Thursday, February 14, 2008

JK afichua siri

na Waandishi Wetu Dar es Salaam na DodomaBARAZA jipya la mawaziri lililotangazwa na Rais Jakaya Kikwete juzi limeanza kufichukua masuala kadhaa yaliyojificha nyuma ya uteuzi huo uliopokewa kwa hisia tofauti na wananchi wa kada mbalimbali.
Uteuzi huo ambao umepunguza idadi ya mawaziri na manaibu wao kutoka 60 ya awali hadi 47, kwa mara ya kwanza umeonyesha dhamira ya wazi na ya kweli ya rais na wasaidizi wake wawili wakuu, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, ya kuunda Baraza la Mawaziri kwa kuzingatia uwiano wa kimikoa, rekodi binafsi za utendaji kazi za wateule na mahitaji ya sasa ya serikali.

Mbali ya hilo, uteuzi huo kwa mara ya kwanza umethibitisha kwamba, Rais Kikwete sasa amedhamiria kwa dhati kuweka kando kundi maarufu la mtandao lililokuwa mstari wa mbele ‘kumbeba’ wakati wa kampeni za kuwania uteuzi wa kuwa mgombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na baadaye urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Baadhi ya wadadisi wa mambo waliozungumza na Tanzania Daima juzi na jana wanaeleza kwamba, uamuzi wa rais kulivunja nguvu kundi la mtandao, umekuwa rahisi kutimizwa, hasa baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, wiki iliyopita.

Uamuzi wa Rais Kikwete kuwaingiza wanasiasa wa aina ya Hamisi Kagasheki katika baraza la mawaziri na kuendelea kubakia kwa watu kama Mark Mwandosya na John Magufuli, huku wakiendelea kupewa wizara kamili ni kiashirio kingine cha dhamira yake ya kuua na kuuzika mtandao wa mwaka 2005.

Katika hatua nyingine, Baraza la Mawaziri linaloendelea kuuacha Mkoa wa Kigoma ukibakiwa na naibu waziri mmoja pekee tofauti na ilivyo katika mikoa mingi, ni ushahidi wa namna Kikwete anavyoendelea kukwama kupata mtu anayemwamini kushika nafasi ya uwaziri kamili serikalini.

Hatua hii ya rais kuendelea kukosa waziri kamili kutoka Kigoma, kwa namna nyingine kunaweza kwa sasa kutoa picha ya kwa nini jina la Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ambaye ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), limekuwa likitajwa kuwa miongoni mwa mawaziri ambao wangeteuliwa katika Baraza la Mawaziri la juzi.

Habari za uhakika kutoka ndani ya serikali na CHADEMA zinaeleza kwamba, siku chache kabla ya kutangazwa kwa mawaziri hao wapya, Ofisi ya Rais Ikulu, iliwasiliana moja kwa moja au kupitia kwa kiongozi mmoja wa juu wa upinzani na mwanasiasa huyo kijana na mdogo kuliko wote wa kuchaguliwa na kumuuliza iwapo alikuwa tayari kuukubali uteuzi huo.

Ingawa viongozi kadhaa wa kambi ya upinzani bungeni akiwamo Hamad Rashid Mohammed (CUF), walikanusha katakata kuwapo kwa mawasiliano ya namna hiyo, Tanzania Daima sasa inaweza kuthibitisha kwa uhakika kwamba Zitto alikuwa miongoni mwa wabunge wa upinzani ambao waliombwa kukubali kuteuliwa kuingia katika baraza hilo la mawaziri.

Hata hivyo muundo wa sasa wa Baraza la Mawaziri linalouacha Mkoa wa Kigoma ukiwa na naibu waziri mmoja tu, ni ushahidi unaoweza kutafsiriwa kwamba, Zitto alikuwa akilengwa kuteuliwa, si kwa sababu ya kutoka kambi ya upinzani, bali kwa lengo la kuujengea uhalali wa kuwa na waziri mwenye nguvu na uwezo anayetokea eneo hilo.

Kwa maelezo mengine, iwapo hivyo ndivyo ilivyo basi, wabunge wa kuchaguliwa wanaotokea majimbo mbalimbali ya Mkoa wa Kigoma kwa kiwango kikubwa kwa jicho la Rais Kikwete, wanaonekana kutokuwa na sifa zinazoweza kuwapa moja kwa moja nafasi za uwaziri.

Ukweli kuhusu suala hili unaweza ukathibitishwa na uamuzi wa Rais Kikwete kumweka kando, Daniel Nsanzugwanko, aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni katika baraza la mawaziri lililovunjwa wiki iliyopita.

Nje ya uwiano huo wa kimikoa, uamuzi wa rais kuunda baraza dogo akiwaacha waliokuwa mawaziri katika serikali iliyopita kama Basil Mramba na Zakia Meghji, kunaonekana dhahiri kuwa ni matokeo ya uchunguzi wa kashfa kuu mbili za Richmond na EPA.

Majina ya Mramba na Meghji kila mmoja kwa namna yake yamekuwa yakitajwa sana kuhusika kwa namna moja katika kashfa hizo mbili kila mmoja akihusishwa kwa njia yake.

Mramba aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, ndiye mtu anayetajwa kuwa alikuwapo wakati shilingi bilioni 133 zikifujwa kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), ambayo bado haijafikishwa rasmi bungeni baada ya Kampuni ya ukaguzi wa mahesabu ya kimataifa ya Ernst & Young kugundua wizi huo hivi karibuni.

Meghji yeye katika suala hili la EPA anatajwa kuwa waziri aliyeyumba wakati ugunduzi wa awali kuhusu wizi wa fedha hizo ulipojulikana mapema mwaka 2006.

Mwanasiasa huyo ambaye ni mwanamke wa kwanza kushika uwaziri wa fedha, jana aliieleza Tanzania Daima kwamba, kuachwa kwake ni tukio la kawaida la kisiasa na akasema bado anaendelea kumshukuru rais kwa kumpa fursa ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Waziri wa Fedha.

“Rais hajakosea, ni utaratibu wa uongozi. Mimi binafsi namshukuru kwa heshima aliyonipa ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Fedha,” alisema Meghji ambaye jana alikuwapo wakati mawaziri wengine wakiapishwa.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, ambaye kurudishwa kwake kumepingwa na watu mbalimbali, amewataka wanaompinga wakamuulize rais kile kilichosababisha ateuliwe.

Chenge, mwanasheria mkuu wa zamani na mmoja wa wanasiasa wanaojiamini, aliyasema hayo jana katika viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino, nje kidogo ya mji wa Dodoma, muda mfupi baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo.

“Mimi nafahamika kama mtu nisiyependa maneno ya pembeni,” alisema Chenge na kuongeza kuwa wanaosema kuhusu yeye wana haki ya kusema, kwa kuwa kila mtu anayo haki ya kutoa maoni yake na yeye hana haki ya kumkataza au kumzuia mtu kutoa maoni yake.

Alisema anamshukuru Rais Kikwete kwa kumwamini na kumteua tena katika nafasi hiyo na sasa ataelekeza nguvu zake katika kutekeleza majukumu yake.

Alisema ana changamoto nyingi katika wizara hiyo na amedhamiria kufanya kazi kwa bidii kwa sababu mtu anapimwa kwa yale anayoyafanya.

Muda mfupi baada ya Chenge kutoa maneno hayo, Rais Kikwete mwenyewe alipofuatwa na waandishi jana, alikataa kusema lolote kuhusu uteuzi akisema: “Nimeshasema mengi sana, kwa sasa hivi nisingependa kusema kitu kingine.”
Kwa upande wake Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima (CCM), ambaye ameteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Naibu Waziri wa Nishari na Madini, alisema hakuamini aliposikia Rais Jakaya Kikwete akitamka jina lake wakati anatangaza Baraza la Mawaziri juzi.

Malima ambaye uteuzi wake unaonekana kuwa ni kuziba pengo la Mkoa wa Pwani kupungukiwa waziri kutokana na Dk. Ibrahim Msabaha kujiuzulu baada ya kuhusishwa na kashfa ya Richmond, alisema uteuzi wake unamaanisha kuwa rais amekiona kitu fulani kwake na akaahidi kujitahidi kufanya kazi kwa mtindo ambao utamridhisha rais na Watanzania wengine.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ambaye kabla ya mabadiliko hayo alikuwa naibu waziri katika wizara hiyo hiyo, alisema anazifahamu changamoto zilizopo katika wizara hiyo, hasa sekta ndogo za madini na nishati.

Alisema hawataianza upya kazi ya kufanya marekebisho katika maeneo yenye matatizo kwa sababu kazi hiyo ilishaanza tangu awali.

Akitoa mfano, alisema ripoti zitakazotolewa na kamati ya kupitia mikataba ya madini iliyoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, na ile ya wizara zitasaidia kuboresha sera ya madini.

Aidha, Ngeleja alisema kutokana na mambo yaliyotokea katika siku za hivi karibuni, hivi sasa watajitahidi kuwa makini katika suala la mikataba, hasa ile ya madini.

“Tunafahamu kuwa watu wanaponda baadhi ya mikataba, kama huu wa Richmond ambayo sasa inatakiwa kuvunjwa. Hii ni changamoto kwetu na kazi kubwa iliyo mbele yetu ni kulishughulikia hilo,” alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Stephen Wassira, alisema changamoto kubwa iliyopo hivi sasa ni kuhakikisha kuwa rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya kuleta maendeleo zinatumika ipasavyo.

Alisema kuna kazi kubwa ya kuzisimamia halmashauri za wilaya, kwani kulingana na mfumo mpya unapeleka fedha nyingi katika ngazi ya halmashauri za wilaya, ambazo ndizo zinatekeleza mipango ya maendeleo.

“Iwapo tutazisimamia vizuri halmashauri zikifanya vizuri tutakuwa tunapata mafanikio, lakini iwapo zitafanya vibaya tutaharibikiwa,” alisema.

Alisema msisitizo utawekwa katika kuhakikisha kuwa huduma zinazopatikana zinalingana na thamani ya fedha zinazotolewa, ili kuleta tija iliyopangwa.

Waziri mpya wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, alikiri kuwa anakabiliwa na kazi kubwa katika wizara hiyo baada ya kuunganishwa na iliyokuwa Wizara ya Usalama wa Raia.

“Lakini nitajitahidi kufanya kazi ili nisimwangushe Rais na Watanzania ambao hali halisi inaonyesha kuwa, wanahitaji mabadiliko makubwa katika maisha yao,” alisema.

Alisema changamoto zinazohitaji majibu ya haraka zipo nyingi na akazitaja baadhi kuwa ni msongamano wa wafungwa katika magereza na mahabusu na kuunda upya Idara ya Zimamoto.

Alisema kuwa kwa upande wa masuala ambayo yalikuwa chini ya Usalama wa Raia, atachukua muda kujifunza na kujizoesha ili ahakikishe kuwa anaitekeleza kazi yake kikamilifu.

Kwa upande wake, Phillip Marmo, ambaye aliapishwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Uratibu na Bunge, alisema hali ya sasa nchini inatoa matumaini katika vita dhidi ya rushwa.

Alisema matumaini hayo yanatokana na ukweli kuwa watu wengi sasa wameonyesha kuwa wapo tayari kutoa mchango wao, hata wa mawazo, katika vita hiyo.

“Mimi ninaamini kuwa kupambana na rushwa ni mchakato ambao utachukua muda mrefu, jambo muhimu ni kuendelea kupambana mpaka pale wananchi watakaporidhika kuwa wanaishi maisha mazuri,” alisema.

No comments: