Sunday, November 9, 2008

EPA yamnasa kigogo wa CCM

na Happiness KatabaziIDADI ya watuhumiwa wa wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezidi kuongezeka, baada ya jana watuhumiwa wengine watatu, akiwemo kigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajab Shabani Maranda, kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Mbali ya Maranda, ambaye ni Katibu wa Uchumi na Fedha mkoani Kigoma, wengine waliofikishwa mahakamani jana ni mfanyabiashara maarufu wa mkoani Kilimanjaro na Arusha, ambaye pia ni mmiliki wa Kampuni ya Njanke Enterprises Ltd, Japhet Lema na Farijala Shabani Hussein.

Wakisomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Hadija Msongo, Mwanasheria wa Serikali, Edger Luhoga, alidai kuwa Farijala na Maranda wanakabiliwa na mashitaka matano likiwemo kosa la kula njama, wizi, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi na kujipatia ingizo la fedha kwenye akaunti yao.

Alidai katika tarehe na mwezi tofauti mwaka 2005, jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao waliwasilisha nyaraka za kughushi katika Benki ya Afrika, wakijifanya wamiliki wa Kampuni ya Kiloloma & Brothers iliyonunua deni la sh 3,868,805,737.13 kutoka Kampuni ya BC Cars Exports Ltd ya Mumbai, nchini India.

Katika kesi hiyo, Hakimu Msongo alitoa dhamana kwa washitakiwa kwa sharti la kila mshitakiwa kutoa nusu ya fedha zinazodaiwa kuibwa, wadhamini wawili ambao wataweka bondi ya sh milioni 900 au hati za mali isiyohamishika, yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha na kwamba ziwe zimefanyiwa thamini na mamlaka husika.

Pia washitakiwa hao wametakiwa kuacha hati za kusafiria mahakamani. Walishindwa kutimiza masharti na kurudishwa rumande hadi Novemba 11 mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa.

Katika kesi ya pili, mtuhumiwa Maranda anakabiliwa na makosa manne, yakiwemo shitaka la kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, wizi na kujipatia ingizo kwenye akaunti yake isivyo halali.

Katika kesi hiyo iliyopo mbele ya Hakimu Henzironi Mwankenja, Wakili wa Serikali, Fredrick Mnyanda, alidai kati ya mwaka 2004 na 2005, mtuhumiwa huyo alijifanya mmiliki wa kampuni hewa ya Rasshes, iliyoteuliwa kukusanya madeni ya Kampuni ya General Market & Co Ltd na kujipatia ingizo la fedha kutoka BoT, lenye thamani ya sh milioni 200.7.

Kwa upande wa serikali, ilisema upelelezi umekamilika na kwamba dhamana ipo wazi na mshitakiwa atatakiwa alipe nusu ya kiasi cha fedha anazotuhumiwa kuiba, au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika na wadhamini wawili ambao kila mmoja ataweka bondi ya sh milioni 69.

Aidha, katika kesi ya tatu, watuhumiwa Farijara na Maranda, wanadaiwa katika tarehe tofauti mwaka 2005, walighushi hati za BRELA, zinazoonyesha kuwa wao ni washirika katika Kampuni ya Money Planers&Consultant Ltd na kufanikiwa kujipatia ingizo la fedha kwenye akaunti yao, sh bilioni mbili kutoka BoT, na kwamba wameteuliwa kukusanya deni la Kampuni ya BC.Grancel&Co Ltd ya Ujerumani.

Watuhumiwa hao ambao walisomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Nikumalila Mweseba, walikana tuhuma hizo na kesi kuahirishwa hadi Oktoba 11 mwaka huu, itakapotajwa tena.

Hakimu Mwaseba, alipanga tarehe hiyo baada kukataa ombi la mawakili wa utetezi, Mpaya Kamala na Martin Matunda, kuomba kesi hiyo iahirishwe hadi leo, kwa kuwa wateja wake watakuwa wamekamilisha masharti ya dhamana.

Katika kesi ya nne, Farijala na Maranda wanakabiliwa na makosa saba ya jinai na kwamba kati ya mwaka 2006 na wenzao wasiojulikana walikula njama na kutenda kosa kwa maelezo wao ni wamiliki wa Kampuni ya Mbare Farm na kujipatia sh bilioni 1.6, kutoka BoT, kwa madai kwamba waliteuliwa kununua deni la Kampuni ya Lakshni Textile Mills Coral Ltd.

Katika kesi ya tano ambayo inamkabili Japhet Lema anayetetewa na wakili wa kujitegemea, Ezra Mwandu, ilidaiwa katika tarehe tofauti mwaka 2006, alitumia Kampuni ya Njake Enterprises Ltd kuchukua deni lenye thamani ya sh bilioni 2.6 la Kampuni ya C.Itoh&Co Ltd ya Japan, kutoka BoT.

Mtuhumiwa Lema ambaye alisomewa shitaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Euphemia Mingi, alikana tuhuma hizo na wakili wake aliiomba mahakama imwachie huru kwa jana, ili aweze kuletwa leo kwa ajili ya kupatiwa dhamana.

Wakili huyo alidai mtuhumiwa huyo alipigiwa simu Jumanne na makachero wa Polisi wakimtaka afike jijini Dar es Salaam bila ya kumweleza kitu walichomwitia.

“Mteja wangu alitii amri hiyo na kufika jijini, lakini ghafla jana aliambiwa na makachero hao anafikishwa mahakamani, hivyo ndugu zake ambao wangemdhamini walipata taarifa jana asubuhi na kwamba walikuwa wameanza safari ya kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kuja kumdhamini,” alieleza.

Hata hivyo, Hakimu Mingi alikataa ombi hilo na kuamuru mtuhumiwa huyo apelekwe rumande na kuahirisha shauri hilo hadi leo, kwa ajili ya mtuhumiwa huyo kupewa dhamana.

Katika hatua nyingine, watuhumiwa 10 ambao walifikishwa mahakamani hapo juzi, jana walifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kukamilisha taratibu za dhamana.

Hata hivyo, mtuhumiwa Johnson Lukaza hakufikishwa mahakamani jana na badala yake wakili wake, Alex Mgongolwa na ndugu zake walifika mahakamani hapo kwa ajili ya kukamilisha taratibu za dhamana.

Baada ya ndugu hao kukamilisha tarartibu hizo, upande wa mashitaka uliandika hati ya kumtoa rumande mtuhumiwa huyo, ili aletwe leo kwa ajili kudhaminiwa.

Hata hivyo, mahakimu mbalimbali wanaosikiliza kesi nne zinazowakabili watuhumiwa wanne wenye asili ya Kiasia, Jayantkumar Chandubhai Patel ‘Jeetu Patel’, Devendra K. Vinodbhai Patel, Amit Nandy na Ketan Chohan, waliongeza masharti ya dhamana kwa watuhumiwa hao, kwa kuwataka wawasilishe hati za mali zisizohamishika, ambazo zitakuwa zimefanyiwa tathmini na mamlaha husika.

Kesi hizo zimeahirishwa hadi Novemba 20 mwaka huu zitakapotajwa tena na washitakiwa hao kukamilisha taratibu za dhamana.

Aidha, katika kesi nyingine inayomkabili Jeetu Patel na wenzake watatu, inatarajiwa kutolewa uamuzi wa kupatiwa dhamana leo katika mahakama hiyo.

No comments: