Friday, February 15, 2008

JK amlilia Lowassa



na Tamali Vullu na Lucy Ngowi



KWA mara ya kwanza tangu kujiuzulu kwa lazima, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Rais Jakaya Kikwete ameelezea hisia zake kuhusu tukio hilo, ambalo anakiri kwamba lilikuja wakati usiotarajiwa.
Akiwahutubia wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alimuelezea Lowassa kuwa kiongozi aliyelitumikia taifa hili kwa ujasiri na uzalendo mkubwa katika kipindi chote cha uongozi wake.

Akizungumza kwa tahadhari kubwa, huku akichagua maneno, Rais Kikwete alisema anaamini Lowassa ameacha alama ya kudumu na kueleza kuwa yaliyotokea ni ajali katika maisha ya kisiasa.

“Namshukuru sana Waziri Mkuu aliyepita, Edward Lowassa kwa moyo wa ujasiri na uzalendo, na kwa utumishi wake kwa taifa letu.

“Ametumikia nchi yetu vizuri kwa jitihada kubwa katika miaka hii miwili. Amenisaidia sana. Amelisukuma mbele gurudumu la maendeleo. Ameondoka akiwa ameacha alama ya kudumu ya kipindi chake cha uongozi,” alisema Kikwete akionyesha dhahiri kuguswa na tukio hilo la kulazimika kujiuzulu kwa Lowassa aliyeongoza harakati za kuhakikisha anakuwa rais wa nne wa Tanzania mwaka 2005.

Kabla ya kutaja jina la Lowassa, Kikwete alikiri kwamba miongoni mwa viongozi waliojiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, alikuwa na uhusiano nao wa kikazi na kimaisha kwa muda mrefu.

“Ni uamuzi mgumu, kwa sababu unawahusu watu ambao ni wenzangu wa karibu kimaisha na kikazi kwa miaka mingi. Na pia kwa sababu unaona wazi kuwa kama mambo fulani fulani yangefanyika mambo yasingefikia kuwa yalivyo,” alisema Kikwete akihuzunikia kumpoteza rafiki na mwenza wake kikazi na kimaisha wa miaka mingi.

Katika kuonyesha kuwa alilazimika kukubali kujiuzulu kwa Lowassa, kwa sababu tu ya upepo mgumu wa kisiasa ulioonekana kuwapo bungeni, Kikwete alisema kama kungepatikana fursa, basi huenda hali isingekuwa hivi leo.

“Lakini, ndiyo imeshafikia hapo. Fursa ya kufanya vinginevyo kwa maslahi ya taifa haikuwepo. Kama ilikuwepo ni finyu sana na haingeleta hatima tofauti na ile tuliyoifikia,” alisema Kikwete.

Akielezea mtiririko wa mambo uliohitimisha safari ya uwaziri mkuu wa Lowassa, Kikwete alisema baada ya Kamati Teule ya Bunge iliyokuwa inachunguza mkataba wa Richmond kuwasilisha ripoti yake bungeni, Kamati ya Uongozi ya CCM ilikutana na kisha Kamati ya wabunge wote wa CCM ikakutana jioni ya siku hiyo hiyo.

Alisema alipoletewa maoni ya vikao hivyo viwili usiku wa siku hiyo hiyo, uzito wa jambo hilo ulimfanya alazimike kumwita Dodoma Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein ambaye wakati huo alikuwa ziarani Tanga ili wajadili na kutafuta ufumbuzi.

Kikwete alisema hali ya hewa kisiasa iliwalazimisha wao wafikie uamuzi mgumu, ambao ingawa hakuutaja, ulionyesha dhahiri kuwa uliokuwa ukishauri kujiuzulu kwa Waziri Mkuu na mawaziri wote waliotajwa katika kashfa hiyo.

“Nchi yetu ilipata mtikisiko mkubwa na wananchi wengi walikuwa katika hali ya mkanganyiko, wakati mwingine walikuwa wakijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu kuhusu hatma ya taifa letu.

“Kwangu mimi ilikuwa kipindi cha mtihani mkubwa sana. Hivyo hivyo kwa Makamu wa Rais. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia rehema zake zilizotuvusha salama katika kipindi hiki kigumu. Tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu atujalie karama zake nchi yetu izidi kutulia na atuepushe na misukosuko ya namna hii tena,” alisema.

Aidha, aliwashukuru mawaziri na naibu mawaziri waliokuwa kwenye Baraza la Mawaziri lililopita, ambao hawakuteuliwa tena, kwa mchango wao kwa taifa.

Pia aliwashukuru wananchi kwa utulivu na uelewa wakati wote nchi ilipokuwa katika mazingira hayo magumu.

Aidha, alisema kabla suala hilo halijapelekwa bungeni na kuamuliwa Kamati Teule ya Bunge iundwe, Kamati ya Uongozi ya CCM Bungeni ilikutana kulijadili na kukubaliana Kamati Teule iundwe.

Katika hili, Kikwete alieleza kushangazwa kwake na madai ya viongozi wa kambi ya upinzani wanaodai kwamba, suala hili la Richmond limeifikisha serikali hapo ilipo kwa sababu ya mchango wao mkubwa.

Bila ya kutaja jina la kiongozi yeyote wa upinzani, Kikwete alimkariri mmoja wao akisema kwamba, ‘wao ndio walioiangusha serikali yake’.

“Hivi kama hili jambo lilikuwa ni la wabunge wa vyama vya upinzani na linapingwa na CCM, lingefika popote? Bunge letu hivi sasa lina wabunge 317, kati yao wabunge wa CCM ni 272 na wabunge wa upinzani ni 44. Hivi kwa tofauti hii kweli wangeweza kufanikiwa kama CCM ingelilipinga?” alihoji Rais Kikwete.

“...Watu wa ajabu wanaotafuta sifa binafsi kwa jambo la wote. Hili suala liliwahusu wabunge wote, hakuna atakayesema langu mie au letu siye. Au wa CCM walikuwa wakali zaidi kuliko wengine,” alisema.

Hata hivyo, alisema hoja hiyo iliwasilishwa bungeni kwa mara ya kwanza na William Shelukindo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Biashara na Uwekezaji, na Bunge liliafiki hoja hiyo na ndipo kamati teule ya wabunge watano chini ya uongozi wa, Harrison Mwekyembe iliundwa.

Wakati Kikwete akisema kwamba wapinzani hawana sababu ya kutamba kuhusu kufichuliwa kwa kashfa ya Richmond, kumbukumbu zinaonyesha kuwa, kabla ya Shellukindo kutoa hoja yake, mawaziri kadhaa walikuwa wameshafanya juhudi kubwa kuzuia suala hilo kujadiliwa bungeni.

Miongoni mwa mawaziri hao wa wakati huo, ni Juma Ngasongwa aliyekuwa Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji na naibu wake Gaudence Kayombo, ambao kwa nyakati tofauti walisema bayana kwamba serikali ilikuwa haina sababu ya kupeleka mkataba wa Richmond bungeni.

Kayombo aliyekuwa akijibu swali la Mbunge wa Bububu, Masolwa Cosmas Masolwa, Februari mwaka jana alisema, serikali haina mpango wa kuleta mikataba kama ule wa Richmond bungeni kwani kwa kufanya hivyo itakuwa ni kuingilia mgawanyo wa madaraka kati ya Bunge na serikali.

Kauli kama hiyo ya Kayombo iliwahi kutolewa Februari mwaka juzi pia na Dk. Ngasongwa wakati huo akiwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

Ngasongwa katika kauli yake hiyo alisema: “Hatuwezi kuleta mikataba hiyo bungeni. Ninachowashauri wabunge wawe wanawahoji mawaziri wanaohusika na sekta husika na siyo kudai mikataba iletwe hapa bungeni.”

Kutokana na kauli na msimamo huo wa serikali, mwaka jana, Spika wa Bunge alieleza kushangazwa na akasema alikuwa ana imani kuwa suala hilo litajadiliwa bungeni.

Sitta alilieleza gazeti hili katikati ya mwaka jana kwamba kulikuwa hakuna mtu anayeweza kulizuia Bunge kuhoji mikataba na akasema bayana kwamba hakuridhishwa na msimamo wa serikali kuhusu kuficha mikataba hiyo.

Alisema kuwa Bunge haliridhishwi na sababu inayotolewa na serikali kwamba kuileta mikataba hiyo bungeni ni kuingilia mgawanyo wa madaraka kati ya Bunge na serikali.

Kwa hali hiyo, Sitta alisema wakati huo tayari Kamati ya Uongozi ya Bunge, ilikuwa imeshaanza kufanya utaratibu wa kutaka kukutana na serikali, ili wajadiliane na kuliweka suala hilo sawa, kabla Bunge halijaanza kujadili mikataba mbalimbali ambayo serikali imeingia kwa niaba ya wananchi.

Hata hivyo, Sitta aliliambia gazeti hili kuwa wakati jitihada hizo zikiendelea ili kuweka utaratibu wa kudumu kuliruhusu Bunge kuijadili mikataba hiyo, mkataba wa kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond, ambao umepigiwa kelele sana, utajadiliwa na Bunge wakati wa kikao kijacho.

Alisema Richmond ni moja ya masuala yaliyomo katika ripoti iliyowasilishwa kwake na Kamati ya Kudumu ya Uwezeshaji na Biashara ambayo ilikuwa ikitakiwa kujadiliwa.

Sitta alisema ripoti hiyo haikuweza kujadiliwa katika mkutano wa saba uliomalizika Aprili mwaka jana kutokana na ufinyu wa muda.

Mbali ya hilo, Julai 4, mwaka jana, Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa aliibua upya sakata la zabuni ya kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond Development Company (RDC) bungeni.

Dk. Slaa alieleza kushangazwa na msimamo wa Mei mwaka jana uliotolewa na iliyokuwa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU, sasa Takukuru) ya kusema kwamba mjadala wa Richmond ulikuwa umefungwa.

Dk. Slaa aliliibua suala hilo wakati huo Bunge likiwa limekaa kama Kamati ya Matumizi, kupitia kifungu kwa kifungu, Bajeti ya Ofisi ya Rais.

“PCB walifunga ule mjadala kwa kusema kwamba wamemaliza. Lakini, wakati wanafunga wakaeleza kwamba kuna mapungufu machache yameonekana katika taratibu zilizotumika. Sasa, kwa mtu anayesimamia shughuli za serikali kama mbunge, anapenda kujua haya mapungufu ni yapi!

“Waziri wakati wa kujibu anasema hili ni suala la kijinai jinai, kwa hiyo taarifa ile haiwezi kuwasilishwa bungeni. Lakini, mimi sina tatizo na hiyo sehemu ya kijinai, nadhani hata wakati tunatunga sheria ya PCB hilo pia tulilisema.

“Lakini, inapofika mahali kwamba kuna mapungufu ambayo wanasema kwenye lile tangazo walilotoa kwenye gazeti kwamba siyo tu upungufu, kuna uzembe pia ulitokea. Sasa, nadhani taarifa zile zinaacha kuwa za kijinai, kuna ‘element’ ya kiutendaji ambayo inaenda kwenye uzembe,” alisema Dk. Slaa wakati huo.

Mbunge huyo alihitimisha kwa kumtaka aliyekuwa Waziri wa Nchi (Utawala Bora), Philip Marmo kulieleza Bunge namna ambavyo wabunge wanaweza wakaijadili ripoti hiyo baada ya kuletwa bungeni.

Hakuishia hapo, kwani alikwenda mbali zaidi na kuuliza iwapo kweli taarifa hiyo ya Takuru ilikuwa ni ya siri, basi ni kwa nini iliichapisha kwenye magazeti badala ya kuwaamini wabunge.

Mbali ya hayo, katika mkutano wa jana na wazee wa CCM Dar es Salaam, rais alisema kabla ya tukio la wiki iliyopita, tayari alikuwa ameshafanya mipango ya kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri baada ya kikao cha Bunge kinachoendea kumalizika.

Aidha, alisema mpango huo ambao uliwashirikisha yeye, Makamu wa Rais na Lowassa, ulitaka mabadiliko hayo yafanyike baada ya kuondoka nchini kwa Rais wa Marekani George Bush anayewasili hapa nchini kwa ziara ya siku nne inayoanza kesho.

“Nilikuwa na mawazo ya kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, lakini siyo wakati huu na kwa namna hii. Kwa fikra yangu tungefanya baada ya Bunge na baada ya mgeni wetu (Bush) kuondoka. Yangekuwa mabadiliko ya kawaida,” alisema.

Rais Kikwete alisema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, walianza kufanya zoezi la tathmini ya hali ya utendaji ya kila kiongozi, ili wajue wajirekebishe wapi na vipi.

“Sikutarajia kufanya mabadiliko makubwa kiasi hiki. Lakini ya Mwenyezi Mungu huyajui. Mwanadamu unakuwa na yako na Mwenyezi Mungu anakuwa na yake usiyoyajua wala kuyategemea. Lakini kila linalotokea lina heri yake,” alisema.

Aidha, alisema ripoti ya Kamati ya Mwakyembe ina mapendekezo mengi na kwamba wanasubiri kwa hamu mapendekezo ya Bunge, ili yale yanayohusu serikali wayafanyie kazi mapema.

No comments: