Wednesday, March 19, 2008

CCM waibeba Simba kuiua Enyimba
Habari moto-moto zilizolifikia gazeti hili, juzi, Jumamosi kutoka chanzo chetu na kuthibitishwa na Katibu Mkuu Msaidizi wa Klabu hiyo, Mohammed Mjenga zilisema vigogo hao wameamua kuchukua uamuzi huo baada ya kuona mambo hayaendi vizuri.

Ziliendelea kueleza kuwa baada ya kuona kuna uwezekano wa Simba kushindwa kwenda Nigeria kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Enyimba kutokana na kukosa fedha, wadau hao walijitolea gharama za kuisafirisha.

Hata hivyo, chanzo chetu hakikuwa tayari kuyataja majina ya vigogo hao, licha ya kuendelea kulihabarisha kwamba, vigogo hao wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali klabuni hapo ikiwa ni pamoja na kugharamia kambi na posho za wachezaji.

Championi likiwa linahaha kutafuta ukweli wa habari hizo ndipo lilipomnasa, Mjenga ambaye alikiri na kuongeza kuwa vigogo hao wa CCM wamekuwa wakishirikiana bega kwa bega na Kundi la Marafiki wa Simba ‘Friends Of Simba kuisaidia timu yao.

Katibu huyo aliweka bayana kuwa, licha ya vigogo hao kutoka serikalini na Friends of Simba, pia wapo wadau wengine kutoka taasisi binafsi ambao kwa mapenzi yao huisaidia Simba ili isonge mbele.

Baadhi ya vigogo wa CCM ambao wanadaiwa kuwa ni wanazi wakubwa wa Simba ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Sophia Simba, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Prof. Juma Kapuya.

Wengine ni Mbunge wa Rorya, Prof. Phillimon Sarungi, Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azzan, Mbunge wa Singida Mjini, Mohammed Dewji, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Rashid Mfaume Kawawa, Fredrick Sumaye na aliyejiuzulu hivi karibuni, Edward Lowassa.

Orodha ya vigogo hao wa CCM haina maana kwamba wao ndiyo waliohusika moja kwa moja kuisaidia Simba kwa kipindi hiki.

No comments: