Friday, February 15, 2008

Wapinzani watangaza Baraza la Mawaziri vivuli

na Rahel Chizoza, DodomaKAMBI ya Upinzani bungeni, jana ilitangaza Baraza lake la Mawaziri vivuli, lililoundwa upya baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri wa Serikali hivi karibuni.
Akitangaza baraza hilo, Kiongozi wa Upinzani bungeni, Hamad Rashid, alisema muundo wa baraza lao umezingatia uwezo wa mawaziri vivuli katika kusimamia wizara walizopangiwa.

Alisema, yapo mabadiliko katika baadhi ya wizara ambazo mawaziri vivuli wamehamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine, ambapo Wizara ya Fedha na Uchumi itakuwa chini yake, wakati Mbunge wa Karatu Dk. Wilbrod Slaa, amepelekwa TAMISEMI.

Wabunge wengine na wizara zao kwenye mabano ni Kabwe Zitto (Miundombinu), Riziki Omari Juma (Muungano), Chacha Wangwe (Mazingira), Susan Lyimo (Elimu), John Cheyo (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Mohamed Mnyaa (Nishati na Madini) na Lucy Owenya (Viwanda, Biashara na Masoko).

Alisema, nia ya kuunda baraza hilo ni kulingana na wizara mpya zilizopo ili kuisimamia serikali kuhakikisha kuwa inafanya kazi zilizokusudiwa kwa wakati muafaka na kuikosoa pale inapokwenda kinyume cha Katiba.

Alisema, upinzani unafanya tafiti mbalimbali kwa muda mwingi ili kuisaidia nchi ingawa wao hawana wasaidizi wala makatibu wakuu kama ilivyo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo kufanya kazi katika mazingira magumu.

“Tunafanya kazi usiku na mchana na wakati mwingine tunalazimika kukesha kwa ajili ya masilahi ya taifa…tupo tayari kufia mezani kwa kujituma kwa ajili ya wananchi kuliko kulala,” alisema Rashid.

Aliongeza kuwa shabaha ya wapinzani kwa sasa ni kuhakikisha wanapambana na vitendo vya rushwa kwa kuhakikisha rasilimali za Watanzania zilizopotea zinarudishwa na kufanya kazi nyingine kwa manufaa ya wananchi.

Rashid, alisema taarifa ya Kampuni ya Richmond iliyowasilishwa bungeni na kamati teule iliyosababisha kuvunjika kwa Baraza la Mawaziri, ni sawa na kupanda mbegu shambani ambapo mavuno bado.

Alisema, hakuna haja ya wananchi kufanya maandamano ya kumpongeza Rais Jakaya Kikwete, kwa kuteua baraza jipya ila ni kutafuta suluhu ya kuona namna gani fedha zinarudi kutokana na ukweli kuwa kila mwaka sh bilioni 244 zinatumiwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kulipa makampuni ya umeme bila kujali kuwa yanazalisha ama hayazalishi umeme.

Alibainisha kuwa, Tanzania si nchi ya kuomba misaada kwenye nchi nyingine kwa kiwango kilichopo sasa kama itatumia rasilimali zake kikamilifu na kusimamia fedha za walipa kodi kwa manufaa ya umma ili zisipotee kama ilivyo sasa.

Alisema, baraza la mawaziri vivuli litahakikisha wananchi wanapatiwa haki stahili katika matumizi ya mapato yao na utaratibu unaotumika kuandaa mikataba kwa kuwa sheria za mikataba zilizopo ni nzuri lakini hazitekelezwi ipasavyo.

No comments: