Saturday, April 11, 2009

CLUB RAHA LEO SHOW NA UNCLE J!


Yapo mambo ambayo ukijaribu kuyakumbuka bila shaka unaweza kutokwa na machozi.Yaweza kuwa machozi ya furaha na pia yaweza kuwa ya huzuni.Lakini kama wasemavyo walimwengu,yote huwa ni sehemu ya maisha.

Mojawapo ya mambo ambayo nikiyakumbuka huwa napata gunia la hisia tofauti tofauti ni kipindi cha Club Raha Leo Show cha enzi hizo za Radio Tanzania Dar-es-salaam kilichokuwa kikiendeshwa na Julius Nyaisangah au maarufu kama Uncle J(pichani). Hizo ni zile enzi za utawala wa RTD kabla vituo mbalimbali vya FM havijaanza kufumuka ili kutanua wigo wa habari na mawasiliano na pia kuongeza ushindani kama sio kutuibulia pia DJs wengine ambao nao wana nafasi ya pekee katika historia ya utangazaji nchini akiwemo rafiki yangu Mike Mhagama na wengine wengi.

Kipindi cha Club Raha Leo Show kilikuwa ni sehemu muhimu sana kwa wasanii na bendi kutambulisha nyimbo zao,kukutana na mashabiki wao na pia nafasi nzuri ya wasikilizaji kutuma na kupokea salamu.Sina uhakika kama kipindi hiki bado kinaendelea.Lakini kama hakipo tena swali muhimu ni kwanini hakipo?

Kwa ijumaa ya leo burudani nzima inatoka hapo Club Raha Leo Show.Hapo utamsikia Uncle J akishirikiana na mtangazaji mwingine mahiri,Michael Katembo. Bendi iliyopo studio ni wana-Ndekule.Bila shaka kipindi hiki kitakukumbusha mbali.Natumaini utacheka kwa furaha na kama ikitokea ukalia,basi natumaini yatakuwa machozi ya furaha,

No comments: