Thursday, February 14, 2008

Richmond yaigawa CCM


na Mwandishi Wetu



UPEPO mbaya wa kisiasa unavuma ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa tisa wa Tanzania, Edward Lowassa.
Habari za uhakika kutoka ndani ya chama hicho zilizoifikia Tanzania Daima zimeeleza kuwa, kishindo cha kujiuzulu kwa Lowassa kimewagawa vigogo na makada maarufu wa CCM, jambo linalotishia uhai na uimara wake.

Habari hizo zimeeleza baada ya Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mchakato wa zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura, ulioipa ushindi Kampuni ya Richmond Development ya Marekani, Dk. Harrison Mwakyembe, kusoma ripoti ya kamati hiyo bungeni wiki iliyopita na kumtaja aliyekuwa Waziri Mkuu Lowassa kuwa mhusika mkuu wa kashfa hiyo, makada wa chama hicho waligawanyika makundi mawili, kundi moja likiiunga mkono ripoti hiyo na jingine likiipinga.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya CCM vimelidokeza gazeti hili kuwa, baadhi ya wabunge, makada wa chama hicho tawala na waliokuwa mawaziri katika baraza lililovunjwa wiki iliyopita hawakubaliani na ripoti ya Dk. Mwakyembe kwa madai kuwa ilipikwa kwa ajili ya kumuangamiza Lowassa.

Kundi hilo linadai kwamba ripoti hiyo ilitengenezwa makusudi kwa ajili ya kummaliza Lowassa kisiasa na watu walioandaliwa na kundi la mahasimu wake kisiasa.

Taarifa nyingine zilizolifikia gazeti hili kutoka kwa watu walio karibu na Lowassa kikazi zilieleza kuwa, ripoti ya Dk. Mwakyembe iliyomtaja Lowassa kuwa mhusika mkuu katika sakata la Richmond, ni kisasi cha kisiasa dhidi ya kundi la wanamtandao ambalo katika siku za karibuni limekuwa likiangaliwa kwa jicho baya na baadhi ya wana CCM wasiokuwa wanamtandao.

Zinaeleza zaidi kwamba, baada ya kundi la wanamtandao kubaini vita inayopiganwa dhidi yao, pamoja na kushitushwa na hatua zinazochukuliwa sasa na Rais Jakaya Kikwete za kuisafisha serikali yake, kundi hilo liliamua kukaa kimya likisubiri kutangazwa kwa baraza jipya la mawaziri kabla halijachukua msimamo wa jinsi ya kutetea nafasi ya kuwepo kwake ndani ya chama hicho.

Habari zaidi zinaeleza kwamba, kukosekana kwa Dk. Mwakyembe au mjumbe mwingine yeyote wa kamati yake katika baraza jipya la mawaziri kumechukuliwa kuwa ni ushindi wa kundi linalomtetea Lowassa na rafiki yake wa karibu Rostam Aziz, wanasiasa wanaotajwa kuwa maadui wakubwa wa kisiasa wa wana CCM wasio wana mtandao.

Watu hao wanaojumuisha mawaziri waliorejeshwa katika serikali mpya wanasema, uteuzi huo wa rais wa kuwaweka kando kina Mwakyembe na wabunge wote wa CCM waliomshambulia Lowassa na wenzake waliotajwa ndani ya Richmond unaonyesha kwamba, hakufurahishwa na namna kamati hiyo ilivyofanya kazi yake.

Kauli iliyotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, muda mfupi tu baada ya Bunge kuthibitisha uteuzi wake wa asilimia 98.9 mwishoni mwa wiki iliyopita kuhusu ripoti hiyo ni ushahidi wa kutosha kwamba taarifa za mgawanyiko huo zimefika ngazi za juu.

Pinda katika kauli yake hiyo aliwataka wabunge kuachana na imani za kuiona ripoti ya kamati teule ya Bunge iliyoongozwa na Mwakyembe kuwa iliyo fanya kazi kwa lengo baya la kumuumiza mtu fulani.

Baadhi ya wajumbe wa kundi hilo la wanamtandao wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM na wale wa Sekretarieti ya chama hicho ambao mwishoni mwa wiki iliyopita waliongoza mapokezi ya kimya kimya ya kumpokea Lowassa alipofika Dar es Saalam akitokea Dodoma, wamekaririwa wakieleza kuwa, tayari walikuwa wameshajipanga kujibu mapigo.

Wakati hali ikiwa hivyo, kundi jingine linalodaiwa kuwa limeundwa mahususi kwa ajili ya kuwashughulikia wanamtandao huo wa Lowassa na Rostam likiongozwa na mmoja wa viongozi wa juu katika moja ya taasisi tatu zinazoongoza dola (ambaye ni mwanamtandao aliyeasi), linaamini kuwa ushahidi uliotumika kumtia hatiani Lowassa ni sehemu ndogo tu ya kashfa zinazomuandama kiongozi huyo.

Baadhi ya watu wazito kutoka ndani ya kundi hilo waliozungumza na gazeti hili hivi karibuni kwa nyakati tofauti, walieleza kuwa ushahidi iliomtia matatani Lowassa ni sehemu ndogo tu ya ushahidi kamili ambao kamati hiyo inao.

Mmoja wa viongozi wa kundi hilo alieleza kuwa kama ripoti hiyo ingetoa ushahidi wote uliokuwa ukimgusa Lowassa katika sakata hilo, serikali ingepata mtikisiko mkubwa ambao ungeweza kuiyumbisha.

Habari zaidi zinaeleza kuwa, Kamati ya Dk. Mwakyembe ilipokea ushahidi mwingi uliokuwa ukimuhusisha Lowassa na kashfa hiyo lakini ilifanya kila linalowezekana ili kulinda hadhi ya waziri mkuu.

Zinaeleza zaidi kwamba, ingawa wajumbe wa kamati hiyo waliapa kutomwangalia mtu bali masilahi ya taifa, walifanya kila njia kuhahakisha hadhi ya waziri mkuu inalindwa kwa kutotoa ukweli wote dhidi yake.

Baadhi ya watu hao wanasema iwapo watathibitisha pasipo shaka kwamba, wanashambuliwa, basi upo uwezekano wa wao kuhakikisha kila kitu kuhusu Richmond na namna kinavyomgusa Lowassa na Rostam watakianika ndani ya Bunge baada ya mjadala kuhusu suala hilo unaoanza leo.

No comments: