Thursday, August 28, 2008

Mbunge: Ndege ya Rais iuzwe

na Salehe Mohamed, Dodoma


HOJA ya ndege ya rais imezuka tena bungeni baada ya Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa (CCM), kudai kuwa haina faida kwa taifa na kutaka iuzwe.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Fedha na Uchumi kwa mwaka wa fedha wa 2008/20009.

Alisema matumizi ya ndege hiyo kwa sasa, ambayo hivi karibuni iligongwa na gari la maofisa usalama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, hayakidhi mahitaji ya rais, kwani haitumiki anaposafiri nje ya nchi.

Alisema uwezo wa ndege hiyo iliyonunuliwa kwa bei kubwa hata kuibua malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na wabunge, ni kubeba watu 12 wakati rais anapokuwa na safari, huwa na ujumbe wa zaidi ya watu 18, hivyo haifai kwa matumizi yaliyolengwa licha ya kununuliwa kwa bei kubwa.

“Hii ndege haifai kwa matumizi yetu na ni vema ikauzwa kwa mabepari wanaohitaji kwa matumizi binafsi na sisi tuangalie ndege nyingine itakayokidhi mahitaji yetu,” alisema Mwambalaswa.

Alisema kwa hali ilivyo, hakuna ubishi kwamba ndege hiyo ni mzigo kwa taifa, kwani hata rais mwenyewe wakati mwingine hulazimika kuwaacha baadhi ya wajumbe anaopaswa kusafiri nao.

“Udogo wa ndege hiyo husababisha wajumbe wengine kutangulia sehemu anayokwenda rais, jambo ambalo kimsingi huondoa uhalisi wa ujumbe wa rais unaopaswa kuongozana na rais,” alisema.

Katika hatua nyingine, mbunge huyo alitaka Serikali iwe na sera ya ununuzi wa magari ili kuwa na magari maalumu ya kutemebelea viongozi kuendana na ngazi zao.

Alisema kwa sasa, kuna vurugu kubwa katika ununuzi, kwani kumekuwa na mashindano ya kubadilisha magari kati ya mawaziri, makatibu, wakurugenzi na watendaji wengine.

“Wenzetu Uingereza, India na mataifa mengine kuna sera na utaratibu wa viongozi kutembelea magari ya aina fulani, hivyo ni vema na sisi tukaanza utaratibu huo ili tusitumie fedha nyingi,” alisema Mwambalaswa.

Akijibu hoja ya ndege ya rais, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustapha Mkulo, alisema jambo hilo litaangaliwa na Serikali ili kuamua hatua za kuchukua.

“Siwezi kutoa jibu la haraka kama ndege hiyo iuzwe au la, lakini ushauri huo tutaufanyia kazi kuangalia nini kitawezekana, kwani lengo ni kuboresha…napenda kumhakikishia mheshimiwa mbunge kuwa ushauri wake tutaufanyia kazi,” alisema Mkulo,”

Kuhusu kuwa na sera ya ununuzi wa magari, alisema suala hilo ni la Wizara ya Miundombinu, Ofisi ya Rais Utumishi na Katibu Mkuu, lakini ana taarifa kuwa kuna mapitio yanafanyika.

Mapitio hayo yatakapokamilika, yataletwa bungeni kwa ajili ya kupata kibali na kila mmoja atajua kilichoamriwa na nini serikali inapanga katika jambo hilo.

No comments: