Wednesday, March 19, 2008

Mr. Blue, Dully Skkes Watekwa


Chanzo chetu kilitujuza kwamba vijana hao, walitekwa Alhamisi iliyopita, majira ya saa 10 alasiri katika eneo la Tabata Kimanga, jijini.

Imelezwa kuwa watekaji waliotekeleza tukio hilo, walikuwa na mapanga, visu na silaha nyingine mbalimbali ambapo msanii Mr. Blue alijeruhiwa begani, shavuni na kwenye kiganja cha mkono.

“Blue amekatwa mapanga kwenye shavu, yaani karibu na sikio, begani na katika kiganja cha mkono, ingawa majeraha siyo makubwa sana,” kilisema chanzo chetu.

Aidha, chanzo hicho ambacho ni swahiba wa wanamuziki hao marafiki, kiliongeza kwamba kwa sasa Mr. Blue anatibu majeraha hayo, katika hospitali moja iliyopo Tabata (haijafahamika).

Akisimulia tukio zima lilivyokuwa, mtoa habari wetu, alisema: “Mr. Blue alikuwa akitokea katika mizunguko yake katikati ya jiji na baadaye akaamua kwenda kumsalimia rafiki yake Dully.”

Aliendelea kusema kwamba, Blue akiwa njiani kwenda nyumbani kwa Dully, Tabata Kimanmga, gari lake aina Starlet, lililoandikwa neno ‘Micharazo’ ubavuni, lilizimika ghafla.

Mara baada ya tukio hilo, mnyetishaji wetu alisema kuwa walitokea vijana wapatao tisa ambao walidai wanataka kumsaidia msanii huyo maarufu.

“Mwanzoni wakajifanya wanamsukuma ili gari liwake, lakini baadaye wakamteka na kumuweka chini ya himaya yao, kisha wakaanza kumpekua mifukoni na kwenye gari,” alisema mtoa habari wetu na kuongeza:

“Uzuri kwenye gari, Mr. Blue alikuwa na rafiki yake (jina halijafahamika), yeye aliwahi kumtumia sms Dully ambaye alifika haraka kumsaidia ‘besti’ wake.”

Hata hivyo, imeelezwa kwamba Dully Sykes baada ya kufika eneo la tukio, naye alitekwa na wahuni hao na kuanza kumpekua mifukoni.

Habari zaidi zinaeleza kuwa kabla ya kuingia kwenye mapambano ya kumsaidia rafiki yake, Dully aliwapigia simu wapambe wao na kuwafahamisha kuhusu sakata hilo.

“Dully alipotekwa, ilichukua takribani saa nzima ndipo wapambe wao walipofika kuwaokoa, ingawa haikuwa kazi rahisi kwasababu yalizuka mapambano makali,” alisema mtoa habari wetu.

Aliongeza, pamoja na kuokolewa, Mr. Blue alipata hasara kubwa, kwani gari lake lilivunjwa vunjwa na baadhi ya vifaa kuibiwa.

Vifaa hivyo ni kioo cha mbele cha gari na vile vya kuangazia pembeni (side mirrors), simu ya mkononi, nyaraka zake binafsi ambazo ni muhimu, pamoja na pesa.

Ilielezwa kuwa wahuni hao pia walimsababishia Dully hasara, baada ya kumpora kiasi cha pesa ambacho idadi yake haijafahamika.

Mwandishi wetu, aliongea na Dully ambaye alikiri kutokea utekaji huo na kusema: “Walitusumbua sana, nadhani lengo lao ilikuwa ni kuiba na hivyo walifanikiwa.”

Alipoulizwa kama waliripoti tukio hilo polisi, Dully alijibu: “Hatukwenda polisi kwasababu tuliamua kuyapuuzia mambo hayo, ila Blue yeye alikwenda hospitali kwasababu aliumia kidogo.”
Blue alipotafutwa, hakuweza kupatikana.

No comments: