Monday, August 18, 2008

Serikali yamnyang'anya Tibaigana gari


SAKATA la mauaji yenye utata ya vijana wawili, wakazi wa Dar es Salaam, Mine Chomba na Hija Shaha Salehe, yaliyotokea mwaka 2006, limechukua sura mpya baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrance Masha, kuagiza magari yote yaliyohusishwa na mauaji hayo, likiwamo analomiliki Kamanda wa zamani wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, kurudishwa ili uchunguzi ufanyike upya.


Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Waziri Masha, zinaeleza kuwa, magari hayo tayari yamesharejeshwa kwa ajili ya kufanyika uchunguzi kuhusiana na jinsi yalivyochukuliwa.

Inaelezwa kwamba, magari hayo yanayodaiwa kuwa mali ya marehemu Chomba, yalikamatwa na Polisi kwa muda mrefu, yakidaiwa kuwa ni ya wizi kabla ya kuuzwa kwa njia ya utata.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu juzi, Waziri Masha alisema kuwa, magari hayo yote yamesharudishwa kama alivyoagiza.

"Kama mlisikia wakati wa hotuba ya bajeti yangu bungeni, niliagiza magari yote yarudishwe na tayari yamesharudishwa," alisema Waziri Masha.

Kati ya magari hayo yaliyopaswa kurudishwa ni pamoja na Toyota RAV 4 ambalo lilinunuliwa kwenye mnada wa hadhara na Tibaigana.Hata hivyo, habari zilizopatikana kutoka kwa ndugu wa marehemu Mine, zinaeleza kuwa, tayari walishakwenda kumwona Waziri Masha kujua hatima ya suala la ndugu yao.
Mmoja wa ndugu hao, ambaye hakupenda kutajwa jina lake, alisema kuwa, walikwenda hivi karibuni kumwoma Waziri Masha na kwamba alisema ameshalishughulikia suala hilo kwa kuagiza magari hayo yarejeshwe.
Hata hivyo, Tibaigana aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari huko nyuma, akisema kwamba, gari hilo alilinunua kwa njia ya halali kupitia mnada wa hadhara.
Mine aliuawa Januari 13, mwaka 2006 katika baa ya Meeda, Sinza, Dar es Salaam, mauaji ambayo yanadaiwa kufanywa na Hija, ambaye aliuawa Januari 16 mwaka huo huo katika eneo la Kimara Temboni.
Baada ya kutokea mauaji hayo, ndugu walilalamikia mazingira ya vifo hivyo, wakidai kuwa yalifanywa na Polisi, madai ambayo yalimlazimu aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Raia, Harith Bakari Mwapachu, kuunda tume ya kuchunguza mauaji hayo.
Hata hivyo, ripoti ya uchunguzi huo haikutolewa hadharani na badala yake Mwapachu aliipeleka Ikulu kwa ushauri zaidi kutokana na kuhusisha majina ya baadhi ya vigogo wa polisi.
Utata huo, pia ulifanyika katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) na Mwapachu mwenyewe kuunda tume, kwa kuwa, Hija, ambaye aliuawa kinyama kifo chake kilitokea akiwa katika mikono ya polisi, lakini baadaye akaelezwa aliuawa na wananchi wenye hasira huku Mine akidaiwa kuuawa na Hija, lakini ndugu wanakataa wakidai wahusika ni polisi.
Hata hivyo, juhudi za Mwananchi kumpata Tibaigana kuzungumzia suala hilo jana hazikufanikiwa na hata alipopigiwa simu zake mbili za mkononi, zote zilikuwa zimezimwa.Source: Mwananchi

No comments: