Wednesday, February 18, 2009

SALAMU ZA FA KUTOKA COVENTRY


Hakuna ubishi kwamba kijana Hamis Mwinjuma au maarufu kama MwanaFalsafa(MwanaFA) ni miongoni mwa wanamuziki wa muziki wa kizazi kipya ambao wamefanikiwa.MwanaFA amefanikiwa sio tu kufikisha ujumbe alioukusudia kwa jamii bali pia kuwa na uwezo wa kuendesha maisha yake kupitia muziki.Miziki yake imekuwa ikiimbwa na watu wa rika mbalimbali.Hayo nayo ni mafanikio.


Pamoja na mafanikio ya kimuziki au kisanii aliyonayo MwanaFA,anabakia kuwa mfano wa kuigwa linapokuja suala zima la elimu,muziki na maisha.Hivi karibuni alithibitisha hilo pale alipoamua kurejea tena shule.Safari hii ameelekea nchini Uingereza.


Nini kinamsukuma kijana huyu katika nyanja ya elimu? Na je hivi karibuni alipoachia wimbo unaokwenda kwa jina “Msiache Kuongea” alikuwa anamjibu Inspekta Haruni?Anazungumziaje maisha ya nchini Uingereza?Fuatana nasi katika mahojiano haya mafupi na MwanaFA


BC: Pamoja na mafanikio mazuri katika muziki kule Bongo bado umeamua kurudi tena shule.Nini kinakusukuma?Hapo UK umeenda kusomea nini na katika chuo gani?


FA: Kuna mengi yanafanya nifanye nnachofanya.Lakini kubwa na la msingi zaidi ni kuwa na nguzo nyingine kwa ajili ya maisha ninayoishi(Plan B).Kama unavyojua muziki pamoja na kuwa unakwenda vizuri lakini hautabiriki sana.Ni ngumu kujihakikishia nafasi ya moja kwa moja kwa angalau miaka 10 ijayo.


Na zaidi ni kuwa naona kama kuna muda mwingi kama msanii wa kibongo nakuwa naupoteza kwa kutofanya chochote baada ya kurekodi(ambayo sio kila siku),kufanya shows(mara nyingi huwa weekends),matangazo(mara chache kama una bahati) na interviews ambazo nazo sio kila siku.Kwa hiyo kwenye wiki kunakuwa na muda mwingi unaenda bure ambao nimeona ni vyema nikautumia kufanya kitu kitakachozalisha.
Hapa UK nasoma Msc Finance na nipo Coventry University.


BC: Una mpango gani na muziki kwa hivi sasa?Kama utaendeleza muziki na shule vilevile,lini labda wapenzi watarajie albamu yako mpya?


FA: Nimeacha album ikiwa tayari,inaitwa ‘mabibi na mabwana’ na naomba maswali kuhusu hiyo ayajibu Hermy B,ndio ipo mikononi mwake..sijapumzika kabisa muziki,ila nimepunguza kiwango ninachoufanya kwa sababu ya umbali.Ngoma zitaendelea kushuka kama kawa..patience kidogo inahitajika nitulize haya ya kwa Bi Eliza kwanza.


BC: Katika wimbo ulioutoa hivi karibuni kabla hujaondoka Bongo(ukishirikiana na Lady Jay Dee),inaelekea kwa namna fulani umemjibu Inspekta Haruni na wengineo wengi.Kwanini umefanya hivyo ikizingatiwa kwamba ulishasema siku za nyuma kwamba hutomjibu?


FA: Kama utakuwa umeniskiza vizuri sikumjibu..nilisema ‘…nisemeni hadharani hata bila hoja kama Inspekta’,nikimaanisha natoa ruhusa kwa kila mtu kunisema hata kama hana sababu za msingi za kufanya hivyo kama alivyofanya jamaa.Na,aina ya mziki tunayoifanya hairuhusu kabisa unyonge,ilikuwa haki yangu ya kimsingi.Watu wengi wanaongea vitu vingi vibaya siku hizi,hivyo inabidi niwaambie najisikiaje wakifanya hivyo.


Ukweli ni kuwa hawaingii kwenye lines zangu za maisha na wananipa nguvu na hasira za kufanya vyema zaidi.Na sio kwangu mwenyewe,kila mtu ana matatizo yanayofanana na yangu kwa namna moja ama nyingine kwa hiyo anaweza kuitumia kimpango wake.


BC: Umekuwa ukiingia na kutoka nchini Uingereza mara kadhaa.Ni mambo gani ambayo unadhani unayafurahia hapo UK na ambayo labda nchini kwetu tungeyaiga yangesaidia katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo?


FA: Uingereza kama nchi imejipanga.Ni dunia ya kwanza.Kuna mengi tunaweza jifunza,siwezi hata kuorodhesha.Lakini napenda namna wanavyoheshimu utawala na nguvu za sheria.Natamani kwetu kungekuwa hivi kwa kuanzia.


BC: Una mpango wowote wa kushirikiana kimuziki na wasanii wa hapo UK?Ni kina nani ambao unawazimia?


FA: Muziki wa UK hauendani sana na wa kwetu.Wana muziki tofauti na sisi.Pamoja na umbali wa kimaendeleo waliotuacha nao sijui hata wanamuziki 10 wa hapa.Hata rap/hiphop ya hapa siamini kama inapendwa mahala pengine popote zaidi ya UK.Haina mafanikio makubwa nje ya hapa.


Hata hivyo napenda mziki wa Lemar na Jay Sean na natamani nifanye nao kitu kama ninavyotamani kuifanya hii shughuli na 2face.


Nimekutana na Amit(Mentor) ambaye apparently ndio amemtoa Jay Sean(japo sasa Jay amepata record deal Cash Money),na tunajaribu kuona nawezaje kufanya mawili matatu toka nyumba yake ya muziki.Huwezi jua..nasubiri nione kitakachotokea

No comments: