Monday, October 20, 2008

Kanumba, Rashida wamfanyia kitu mbaya Diof


Wawili hao walimfanyia kitu mbaya Diouf usiku wa kuamkia Oktoba 16, mwaka huu na kushuhudiwa na mwandishi wetu, ndani ya Ukumbi wa Mango Garden, uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambapo Bendi ya African Stars Twanga Pepeta International ilikuwa ikifanya onesho maalum la usiku wa Zain.

Habari zilidai kuwa katika tukio hilo, Diouf aliomba kupanda jukwaani kwa lengo la kuwaburudisha mashabiki wake wa zamani, ambapo mwimbaji huyo baada ya kuruhusiwa kufanya hivyo, alichukua kipaza sauti na kuanza kuimba wimbo wake wa zamani wa ‘Aminata’.

Mwimbaji huyo aliushangaza umati uliofurika ukumbini hapo baada ya kuacha kuimba jukwaani na kushuka chini kuelekea meza za mashabiki dakika chache baada ya kupanda jukwaani hapo.

Katika ‘staili’ hiyo, Diouf alijikusanyia kiasi kikubwa cha fedha baada ya kutuzwa na mashabiki mbalimbali ukumbini hapo, ambao kwa aliowafahamu alikuwa akiwataja majina yao na kuwapamba ndani ya wimbo huo.

Diouf aliendelea na zoezi hilo, ambapo alipoangaza macho na kuwaona Kanumba na Rashida alianza kuwapamba huku akiwafuata, lakini jambo lililowashangaza watu ukumbini hapo, wasanii hao walionekana kuhamahama meza kwa lengo la kumkwepa.

Habari ziliendelea kudai kuwa mwimbaji huyo hakuishia hapo, aliendelea kuwafuata tena huku akiwataja majina yao na kuwapamba lakini walionekana kumkwepa tena hali iliyomfanya aachane nao na kwenda meza za wateja wengine.
Baada ya tukio hilo, mwandishi wetu aliongea na Rashida juu ya kuhama meza kila alipofuatwa na mwimbaji huyo ambaye wengine walikuwa wakimtunza kila walipofuatwa, ambapo mrembo huyo alisema hakuna ulazima wa kumtuza mtu kwani huo ni uamuzi wa mtu binafsi.

Mwandishi wetu hakufanikiwa kuzungumza na Diouf wala Kanumba baada ya kupotezana nao ukumbini hapo na hata alipowatafuta kwa njia ya simu, hawakuweza kupatikana.

No comments: