Tuesday, January 20, 2009

Kagoda njia nyeupe

• DPP, waziri wanawa rasmi mikono


na Salehe Mohamed




NDOTO za Watanzania kuona Kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd iliyochota kiasi cha sh bilioni 40 katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaendelea kufifia baada ya kubainika kuwa serikali haina ushahidi wa kutosha kuiburuza mahakamani.

Kukosekana kwa ushahidi huo kunaelezwa ni mipango madhubuti iliyoandaliwa na baadhi ya viongozi waliopo na waliondoka serikalini kwa kushirikiana na wafanyabiashara maarufu kupoteza nyaraka zote ambazo zingesaidia kampuni hiyo kufikishwa mahakamani kama walivyofikishwa baadhi ya watuhumiwa wengine waliochota fedha kwenye akaunti hiyo.

Pamoja na Rais Jakaya Kikwete, kukabidhi mafaili ya watuhumiwa wote wa wizi wa EPA kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Elieza Feleshi, miezi miwili iyopita, ofisi yake imeshindwa kupata ushahidi wa kutosha kuishtaki Kagoda kama iliyotarajiwa na wengi.

Kampuni hiyo ambayo umiliki wake unahusishwa na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) inadaiwa walichota fedha hizo kwa ajili ya kusaidia kampeni ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 ambao CCM iliibuka na ushindi wa kishindo.

Chanzo cha habari kutoka ofisi ya DPP, kiliiambia Tanzania Daima Jumapili, kuwa wamiliki wa Kagoda walijua nini kitatokea baada ya wizi huo, hivyo kwa kushirikiana na viongozi walifanya kila njia kuhakikisha hawaachi nyaraka zozote ambazo zingekuja kuwaleta matatizo siku za usoni.

Miongoni mwa mbinu zilizotajwa kutumiwa na wahusika hao ni kwenda benki na kunyofoa nyaraka zote zilizokuwa zikionyesha mtu na akaunti ambayo fedha hizo ziliingia, nyaraka za umiliki wa kampuni katika Wakala wa Usajili wa Biashara na Makampuni (Brella) nazo mpaka sasa hazijulikani zilipo.

Chanzo hicho kimeongeza baada ya kelele za ufisadi kuzidi hapa nchini na Kampuni ya Kagoda kuandamwa, wamiliki halisi walianza kujawa na hofu ya kutajwa hivyo wakaamua kuwaendea baadhi ya viongozi na kutoa tishio kuwa kama hawatalindwa katika kashfa hiyo basi watakuwa radhi kuueleza umma walivyoshirikishwa katika wizi huo.

Kutokana na tishio hilo, baadhi ya viongozi waliopo serikalini na wale waliomaliza muda wao waliwahakikishia wamiliki hao kuwa kamwe hawataguswa kwa kuwa kampuni hiyo imebeba siri nzito ambayo ikiwekwa hadharani taifa litatikisika.

“Wamiliki wa Kagoda wanajulikana lakini serikali haiwezi kuwakamata kwa kuwa hakuna ushahidi lakini pia wana siri nzito, ndiyo maana wizi wa nyaraka ulifanyika kwa kiwango cha juu,” kilidokeza chanzo chetu.

Sakata la Kagoda linaonekana kukosa mwelekeo uliotarajiwa na Watanzania baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe juzi kuweka bayana kuwa hawawezi kuishitaki kampuni hiyo kwa kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kufanya hivyo.

Chikawe alikaririwa na vyombo vya habari kuwa serikali kamwe haiwezi kumuonea mtu kwa kumpeleka mahakamani bila ya kuwa na ushahidi wa kutosha ndiyo maana Kampuni ya Kagoda haijaguswa.

“Serikali hatuwezi kufanya kazi kwa shinikizo la kisiasa, tunampeleka mtu au kampuni mahakamani kwa mujibu wa taaluma ya sheria na pia sisi si wapelelezi” alikaririwa Chikawe.

Wakati serikali ikibaninisha msimamo huo wa kutokuwa na ushahidi wa kuishtaki kampuni ya Kagoda, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamesema uamuzi huo una lengo la kulinda ufisadi uliofanywa na viongozi waliopo madarakani na waliomaliza uongozi, jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya taifa.

Miongoni mwa viongozi hao ni, Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe (CHADEMA), alisema vielelezo alivyonavyo vinaonyesha jinsi CCM ilivyochota fedha hizo na kuzitumia katika kampeni za uchaguzi wa 2005, ndiyo maana serikali imepata kigugumizi kuifikisha mahakamani Kampuni ya Kagoda.

Kampuni ya Kagoda Agriculture, inayotuhumiwa kuchota sh bilioni 40 katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) kupitia Benki Kuu ya Tanzania, wizi huo ulimfanya Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa aliyekuwa Gavana wa BoT, marehemu Daudi Balali.

Kutengua uteuzi huo kulikuja baada ya ukaguzi uliofanywa na Kampuni ya Ernst&Young na kubaini wizi wa sh bilioni 133 katika akaunti hiyo.

Hadi sasa jumla ya watuhumiwa 20 tayari wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kujibu tuhuma za wizi huo huku kati yao 19 wakipata dhamana na mmoja kuendelea kusota rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti

No comments: