Tuesday, January 20, 2009

Ufisadi wa kutisha wagundulika Kiwira

• Shellukindo: Tutaonana na Ngeleja Dodoma


na Christopher Nyenyembe, Kyela




WIMBI la ufisadi linaendelea kuiandama Serikali ya Awamu ya Nne, baada ya kugundulika matumizi mabaya ya sh bilioni 13 kwenye mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, uliopo mkoani Mbeya.

Mbunge wa Kishapu, Fred Mpendazoe (CCM), ndiye aliyeibua tuhuma hizo nzito alipotaka kujua fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kukarabati mgodi huo zilivyotumika kutokana na matatizo katika mgodi huo kuzidi kushamiri siku hadi siku.

Mapendazoe ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo ipo mkoani hapa chini ya Mwenyekiti wake,William Shelukindo, alihoji hayo kwenye kikao kilichowakutanisha wakuu wa wilaya za Ileje, Kyela na wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama kama wamewahi kusikia au wana taarifa kwamba serikali ilitoa sh bilioni 13 kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya mgodi huo.

“Ndugu Mwenyekiti, ninachofahamu kupitia ripoti ya Jaji Mark Bomani, sh bilioni 13 zilitolewa kwa ajili ya ukarabati wa mgodi wa Kiwira, tunaambiwa mpaka sasa hivi hakuna chochote kilichofanyika, je, fedha hizo zilifikishwa au zimeishia wapi?” alihoji Mpendazoe.

Huku wajumbe wengi kwenye kikao hicho wakishangazwa na uwepo wa fedha hizo, inadaiwa kuwa serikali ina hisa asilimia 20 na mwekezaji Kampuni ya Kiwira Cool and Power (KCP) ina asilimia 80, hawajui kiasi hicho kikubwa cha fedha kilivyotumika.

Kauli ya mbunge huyo kuhoji mahali zilipoishia fedha hizo huku hakuna hata mbunge mmoja kwenye kamati hiyo aliyewahi kuuona mkataba wa ubinafsishaji uliowekwa kati ya serikali na mwekezaji, hoja hiyo nzito ilionekana kumshtua Mwenyekiti wa kamati hiyo, William Shellukindo, ambaye alitaka uchunguzi ufanyike kwanza mara moja.

Kwa kuonyesha kuwa alichokisema ni sahihi, Mpendazoe aliinuka na kufuata kitabu chenye taarifa ya Jaji Bomani kuwa alitoa ushauri akiitaka serikali ichunguze kwa kina mahali zilipopelekwa fedha hizo mwaka 2006 kwa ajili ya ukarabati wa mgodi huo.

“Naomba muangalie ukurasa wa 119 wa taarifa ya Jaji Bomani, alishauri serikali ichunguze uhalali wa matumizi ya sh bilioni 13 za ukarabati, haiwezekani kiasi kikubwa cha fedha kama hizo zifikishwe katika mgodi huo leo hii, wawekezaji wanashindwa kununua hata baruti, hatuwezi kuridhika na hali hii,” alisema Mpendazoe.

Baada ya hoja hiyo, Mwenyekiti wa Kamati, Shelukindo, aliwageukia wakuu wa wilaya za Kyela, Hussein Mashimba na Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Esther Wakali, kama serikali kuu imewahi kuwaeleza kuwa imewekeza kiasi hicho cha fedha kwenye mgodi huo na wamewahi kuuona mkataba wa serikali na mwekezaji.

Swali hilo lilionekana kuwa gumu baada ya wakuu hao huku kila mmoja akijibu anavyoelewa kwamba hawajawahi kusikia wala kuambiwa kama kuna mabilioni ya fedha yamewahi kumwagwa Kiwira na hawajawahi kuona mkataba uliosainiwa kati ya serikali na mwekezaji.

“Ndugu mwenyekiti mimi kama mkuu wa wilaya kazi yangu kwa kushirikiana na Kamati yote ya Ulinzi na Usalama tumekuwa tukifanya kazi ya kuzuia migomo ya wafanyakazi ili kuepusha hujuma na hilo tumefanikiwa, lakini hatujui chochote wala Wizara ya Nishati na Madini haina mawasiliano na sisi kuhusu Kiwira,” alisema Mashimba.

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Wakali alisema kuwa hajui chochote kuhusu mkataba au fedha zilizowahi kutolewa, kwani halmashauri ya wilaya hiyo ndiyo inayolipwa ushuru lakini nayo inadai fedha za ushuru bila mafanikio, huku shughuli za uzalishaji zikiwa zimeshuka kwa kiasi kikubwa.

Baada ya majibu hayo, Shelukindo alimgeukia ofisa wa Madini kutoka makao makuu, Dar es Salaam, aliyetumwa kuongozana na kamati hiyo, alipoulizwa kama aliwahi kuuona mkataba wa serikali na mwekezaji, alijibu hajui kitu chochote.

Swali hilo lilionekana kuwa mwiba mkali kwa ofisa huyo, Jerad Remmy, ambaye alikiri wazi kutokufahamu chochote kuhusu mkataba wa Kiwira na serikali na kwamba hajawahi kuuona na hafahamu mambo mengi yanayoihusu serikali kupitia wizara hiyo na KCP.

“ Mwenyekiti sifahamu chochote wala sijawahi kuuona mkataba wa serikali na mwekezaji, hilo swali linaweza kujibiwa na waziri mwenye dhamana, kwa kuwa ndiye anayeweza kuwa na jibu sahihi kwa upande wa serikali, kweli sijui chochote wakati mkataba unasainiwa sikuuona,” alisema Remmy.

“Wapo watu wanaosema kuwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imefadhiliwa na wawekezaji ili isifanye kazi vizuri na waandishi wa habari wamekuwa wakitupigia simu, nawaambia huyo atakaye kuja kutuhonga ndio mwisho wake, wote tunajitosheleza, kazi tuliyonayo sasa ni kusaka mafisadi tu, huyu Waziri wa Nishati na Madini tutaonana naye bungeni,” aliongeza.

Mbali ya madai hayo, kamati hiyo ya Bunge ilihoji mambo mbalimbali yanayokwamisha shughuli za uzalishaji katika mgodi huo, na sababu zilizochangia mwekezaji ashindwe kujenga mtambo wa kuzalisha umeme wa megawati 200 kama walivyowekeana mkataba na TANESCO.

Kusimimama kwa shughuli za uzalishaji kumewafanya zaidi ya wafanyakazi 500 katika kiwanda hicho wakose mishahara tangu Agosti mwaka jana na maofisa wa juu inadaiwa kuwa wengi hawajalipwa mishahara yao tangu mwezi Mei mwaka jana na haieleweki wanaishije.

Kamati hiyo ya Bunge ikiwa na Makamu Mwenyekiti wake, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kyela, aliwaomba wafanyakazi hao kuwa na subira wakati kazi inayofanywa na wabunge hao itakapowasilishwa bungeni na kuishauri serikali kuhusu hali halisi waliyoiona.

No comments: