Saturday, February 16, 2008

Majibu ya ukimwi yamliza Aisha


Chanzo chetu cha habari kilisema Aisha Madinda, alilazimishwa aende kupima Ukimwi baada ya ndugu zake kutojua kinachomsumbua.

Aisha alisema kuwa baada ya kupima na kusubiri majibu kwa muda mrefu, anashukuru ameyapata ingawa yamemuumiza kwa kiasi kikubwa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwake jana (Alhamisi), Aisha alisema aliamua kwenda kufanyiwa uchunguzi wa kina katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, ikiwa pamoja na kupima virusi vya Ukimwi baada ya ndugu zake kumtaka afanye hivyo.

“Wakati naenda kupima nilikuwa roho juu, kwani ndugu zangu ndiyo walionishupalia nipime Ukimwi na unajua kupima ugonjwa huo inahitaji ujipe moyo mgumu.

“Wakati nasubiri majibu kidogo nife kwa kihoro, kwani roho ilikuwa inanienda mbio lakini nilipopewa majibu kwamba sina, niliona dunia yote kama inaanguka, nikalia kwa furaha.

“Maana kutokana na watu walivyokuwa wanazungumza mengi kuhusu mimi, nilijiona labda tayari nimeshaukwaa, lakini nashukuru Mungu sina kimwi, sasa nitajilinda zaidi,” alisema Aisha huku akionyesha vyeti vyake.

Juu ya vipimo vingine alivyofanyiwa katika mwili wake alisema, madaktari bingwa wa Muhimbili wameamua aendelee na matibabu mengine, lakini wao wameshindwa kwani hawaoni chochote anachoumwa.

Kutokana na hilo alisema kwa sasa ameamua kuikimbia nyumba anayoishi na kwenda kupanga nyumba nyingine eneo la Mikocheni. Kwa sasa Aisha anaisha Sinza Lion.

Alipoulizwa iwapo anakimbia nyumba ya sasa labda kuna mambo ya ushirikina, Aisha alikataa kwa madai amechoka kuishi hapo na kutupiwa kila aina ya jicho.

Kwa muda mrefu sasa, mnenguaji huyo anaugulia maumivu huku akidai hajui anaumwa nini, ingawa kuna madai mengine kuwa kukatazwa kwake kutumia dawa za kulevya ndiko kunakomponza.

Kuhusu kutumia dawa za kulevya, Aisha amekana kuhusika nazo, huku akidai anazushiwa kutokana na umaarufu wake amekuwa akizushiwa mambo mengi hali inayosababisha akosane na ndugu zake, ambao wanamuona hafai katika jamii yao.
“Unajua watu wanapenda kuongea vitu ambavyo hawajui, kama natumia vitu kama hivyo si ingejulikana mapema? Mimi mwenyewe sijui naumwa nini, lakini utashangaa watu wanakuzushia ugonjwa unaoumwa.”

Kutokana na hali ya mnenguaji huyo ni vema Watanzania wakamuombea kwa Mungu ili arejewe na afya njema na kuendelea na kazi yake.

No comments: