Wednesday, February 25, 2009

Kocha Mziray adai M mfumo wa Maximo unakwaza wachezaji


Kiungo mshambuliaji wa Taifa Stars, Mrisho Ngassa,hana hofu na vipimo kutambua kama
anatumia dawa za kuongeza nguvu.
Na Dorice Malyaga

ALIYEKUWA kocha wa Taifa Stars, Syllersaid Mziray, amesema mfumo anaotumia kocha Mbrazil Marcio Maximo ni mgumu kutokana na uzoefu mdogo wa timu yetu ya Taifa.


Akizungumza jijini jana Mziray alisema timu ya taifa mpaka sasa ina uwezo mkubwa wa kufanya vizuri kwenye mashindano yoyote mpaka sasa cha msingi ni kubadilisha mfumo unaotumika sasa na kuhakikisha wachezaji kushirikiana katika kuzuia na kushambulia kwa pamoja.


Alisema mpaka sasa kwenye michuano ya CHAN anaipa namba moja timu ya Zambia kutokana na staili wanayoitumia wakishirikiana katika kuzuia na kushambulia kwa ujumla huku wakitumia pande zote mbili na pasi za uhakika.


Mziray alisema endapo timu ya Tanzania ingefanya mashambulizi kama ya Zambia ilikuwa na uhakika wa kushinda mechi yao dhidi ya Senegal iliyopigwa bao 1-0. Stars jana ilikuwa ikicheza na wenyeji Ivory Coast.


“Kitu kingine ni kuingiza wachezaji wazuri, katika dakika za mwishoni ili kufanya mashambulizi hii pia inachangia kutopata magoli kwa haraka... Wasenegal walitushambulia kipindi cha kwanza na wakafanikiwa kupata goli lakini kipindi cha pili walicheza kwa kujihami na ndiyo maana hatukuweza kupata nafasi ya kufunga,”


“Stars itafanya vizuri endapo itabadili mfumo unaotumiwa sasa mtindo huu wa kucheza 3,5,2 unapoteza mipira mingi kutokana na viungo kuwa wengi hali ambayo inasababisha safu ya ushambuliaji kufa'' alisema Mziray.


Akiuzungumzia ubora wa Maximo alisema ni kocha mzuri mwenye kila namna ya kuigwa na makocha wote kwa kuisaidia timu yetu kufikia hatua iliyofikia sasa kwa kuonekana katika ulimwengu wa soka na anapongeza wadhamini na taifa kwa ujumla kwa kuinga mkono Taifa Stars.


Hata hivyo, Syllersaid, aliwataka Watanzania kutokuwa vigeugeu na kusahau kwa kipindi kifupi matokeo na mwenendo wa timu ya taifa.


Mziray alisema kuna haja ya kuwa na mipango ya muda mrefu katika kuitengeneza soka ya Tanzania lakini si kuwa na mipango ya kukurupuka, kuwa unalala ukiamka unataka ushindi.

No comments: