Wednesday, March 5, 2008

YOU ARE WHAT YOU EAT


IJUE UWEZO ZAIDI WA KITUNGUU SAUMU NA TANGAWIZI KATIKA AFYA YAKO!

Wiki iliyopita tulisoma kuhusu orodha ya baadhi ya vyakula venye nguvu ya kuponya matatizo mbalimbali ya kiafya. Katika makala hayo niliorodhesha baadhi ya vyakula kama vile samaki, uyoga na vingine vingi yakiwemo matunda kadhaa.

Baadhi ya wasomaji wetu walinipigia simu na kunitutumia ujumbe wakitaka kujua matumizi ya vyakula hivyo katika kuponya matatizo yao. Kimsingi katika makala hayo sikukusudia kuelezea njia za kuzitumia kuandaa vyakula hivyo ili kujitibu kama dawa.

Hayo nilikwishaeleza kwa utaratibu mwingine katika makala zangu zilizotangulia, lakini hapo nilikusudia kuorodhesha tu vyakula hivyo na faida zake unazozipata kila unapokula, kwa utaratibu wa kawaida na unaoutumia wewe siku zote.

Katika maisha ya sasa, ni vizuri sana kujua kila unachokula kina faida au madhara gani mwilini mwako, kwani unachokula leo, ndicho kitakachokufanya uugue au uwe mzima kesho, tiba au madhara ya chakula hujijenga mwilini kidogokidogo na matokeo yake huonekana baada ya muda mrefu.

Nikurudi kwenye swali la msingi ambalo waliuliza baadhi ya wasomaji kwamba waandae vipi vyakula au matunda niliyoyaeleza iwapo wanataka kutibu ugonjwa fulani. Kimsingi, kama nilivyosema hapo awali, hapa sikukusudia kufanya hivyo, bali nimekusudia kuonesha faida na uwezo wa vyakula hivyo katika miili yetu, hivyo unashauriwa kuvila vyakula hivyo kawaida kama unavyovila siku zote, ukielewa kuwa unajijengea kinga mwilini mwako au unajitibu ugonjwa fulani taratibu.

Katika makala ya leo, tutaangalia kwa kirefu uwezo wa KITUNGUU SAUMU katika uwezo wake wa kutumika kama dawa za anti-biotic. Vile vile tutaangalia kwa kirefu uwezo wa TANGAWIZI kutumika kama dawa ya maradhi mbalimbali, kama ilivyoelezwa na mwandishi Tanushree Podder katika kitabu chake cha You Are What You Eat:

Kitunguu saumu kimekuwa kikitumika kama dawa ya mitishamba, takribani miaka 5,000 iliyopita. Historia inaonesha kuwa wafungwa wa nchini China walikuwa wanatakiwa kula kitunguu saumu kibichi kila siku asubuhi ili kuimarisha afya zao.

Aidha inaelezwa zaidi kuwa nchini Misri, watumwa walikuwa wakilishwa vitunguu saumu na vitunguu maji ili wapate nguvu za kujenga ‘ma piramid’. Vile vile vitunguu vilikuwa vinatumika kama dawa ya kufukuza majini na mapepo wabaya.

Ukiacha ushahidi huo wa kiasili kuhusu uwezo na umuhimu wa kitunguu saumu kiafya, utafiti wa kisayansi umegundua pia kuwa kishina kimoja cha kitunguu saumu kina dawa sawa na uniti 100,000 za vidonge vya Pennicillin ambayo ni karibu ya robo dozi ya vidonge hivyo na havina madhara yoyote katika mwili wa binadamu.

KITUNGUU SAUMU:
kinaaminika kuwa na uwezo wa kuzuia aina mbalimbali za saratani, kama vile saratani ya tumbo, ngozi, matiti, koo na utumbo mkubwa. Aidha kitunguu saumu kina uwezo wa kudhibiti seli zisizaliane vibaya na kuleta madhara mengine mwilini.

Aidha, kitunguu saumu kina uwezo wa kushusha shinikizo la juu la damu, ili kupata matokeo yake katika kuponya maradhi hayo, unahitaji kuwa unakula angalau kitunguu saumu kimoja mpaka vitatu kila siku kwa muda wa miezi mitatu. Lakini hata utakapokula kiasi chochote utakachoweza kwa wale msio na maradhi yoyote, bila shaka mtakuwa mnajijengea kinga katika miili yenu.

Aidha ulaji wa vitunguu saumu vibichi, husaidia kurekeshi kiwango cha sukari kwa wagonjwa wa kisukari na manufaa yanapatikana zaidi kwenye vitunguu vibichi kuliko vya kupika au kukaanga. Vilevile unaweza kuchanganya asali na vitunguu saumu na kula pamoja kama dawa ya kuondoa mafua.

TANGAWIZI

Hii nayo ni dawa ya mitishamba yenye nguvu na maarufu sana nchini China, India na Japan. Imekuwa ikitumika katika nchi hizo kwa karne kadhaa na kuenea hadi Mashariki ya Kati, Spain na West Indies. Kwa mujibu wa historia yake, kwa mara ya kwanza Tangawizi ilitengenezwa nchini Jamaika ili kusaidia tatizo la ukosefu wa choo, kichefuchefu, ugonjwa unaotokana na kutembea kwa muda mrefu na uchovu wa asubuhi.

Tangawizi inaaminika kuwa na uwezo wa kuzuia kuchafuka kwa tumbo, kubana kwa kifua na kuumwa kwa kichwa. Kwa mujibu wa kitabu cha You Are What You Eat, katika bara la Asia, Tangawizi hutumika kuogea ili kuponya tatizo la kuziba kwa pua kutokana na mtu kuwa na ‘aleji’. Tangawizi husagwa na unga wake kutumika kuandaa kinywaji au inaweza kutumika ikiwa bado mbichi kwa kuwekwa kwenye maji ya moto na kunywa.

No comments: