Thursday, February 14, 2008

Mrema amtaka JK kueleza anayofahamu
KASHFA YA RICHMOND

na Prisca Nsemwa na Mobin Sarya

MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, amemshauri Rais Jakaya Kikwete, kuuelezea umma kwa kauli yake namna anavyoifahamu na kuitambua Kampuni ya Richmond.
Mrema alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa chama hicho uliopo Magomeni, Dar es Salaam.

“Kikwete aseme pia kama anaifahamu vipi Richmond na kuitambua, sisi tunataka kusikia kauli yake, hata huo uteuzi wake wa baraza la mawaziri hakuna kikubwa alichofanya, kwakuwa amewarudisha mafisadi wengine kwenye baraza hilo,” alisema Mrema.

Sambamba na hilo, Mrema aliongeza kuwa ni unafiki kumpongeza Rais Kikwete kwa kuvunja Baraza la Mawaziri wakati lilivunjika lenyewe baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, kujiuzulu.

Alisema wapinzani ndio waliojitoa kufichua ufisadi unaofanywa na mawaziri na kuamua kuuweka hadharani katika viwanja vya Mwembe Yanga kwa kutaja majina ya viongozi waliotuhumiwa kwa ufisadi.

Kwa mujibu wa Mrema wanaostahili kupongezwa si Rais Kikwete bali wapinzani kutokana na kuibua tuhuma nzito zilizosababisha kujiengua kwa Lowassa, hivyo kumlazimu rais kuvunja Baraza la Mawaziri.

“Rais hawezi kupongezwa kwa hili, kubwa ni kwamba yeye ndiye aliyekuwa akililinda kundi la mafisadi, kwa kuwa wakati wapinzani wanawataja mafisadi, Rais alisema kuwa wapinzani wanajifanya wao ni mapolisi na hivyo kelele zao hazitamnyima usingizi, leo ndiyo haya yametokea,” alisema Mrema.

Alisema lazima rais atambue kuwa kitendo cha kuvunjika kwa baraza hilo kutokana na tuhuma zilizowagusa baadhi ya viongozi ni fedheha kwake na nchi kwa ujumla.

Hata hivyo alisema kuwa rais lazima auambie umma wa Watanzania habari za EPA japokuwa mtuhumiwa wa ufisadi huo ambaye Mrema alimtaja kuwa ni Zakia Meghji, ametolewa na kuwa pamoja na hilo, bado wananchi wanataka kufahamu mchanganuo huo.

Akizungumzia suala la ujio wa Rais wa Marekani, George Bush, alisema TLP watafanya maandamano kwa kumtaka Rais huyo kuja na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT) Daudi Ballali.

Alisema kuwa atakapokuja yeye ndiye atakayebeba bango ambalo atakwenda nalo uwanja wa ndege katika mapokezi ya Bush litakalomtaka rais huyo wa dunia kumleta Ballali hapa nchini na si vinginevyo.

“Kama mtaogopa kubeba bango hilo mimi mwenyewe nitalibeba tena mbele na kumwambia kuwa tunamtaka Ballali hapa kama sivyo basi ziara yake itakuwa ni ya kibiashara,” alisema Mrema.

Wakati huo huo, Rais Kikwete leo anatarajiwa kuzungumza na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, kuzungumzia hali ilivyo ndani ya serikali yake baada ya kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

Hayo yalielezwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Barongo, alipozungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa Rais Kikwete atazungumza na wazee hao katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.

“Kesho (leo) Rais Kikwete saa tisa alasiri atakutana na wazee wote wa mkoa, ili apate nafasi ya kuwaambia wananchi kupitia kwa wazee hao, mabadiliko yaliyofanyika katika serikali yake,” alisema Barongo.

No comments: