Monday, August 25, 2008

Wiki ya moto bungeni

na Mwandishi Wetu, Dar, DodomaBUNGE la Jamhuri ya Muungano, linatarajiwa kuwaka moto katika siku tano zilizosalia kutokana na mijadala mizito inayotarajiwa kutawala bungeni wiki hii.

Hakuna shaka kuwa mjadala huo wa Bunge kwa kiwango kikubwa unaweza kuirejesha upya hoja ya wizi wa sh bilioni 133 kutoka katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).

Baadhi ya wabunge waliozungumza na Tanzania Daima kwa masharti ya kutotajwa majina hadi hapo watakapochangia mjadala wa hotuba ya rais wanasema, uamuzi wa Kikwete kutochukua mkondo wa kisheria dhidi ya makampuni 13 yaliyoiba sh bilioni 90 kupitia EPA kwa kutumia nyaraka za kughushi unaonekana kutaka kuwanusuru baadhi ya watu.

Wasiwasi huo wa baadhi ya wabunge unaweza kupimwa pia na kauli zilizotolewa mwishoni mwa wiki na Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambaye amemwagiza Katibu wa Bunge kupanga ratiba kwa ajili ya kuijadili hotuba hiyo wiki hii.

Mbali ya suala la EPA, mjadala huo unatarajiwa kujikita kutaka kupata ufafanuzi kuhusu suala la hadhi ya Zanzibar na mwelekeo wa serikali mahala ilipo, ilipotoka na inakoelekea, hasa baada ya kufikisha nusu ya muda wake wa miaka mitano madarakani.

Leo Rais Jakaya Kikwete, atarejea tena bungeni lakini si kwa ajili ya kutoa hotuba kama wiki iliyopita, bali atakuwa mwenyeji wa Rais wa visiwa vya Comoro, Ahmed Abdallah Mohamed Sambi, ambaye atapata nafasi ya kulihutubia Bunge.

Rais huyo wa Comoro anatarajiwa kulihutubia Bunge na moja kati ya mambo anayotarajia kuyazungumza ni kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kupeleka majeshi yake katika visiwa hivyo kumng’oa kiongozi wa kijeshi aliyegoma kuondoka madarakani, Kanali Mohamed Bakar.

Wakati kiongozi huyo wa Comoro akilihutubia Bunge, mawazo ya wabunge wengi yatakuwa yamejikita katika kujadili hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha na Uchumi, ambapo baadhi ya wabunge wameonyesha kukerwa na matumizi yake.

Wabunge wameonekana kutoridhishwa na matumizi yanayofanywa na wizara hiyo kwa kununua magari ya kifahari pamoja na kutoa misamaha ya kodi kwa kampuni za madini zinazodaiwa kupata faida kubwa.

Baadhi ya wabunge waliozungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa majina, wameilalamikia wizara hiyo kuwa inafanya baadhi ya mambo kwa anasa bila kuangalia vipaumbele vya taifa.

Lakini pamoja na yote, shughuli kubwa inayosubiriwa na wabunge wengi ni mjadala wa hotuba ya Rais Kikwete, aliyoitoa Alhamisi iliyopita na hasa kuhusu hatua alizozichukua juu ya wezi wa EPA.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete, alisema wezi hao wamefilisiwa mali zao na kunyang’anywa pasi za kusafiria wakati wananchi wengi walitaka kuona wakifikishwa mahakamani.

“Unajua alichokisema Rais Kikwete kuhusu wezi wa EPA, hakikubaliki kwenye jamii inayozunguka, kwanini wezi hawafikishwi mahakamani?” alihoji mmoja wa wabunge hao.

Mbali ya mjadala wa hotuba ya rais, moto mwingine utaibuka bungeni baada ya Waziri Mkuu Pinda, atakapowasilisha ripoti ya Kamati ya Bunge, iliyochambua utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe, kuchunguza kashfa ya mkataba wa Richmond.

Habari ambazo Tanzania Daima imezipata jana mjini Dodoma, zilisema Pinda, atawasilisha bungeni taarifa rasmi ya utekelezaji wa mapendekezo hayo, yaliyowasilishwa serikalini Machi mwaka huu.

Agosti 7, mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Philip Marmo, aliahidi bungeni kuwa ripoti hiyo itawasilishwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kabla ya kuahirishwa kwa mkutano huo wa 12, unaoendelea mjini Dodoma.

Hoja ya Richmond, ilirejea tena bungeni wakati wa kipindi cha maswali na majibu Agosti 7 mwaka huu, baada ya Mbunge wa Ziwani, Ali Slimu (CCM), kutaka kujua ni lini serikali itatekeleza azimio la Bunge lililokuwa na mapendekezo 23, ambayo utekelezaji wake unasubiriwa kwa hamu na Watanzania wengi.

Kamati hiyo ilikamilisha kazi yake na kuwasilisha mapendekezo ya utekelezaji serikalini tangu Machi, mwaka huu.

Marmo alisema Waziri Mkuu Pinda, atafanya hivyo baada ya Bunge kupanga ratiba yake kupitia Kamati ya Uongozi ya Bunge.

Hatua hiyo inakuja wakati baadhi ya watendaji ambao walitakiwa kuwajibishwa au kuchukuliwa hatua kutokana na majina yao kutajwa katika ripoti ya Mbunge wa Kyela, Dk. Mwakyembe (CCM), wakiendelea na kazi zao.

Miongoni mwa waliokuwa wakitarajiwa kuchukuliwa hatua ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (TAKUKURU), Edward Hoseah.

Wengine ambao majina yao yalitajwa katika mkumbo huo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, ambaye kama ilivyo kwa Hoseah, anaendelea na kazi kama kawaida.

Richmond inatajwa kuwa kashfa kubwa kuikumba Serikali ya Awamu ya Nne tangu ilipoingia madarakani Desemba mwaka 2005.

Ukubwa wa kashfa hiyo unatokana na ukweli kwamba, ilisababisha kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa, kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, baada ya jina lake kuhusishwa katika mchakato ulioipa ushindi wa kuingiza nchini mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura Kampuni ya Richmond.

Mbali ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu, kashfa hiyo ilisababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, na yule wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha.

Kutokana na kujiuzulu kwa mawaziri hao watatu, Rais Jakaya Kikwete alifanya mabadiliko ya kwanza makubwa katika Baraza lake la Mawaziri.

Wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma kesho kinatarajia kufanya maandamano ya kumpongeza Rais Jakaya kwa hotuba aliyoitoa bungeni wiki iliyopita.

Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, alisema sherehe za aina hiyo zitafanyika nchi nzima, kwani alichokifanya Rais Kikwete ni cha kupongezwa na kinachoonyesha ukomavu wake kisiasa.

No comments: