambana na umaskini. Sisi Wakristo tunaamini ukipiga magoti Mungu anakujibu…waasisi hao waliomba si kwa wiki wala miezi, ni muda, wegine wanaona tunajenga hoja ya kudhulumu, lakini sivyo.

“Baada ya kumuomba Mungu kwa kina, wakapata majibu juu ya mateso ya jamii wanamoishi, wakaomba Mungu awafungulie watu wakaunganika na makanisa mengine hata ya nchi jirani, wakajiuliza tufanye nini, na baada ya hapo walianzisha DECI kwa madhumuni mengi na jinsi ya kuwasaidia watu, lakini kwa maono waliyoyapata wakaona ni bora kuanza na ‘Microfinance’, wakajikita katika kupanda na kuvuna, ambako ni lazima iendane na taratibu zinazofahamika,” alisema Kipilimba.

Alisema, wanasikitika wao kama viongozi wa DECI hawajawahi kupata nafasi ya kukaa na serikali, kwani hata walipowatafuta, hawakuwapata kirahisi ingawa leo wamewaita upatu, piramidi na matapeli. Ili kuondoa dhana hiyo na kuweka mambo sawa, wameitaka serikali ikae pamoja nao.

“Kauli ya Waziri Mkuu ni nzuri ingawa sisi tuna hoja ya kupinga kuitwa piramidi, upatu na matapeli, kwa sababu hata mimi nashangaa mtu anayetuita piramidi kwa sababu piramidi haina ‘organization structure’, haina kitu kinaitwa ‘retainer’ ili uweze kupata ‘profit’.

“Sasa tunataka tukae na serikali tuwaonyeshe, watukosoe kwani dhumuni la DECI ni kutumia nguvu na uwezo ili wajasiriamali wadogo waweze kuwa wakubwa na hapo ndipo tunapokabwa tueleze, hatuelezi ng’o.

“Tunaishukuru sana BoT kwa tangazo lake kwani wengine walikuwa wanadhani tunaichukia… BoT tumekuwa tukiwasiliana nayo tangu mwaka 2007 tuliposajili. Biblia ina maneno haya: ‘Tunawarudi tuwapendao’, leo huyu aliyepewa kusimamia, Registrar wa BoT, anaturudi hatuna ugomvi na BoT. Tulipokuwa tunawasiliana na BoT kuna wataalamu walitushauri, kwa hiyo hatuwezi kusema wanatuchukia.

“Sisi tumekuja tuwaeleze washiriki wetu, tuwatie moyo kwa sababu kwenye ule mkutano uliofanyika Viwanja vya Sabasaba kwenye Ukumbi wa PTA hatukuwepo, tunataka tuwatie moyo washiriki wetu kuwa DECI bado inaendelea na mazungumzo na serikali.

“Tume zilizoundwa bado zinapita katika maofisi yetu kutuhoji, hivyo washiriki wetu wawe na subira, wasiwe na hofu, tunaamini serikali inachokifanya ni kizuri tu, hata taarifa za BoT ni nzuri, tunajua wameathirika na kupotoshwa kuwa sisi ni upatu, piramidi, hilo wasijali, tunawaomba wale ambao wamepanda waendelee maana ukipanda mbegu nyingi mavuno ni mengi,” alisema Kipilimba.

Aidha akielezea idadi ya washiriki pamoja na fedha zilizopo, Mwenyekiti wa Bodi ya DECI, Mtaresi, alisema hadi sasa wana washiriki zaidi ya 700,000; fedha zilizopandwa ni sh bilioni 54 na zilizovunwa ni bilioni 38/-.

Alisema hata hivyo kuwa, baada ya kutolewa kwa matangazo ya BoT, zaidi ya sh bilioni tano, zimeng’olewa ili kurejesha fedha hizo kwa waliopanda, hivyo kwa sasa wana sh bilioni 11 ambazo wamezihifadhi benki bila kutaja jina la benki kwa madai kuwa ni siri.

Mwenyekiti huyo alisema, kama DECI kingekuwa chombo hatari, basi wangekuwa wamefikishwa katika vyombo vya sheria, lakini hadi kufikia juzi hakuna mtu yeyote aliyefika polisi kudai kama DECI imemdhulumu au imemfanyia lolote baya.

Aidha alipoulizwa kama chombo hicho kina uhusiano wowote na watu wa kutoka nchi za nje, mwenyekiti huyo aliendelea kusisitiza kuwa wao ndio waasisi, na kwamba hata serikali ifikirie kuwa jambo hilo linafanywa na Watanzania.

“Najua gharama niliyotumia kumlilia Mungu juu ya kuweka chombo hiki, leo DECI imeanzishwa Mabibo, serikali ichunguze hili jambo. Viongozi watupe nafasi, tukikaa tutawaeleza kinachostahili,” alisema.

Alipoulizwa juu ya faida kubwa ambayo anapata mpandaji, Mtaresi alisema anashangaa kuona hata watu wanaojua mahesabu wanahoji juu ya jambo hilo ingawa awali alisema hawako tayari kutoa mfumo wanaotumia.

Pia viongozi hao wa DECI walikanusha kauli zilizopata kutolewa kwamba kampuni hiyo inaua Saccos na kuwafanya watu wasihifadhi pesa zao benki.

“Nia ni kuwafanya washiriki waweze kupata pesa za kwenda kuweka Saccos ili waweze kukopa na kuhusu benki, tulishafanya mipango washiriki wote wakapokelee fedha zao katika mabenki, lakini bado hatujafikia muafaka,” alisema.

Walipoulizwa juu ya barua ambayo BoT inadai kuwa DECI iliomba kufanya shughuli ya kutoa mikopo na si kupanda na kuvuna kama ilivyo sasa, viongozi hao walisema kuwa BoT inawazushia na kwamba walifanya taratibu zote wakimtumia mshauri wao.

“Tuliomba tuwe Microfinance benki tukaambiwa tuandike barua tutajibiwa na hatujajibiwa mpaka leo… na kitengo cha Microfinance cha BoT ndio walezi wetu DECI,” alisema.

Kuhusu usalama wa washiriki, Mtaresi alisema kuwa usalama wanao wa kutosha, lakini akakataa kusema ni upi na kusisitiza kuwa mtu akihitaji kung’oa wanampa na kama mtu akifa zipo taratibu zinazofanyika kurejesha fedha hizo.

Aidha, viongozi hao walisema wanahofia usalama wao kwani tangu kuzuka kwa sakata hilo, mmoja wa viongozi wake, aliwahi kutekwa nyara na watu asiowajua, lakini alifanikiwa kuwatoroka.

“DECI imeathirika si tu kwa wanachama wanaong’oa, bali hata usalama wetu sisi ni hatari... nilitekwa nyara wakaniambia twende kwa fulani (simtaji) ndiye atakayenitatulia tatizo langu, mimi nikasema bila Rais Kikwete wala Waziri Mkuu Pinda na BoT siendi.

“Watu hao walikuwa kwenye Pajero ndogo namba nimezihifadhi, nikawaambia subirini huku nikiomba Mungu anisaidie, niliweza kuwashawishi na kuwatoka,” alisema Kipilimba.

Katika hatua nyingine, DECI imetangaza kufunga ofisi za matawi yake yote nchini hadi hapo itakapomaliza majadiliano na serikali.

Ingawa viongozi wake hawakutoa taarifa hiyo katika mkutano wao na waandishi wa habari, lakini tangazo la kuzifunga ofisi zao, lilisikika kupitia kituo cha Redio WAPO.

Tanzania Daima ilipofika katika ofisi za makao makuu ya DECI, Mabibo, ilishuhudia zikiwa zimefungwa, huku kukiwa na makundi ya watu waliokuwa wakijadili hatma ya kampuni hiyo.

Kati ya watu hao, wapo ambao walikuwa wamekwenda kwa nia ya kuvuna, na wengine wakiwa wanasikilizia hatma yao ambao walisikika wakiilaumu serikali kwa hatua yake ya kutotambua shughuli za DECI.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, jijini Dar es Salaam, Zachary Kakobe, aliitaka serikali isiionee huruma DECI kutokana na kukiuka taratibu za nchi.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kanisa hilo, Kakobe aliitaka serikali ichukue hatua haraka.

Kwa maelezo ya Kakobe, fedha hizo zingekuwa benki, wananchi wasingepata hasara, lakini kwa kuwa zilipandwa DECI lazima hasara iwepo.

Kwa upande mwingine, askofu huyo aliwataka viongozi wa siasa wasitafute kura kwa wananchi kwa kuwaruhusu kuvunja sheria, bali wawafundishe kusimama katika sheria.

No comments: