Wednesday, March 19, 2008

Mtoto wa kigogo abambwa akijiuza


Mtoto huyo na wenzake kadhaa walinaswa katika mitaa ya Ohio, Mnazi mmoja na maeneo ya Buguruni usiku wa manane wakiwa katika mawindo yao.

Wasichana hao walitupwa rumande katika Kituo cha Polisi cha Buguruni jijini la Dar es Salaam mara baada ya kufikishwa kituoni hapo.

Hata hivyo, watu wanaomfahamu mtoto huyo wa kigogo walimwambia mwandishi wetu kuwa licha ya kufanya biashara hiyo haramu binti huyo yuko ‘njema’ kwao.

“Huyu msichana namfahamu, yuko fiti kwao Masaki, sijui ni kitu gani kinamzuzua hadi anakamatwa usiku wa manane akijinadi kwa wanaume,’’ alisema kijana mmoja aliyedai anamfahamu vema binti huyo wa kigogo.

Mtoto huyo wa kigogo alipohojiwa na mwandishi wetu alisema kuwa anafanya hivyo kwa ‘starehe yake’ kwani anapata kila kitu anachokihitaji nyumbani kwao.

“Mtoto wa mkurugenzi ndio nini? Acha nifanye mambo kwa raha zangu,” alisema msichana huyo huku akionyesha kukerwa na swali hilo la mwandishi.

Rafiki wa karibu wa msichana huyo, alimwambia mwandishi wetu kuwa pamoja na msichana huyo kujihusisha na biashara ya ukahaba, hafanyi hivyo kwa ‘njaa’ ya kutafuta fedha, bali kwa ajili ya kufurahisha nafsi yake.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi, Ilala, Faustine Shilongire alipoulizwa na gazeti hili kuhusu msako huo, alithibitisha kufanyika na akasema litakuwa ni zoezi la kudumu.

Shilongire aliongeza kuwa watakuwa wakiwakamata mara kwa mara makahaba hadi waache tabia hiyo, licha ya kutozwa faini aliyoiita kuwa ni ndogo wanapofikishwa mahakamani.

“Tutapambana nao kwa kuwakamata kwa kuwa ni tabia mbaya ambayo inachangiwa na mahakama kuwatoza faini ndogo sana ambayo wahusika wanamudu kuilipa,” alisema.

Zoezi hilo la kukamata makahaba limeibuka kutokana na amri ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro ambaye amekuwa mstari wa mbele kupiga vita biashara hiyo inayoaminika kuwa inachangia kusambaza ugonjwa wa Ukimwi.

No comments: