Sunday, November 9, 2008

Makamba aigawa CCM

MGOGORO unaotishia uhai wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeshika kasi baada ya baadhi ya wabunge wa chama hicho, kuzidi kumshinikiza Katibu Mkuu wao, Yussuf Makamba, ajiuzulu kwa madai ya kukidhoofisha chama huku kundi jingine likifanya juu chini kujaribu kumnusuru.

Wakati kundi moja la wabunge likitoa kibano hicho kwa Makamba, kundi la viongozi wa CCM, Ofisi Ndogo Dar es Salaam na Dodoma, limejitokeza kumtetea kwa madai kuwa wabunge hawana uwezo wa kumtaka Makamba ‘aachie ngazi’. Kwa kufanya hivyo watakuwa wamekiuka kanuni na taratibu za chama.

Vyanzo vyetu vya habari kutoka Dodoma ambako juzi kikao cha wabunge wa CCM kilifanyika, zinaeleza kuwa wabunge hao wamemtaka Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kutengua uteuzi wa Makamba kwa sababu kadhaa zikiwamo kudaiwa kuwatumia watu wasiojulikana kufanya kampeni katika Jimbo la Tarime na kusababisha CCM ishindwe.

Wabunge hao walitaka Makamba pamoja na baadhi ya wajumbe wa sekretarieti wang’oke, kwa madai kuwa wapo wenye vyeo zaidi ya vitatu wakati kuna baadhi ya makada wasio na cheo hata kimoja lakini wana uwezo - tena kuwashinda waliolimbikiziwa vyeo.

Waliwataja viongozi wenye vyeo zaidi ya kimoja mbali ya Makamba, ambaye ni kiongozi mmoja wa juu serikalini mwenye wadhifa wa kitaifa ndani ya chama, na John Chiligani, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; mbunge na Katibu wa Uenezi na Itikadi Taifa wa CCM.

Waliwataja wanachama wanaodaiwa kukumbatiwa na Makamba na aliowatumia kwenye kampeni za Tarime kuwa ni Richard Hiza Tambwe, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Propaganda; na Shaibu Akwilombe - wote waliojiunga na CCM hivi karibuni wakitokea vyama vya upinzani.

“Kitendo cha Makamba kuwatumia Tambwe, Akwilombe na Steven Mashishanga kwenye kampeni hizo badala ya kuwatumia wenyeji wa eneo hilo, ndicho kilichochangia kwa kiasi kikubwa kulikosa jimbo hilo kwa vile hawakuwa wakijua siasa za Tarime zinavyofanywa,” alisema mmoja wa wabunge katika mkutano huo.

Wabunge hao walitaja sababu nyingine ya CCM kushindwa Tarime kuwa ni kitendo chake cha kulala nyumbani kwa mfanyabiashara Mwita Gachuma, kwa madai kuwa hatua hiyo iliwagawa wana-CCM, kwani mfanyabiashara huyo amekuwa akitajwa kuwa na tofauti za kisiasa na kada mwingine wa chama hicho wa huko huko Tarime, Kisyeri Chambiri.

Wabunge hao ambao baadhi yao ni wajumbe wa kikao cha Halmashauri Kuu ya (NEC), kinachokutana wiki hii Dodoma, wamepania kuleta hoja hiyo ndani ya kikao hicho na baadhi ya wajumbe wameshawasili kwa ajili ya kikao hicho.

Wakati wabunge wakitoa shinikizo hilo kwa Makamba, viongozi wa Ofisi Ndogo ya CCM, Dar es Salaam na Dodoma, walisema wabunge hao hawana mamlaka ya kumwengua Makamba na kwamba wamekiuka kanuni na taratibu za chama.

Taarifa iliyotolewa na Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya tawi la CCM, Ofisi Ndogo Dar es Salaam, imemtetea Makamba kuwa ni mtu safi. Shutuma zilizotolewa dhidi yake na baadhi ya wabunge ni za uongo.

“Kamati imeshindwa kuelewa kama kweli taarifa hizo za kwenye vyombo vya habari zilitoka kwa wabunge wa CCM hadi hapo itakapothibitishwa na wao wenyewe,” ilisema taarifa hiyo.

“Tumeshindwa kuamini kutokana na kufahamu kwamba kamati ya wabunge wa CCM ina majukumu yake yaliyoainishwa vizuri na hayahusiani hata kidogo na masuala ya kupinga au kutaka kumwondoa kiongozi yeyote katika ngazi ya chama. Kamati ya siasa ya tawi inaamini kuwa wabunge wetu ni waelewa, wenye ufahamu mkubwa wa majukumu yao na kwamba hawawezi kufikia uamuzi huo,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa nyingine ya kumtetea Makamba ilitoka Dodoma ambako Kamati ya Siasa Tawi la Makao Makuu Dodoma ilisema kuwa tuhuma hizo hazina maana na kuwataka wana-CCM wazipuuze.

Taarifa hiyo ilibeza tabia ya baadhi ya viongozi wa CCM kutumia vyombo vya habari badala ya vikao halali vya chama katika ngazi husika kuwa ni ukiukwaji wa katiba, kanuni na maadili ya uongozi.

Katika hatua nyingine, kinyang’anyiro cha kuziba nafasi ya mjumbe wa NEC iliyoachwa wazi na Jaka Mwambi, kimeshika kasi na kuwagawa wajumbe katika makundi.

Zaidi ya wagombea 30 wamejitokeza kuziba nafasi hiyo, lakini waliopendekezwa na kikao cha Kamati Kuu (CC) ni watatu. Nao ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba, Meneja Uhusiano wa Benki ya National Microfinance (NMB), Shy-Rose Bhanji, na Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Londa.

Mwambi alikuwa mjumbe wa NEC lakini nafasi yake ilibaki wazi baada ya kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania Urusi. Nafasi hiyo itajazwa katika kikao cha NEC wiki hii.

No comments: