Wednesday, February 25, 2009

Maskini Liyumba



na Mwandishi Wetu
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilimfutia dhamana aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba, ambaye ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na kusababisha hasara ya sh bilioni 221, baada ya kubaini kuwa aliidanganya mahakama.

Aidha, mahakama imebaini hati 10 zilizotumika kumdhamini mshitakiwa huyo zilizowasilishwa wiki iliyopita zina upungufu mkubwa na hivyo kuamuru hati hizo zikabidhiwe kwa Jeshi la Polisi ili zifanyiwe uchunguzi.

Uamuzi huo ulitolewa jana majira ya saa 8:02 na Hakimu Mkazi Hadija Msongo, katika chumba namba moja, ambapo umati wa watu ulifurika kufuatilia kesi hiyo, alisema baada ya kusikiliza hoja za pande mbili amekubaliana na hoja za upande wa serikali za kumfutia dhamana mshitakiwa, kwa kuwa ameidanganya mahakama kwa kutoa taarifa za uongo.

Februali 17 mwaka huu, Hakimu Msongo alimpatia dhamana mshitakiwa huyo baada ya kuwasilisha hati zenye thamani ya sh milioni 882, badala ya sh bilioni 55 na hati ya kusafiria ambayo ilikuwa imekwisha muda wake.

Msongo, alisema kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama katika maombi ya dhamana, aliwasilisha hati ya kusafiria ambayo ilikwisha muda wake wa matumizi Februari 12, mwaka 2007.

Katika kumbukumbu za mahakama zinaonyesha alimuuliza kama ana pasi nyingine za kusafiria, mshitakiwa huyo alikana na ili kuthibitisha taarifa hizo mahakama iliiomba Idara ya Uhamiaji ambayo ilibainisha kuwa Liyumba ana hati nyingine ya kusafiria yenye namba AB 019418 iliyotolewa Juni 10, mwaka 2005 ambayo muda wake wa matumuzi unamalizika mwaka 2015, ambayo aliwasilisha mahakamani hapo siku moja baada ya kupata dhamana.

Alisema kutokana na sababu hiyo mahakama imeona mshitakiwa huyo ametoa taarifa za uongo kwa vile hati ya kusafiria inamruhusu mtu kusafiri ndiyo maana Jumatano iliyopita mahakama hiyo ikatoa amri ya kukamatwa kwa mshitakiwa huyo.

“Baada ya kupokea taarifa hizo mahakama imebaini Liyumba alitoa taarifa za uongo, mimi nilimuuliza kama ana hati mbili za kusafiria, alikana lakini uhamiaji imethibitisha ana hati mbili, leo mahakama inatoa ufafanuzi kama ifuatavyo:

“Baada ya taarifa hizo Februari 18 mwaka huu mahakama ililazimika kutoa amri ya kukamatwa kwa mshitakiwa, kwa sababu aliidanganya mahakama kuwa hakuwa na pasi nyingine ya kusafiria.

“Mshitakiwa baada ya kutoa pasipoti iliyoisha muda wake aliwasilisha nyingine kwa kupitia njia zisizo na utambulisho na alimtuma mtoto wake kuileta.”

Msongo alisema baada ya kupitia kwa kina hoja za pande mbili, amebaini mshitakiwa aliidanganya mahakama na kutupilia mbali hoja za wakili wa mshitakiwa Majura Magafu, kwasababu hoja zake alizozitoa hakuzielekeza kwenye suala la msingi lililopo mahakamani, kwani mshitakiwa ndiye alikana kwa kinywa chake kwamba hana hati nyingine ya kusafiria.

“Jibu kwamba hana pasipoti nyingine lilitolewa na Liyumba mwenyewe na alijibu hivyo kwa sababu alikuwa akijua hana hati nyingine ya kusafiria, hivyo hoja ya Magafu ya kudai mteja wake hakuwa na lengo la kuiadaha mahakama haikubaliki kwa sababu Magafu hawezi kuthibitisha kauli ya Liyumba aliyokana kuwa na pasipoti mbili,” alisema Msongo.

Hakimu Msongo, alisema anakubaliana na hoja za wakili wa Serikali Prosper Mwangamila kwamba Liyumba aliidanganya mahakama na kupinga hoja ya Magafu kwamba mshitakiwa ndiye aliyegundua kuwa alitoa hati zilizoisha muda wake, bali ni mahakama, hivyo kutokana na kumbukumbu mahakama inamuona si mkweli.

Akizungumzia hati 10 zilizotumika kumdhamini mshitakiwa huyo, alisema mahakama imegundua hati ya Avogiti Chiwando, ambayo inaonyesha ilitolewa na Afisa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, si kweli, mtu huyo hayupo kwenye wizara hiyo na hati ya Abubakar Ogunda, ambayo ilionyesha kuwa na mali kama kuku na ng’ombe haikubaliki, kwani sharti la dhamana lilitaka kuwasilisha hati ya mali zisizohamishika.

‘Kwa ujumla hati zote 10 zinazoonyesha nyumba na viwanja katika maeneo mbalimbali zimeonekana kuwa na kasoro kwani majengo katika hati hizo zinaonekana kufanana.

“Na hati hizo ambazo zinaonyesha ziligongwa muhuri na Mtathimini wa Gharama za Majengo, Thomas Antabe, hazikubaliwi na mahakama, kwani muhuri wa mtu huyo hauonyeshi mahali ilipo ofisi yake, hivyo mahakama inaona mshitakiwa hajatimiza masharti ya dhamana.

“Kwakuwa masharti ya dhamana hayajatimizwa, mahakama hii inatoa amri ya kumfutia dhamana mshitakiwa na hati hizo kumi zipelekwe Jeshi la Polisi ili ziweze kufanyiwa uchunguzi wa kimaandishi na kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 10 mwaka huu, ambapo mahakama itakuja kusikiliza ombi la upande wa utetezi.

Kabla ya kutolewa uamuzi huo, wakili Mwandamizi wa Serikali, Justas Mulokozi, aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na mahakama hiyo ilitoa hati ya kukamatwa mshitakiwa wa kwanza, ambaye amekuja leo (jana) mahakamani hapo.

Baada ya kusema hayo, wakili Majura Magafu alisimama na kusema awali kuwa anapinga maelezo ya Mulokozi kwamba mteja wake amekamatwa, bali alifika mahakamani hapo kama alivyotakiwa na mahakama hiyo wiki mbili zilizopita.

“Mteja wangu amekuja mwenyewe mahakamani, hakuwa na habari kuwa anatafutwa, licha ya magazeti kuandika habari nyingi kuwa anatafutwa, alivyofika asubuhi aliripoti kwa Mkuu wa Waendesha Mashtaka, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Charles Kenyela, kujua kama ni kweli alikuwa akitafutwa au ni maneno ya magazeti.

“Kwa hiyo tunaomba ieleweke Liyumba hajakimbia na wala hajakamatwa na taarifa za yeye kutafutwa zilikuwa zikitolewa kwenye magazeti … leo amekuja mwenyewe kwa sababu alikuwa akifahamu ndiyo kesi yake inakuja kutajwa,” alidai Magafu.

Aidha, alikiri hati ya kusafiria ya mshitakiwa ilikuwa imeisha muda wake lakini alidai hali hiyo ilitokea kwa bahati mbaya, kwani mteja wake alikaa mahabusu kwa muda mrefu, hivyo alichanganyikiwa na aliagiza watoto wake ndio walete hati na wakaleta hati iliyokwisha muda wake, mteja wake aligundua kosa hilo na alihakikisha analeta hati mpya ambayo imechukuliwa na mahakama hiyo.

“Hivyo mheshimiwa hakimu, mteja wangu hakuwa na nia mbaya ya kuihadaa mahakama, kwakuwa hati hiyo ipo mahakamani na hatukufanya makusudi, tunaomba ile amri ya kumkamata mteja wangu iondolewe na dhamana yake iendelee,” alidai Magafu.

Akijibu hoja hiyo, wakili Mulokozi alidai pamoja na maelezo marefu na matamu ya wakili Magafu, bado amri iliyotolewa na mahakama ya kumkamata mshitakiwa inatekelezwa na ndiyo maana mshitakiwa alivyofika mahakamani alikuwa chini ya ulinzi, na kuongeza kuwa hoja ya wakili wa utetezi kwamba hajakamatwa haina msingi.

Hata hivyo Wakili wa Serikali Prosper Mwangamila, aliinuka kuomba ridhaa ya mahakama ili aweze kujibu hoja ya Magafu na alikubaliwa na hakimu huyo.

“Wakili Magafu kwa mujibu wa hoja zake hizo zimeonyesha uzalendo na amekomaa kitaaluma, kwani amekiri mbele ya mahakama hii kwamba hati ya kusafiria iliyowasilishwa awali na mteja wake ilikuwa imeisha muda wake na kwamba hivyo ndivyo afisa wa mahakama anatakiwa atende.

“Lakini Jumanne iliyopita mteja wake alivyopewa dhamana, upande wa mashtaka ulipinga kwa nguvu zote hati hiyo ya kusafiria isipokelewe, hivyo haiingii akilini kwamba hati hiyo iliyokwisha muda wake ilitolewa mahakamani hapa bila kukusudia.

“Hakimu ni wewe mwenyewe ulimuuliza mara mbili na sisi ni mashahidi, na mshitakiwa alikana kwamba hana hati nyingine ya kusafiria, kwakuwa sisi tulipinga utolewaji wa hati hiyo, hivyo hoja ya Magafu kuwa hawakuwa wamedhamiria kuihadaa mahakama, si ya msingi,” alidai Mwangamila huku akionyesha kujiamini.

Aliendelea kudai kuwa kutokana na hali hiyo, ni dhahiri shahiri kuwa Liyumba si muaminifu na haaminiki, hawana pingamizi la kufutwa kwa amri ya kukamatwa ila wanapinga ombi la kutaka asifutiwe dhamana, kwasababu mshitakiwa huyo ameonekana si mwaminifu.

“Ili siku nyingine mshitakiwa awe mwaminifu, sisi upande wa mashtaka tunaomba afutiwe dhamana, arudishwe mahabusu hadi tutakaporidhika kwamba ametimiza masharti ya dhamana, ili sisi tuwe tumepata majibu ya hati zilizotumika kumdhamini kutoka kwenye taasisi za serikali kama ni halali au la,” alidai Mwangamila.

Aidha, Magafu aliinuka kwenye kiti na kudai kuwa dhamana ni mkataba kati ya mahakama na mshitakiwa na kusisitiza kuwa mteja wake hakufanya makusudi kuwasilisha hati hiyo iliyomaliza muda na kuongeza kuwa mtu akitoka jela huwa amechanganyikiwa.

Baada ya kumalizika kwa kesi hiyo saa 9:04 Liyumba alipakiwa kwenye basi la Jeshi la Magereza chini ya ulinzi mkali, lakini hata hivyo alikosa kiti cha kukaa kwenye basi hilo na kulazimika ‘kushika bomba’ huku mahabusu waliokuwa kwenye basi hilo wakishangilia na kumwambia ‘karibu, umerudi tena gerezani.’

Nje ya mahakama hiyo umati mkubwa wa watu ulikuwa umetanda kushuhudia basi lililombeba mshitakiwa huyo likiondoka kuelekea gerezani.

Wakati Liyumba akisimama kwenye basi hilo, mshitakiwa mwenzake ambaye ni Meneja Mradi wa Benki Kuu, Deogratius Kweka, anayetetewa na mawakili wa kujitegemea, Profesa Mgongo Fimbo na Hurbet Nyange, alipandishwa peke yake kwenye Toyota Land Cruiser, lenye namba za usajili STK 4479 na kurudishwa gerezani.

Liyumba aliwasili mahakamani hapo saa 2:47 akiwa kwenye gari lenye namba za usajiri T 526AVB, aina ya NOAH, ambapo alitangulia kushuka wakili wake Magafu, akafuata Liyumba.

Wakili wake akawaambia waandishi wa habari ambao walifika mahakamani hapo tangu saa 12:45 asubuhi, wampige picha mteja wake na alivyoshuka moja kwa moja alikwenda kwenye Ofisi ya Mkuu wa Waendesha Mashtaka, Kenyela, ambapo alikaa hadi saa 3:30 na kuingizwa kwenye mahabusu ya mahakama hiyo hadi saa 5:10 alipoingizwa mahakamani.

Liyumba na Kweka, wanakabiliwa na matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuidhinisha ujenzi wa minara pacha ya BoT, maarufu kama ‘Twin Towers’ na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

No comments: