Thursday, August 28, 2008

Leo ni leo Richmond

na Salehe Mohamed, Dodoma


WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, leo anatarajiwa kutoa ripoti ya mapendekezo ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya vigogo waliohusika, katika kashfa ya uingiaji wa mkataba wa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond.

Mapendekezo hayo yaliwasilishwa serikalini Machi, mwaka huu, na Kamati ya Bunge, yametokana na maazimio 23 ya Kamati Teule ya Bunge, iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe (CCM), iliyokuwa na kazi ya kuchunguza kashfa hiyo.

Miongoni mwa watu ambao Kamati Teule ilipendekeza wawajibishwe ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, John Mwanyika, na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hosea; na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.

Wengine walioguswa na kashfa hadi kusababisha kujiuzulu ni aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ni Dk. Ibrahim Msabaha, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini na baadaye Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, na Nazir Karamagi, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini,.

Baadhi ya wabunge waliozungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa majina yao, walisema wanatarajia ripoti hiyo itakidhi kiu ya wabunge na wananchi kwa kuwachukulia hatua wahusika bila kujali majina au nyadhifa zao.

“Hawa watu wachukuliwe hatua kikamilifu, hatutaki kusikia mambo kama yale ya watuhumiwa wa EPA ambao wamezidi kuongezewa muda wa kutanua,” alisema mmoja wa wabunge wa CCM kutoka kanda ya Ziwa.

No comments: