Thursday, February 14, 2008

az Chang’ombe Kitovu cha elimu ya Kiislamu Tanzania

George Maziku


UISLAMU kama dini nyingine, umejaa mafundisho yanayohimiza uadilifu wa kiroho, kwa maana ya kukataza mawazo na matendo maovu na kuamrisha mema.
Kwa mujibu wa Uislamu, watu wote wanaoishi kwa kutenda mema wakati wote wa maisha yao hapa duniani, Mungu wao (Allah) kawawekea malipo manono huko peponi ili waishi na kufaidi huko milele.

Kwa watenda maovu, Uislamu unasema Allah amewaandalia moto mkali usiokuwa na mfano wake hapa duniani, na kwamba wataishi katika moto huo milele huku wakipata mateso makali yasiyo na mwisho.

Ni ukweli usiopingika kuwa mafundisho haya ya Uislamu yamechangia kwa sehemu kubwa kuifanya dunia yetu kuwa mahali salama kuishi.

Mbali na kukazia sana mafundisho ya kiroho, Uislamu haujasahau kuweka mwongozo wa maisha ya mwanadamu hapa duniani, kwa maana ya huduma za kijamii zinazohusu ustawi wa watu.

Uislamu umehimiza waumini wake kutopuuza elimu ya mambo ya kidunia, mfumo wa uchumi, mfumo wa kulinda haki ya kila mtu, mfumo wa kusaidia watu na makundi mbalimbali yasiyojiweza.

Kwa upande wa elimu, Waislamu mmoja mmoja au taasisi za Waislamu au serikali za Kiislamu zimekuwa zikijihusisha kutoa huduma ya elimu ya dini na ya kidunia kwa Waislamu kwa njia ya kujenga mashule na kuyaendesha au kugharamia masomo ya watu hao nje ya nchi.

Misri ikiwa miongoni mwa nchi zenye waislamu wengi, imekuwa ikitoa misaada mbalimbali ya kidini na kijamii kwa Waislamu katika nchi nyingi mbalimbali.

Tanzania ni moja ya mataifa yanayonufaika na misaada ya Misri inayotolewa na nchi hiyo kwa Waislamu wa hapa nchini.

Shule ya Kiislamu ya Markaz iliyopo eneo la Chang’ombe, jijini Dar es Salaam, ni moja ya misaada ya elimu inayotolewa na nchi hiyo kwa Waislamu wa Tanzania.

Shule ya Markaz ya Chang’ombe ilijengwa na Serikali ya Misri mwaka 1969, chini ya usimamizi wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), ambacho ni chombo kikuu cha kuangalia na kusimamia masilahi ya Waislamu nchini.

Akizungumza na mwandishi wa makala hii, Mkurugenzi Mtendaji wa shule ya Kiislamu – Markaz, Dk. Muhammad Rashid, anasema kuwa shule hiyo huendeshwa kwa ushirikiano kati ya wataalamu kutoka Misri na uongozi wa BAKWATA.

Dk. Rashid anasema kuwa serikali ya Misri ikiwa ndiye mfadhili pekee wa fedha za kuendeshea shule hiyo, huteua mkurugenzi mtendaji wa shule ya Markaz ili kusimamia uendeshaji wa shughuli za kila siku za shule hiyo, huku BAKWATA wakitoa miongozo ya mitaala ya elimu ya kidini na kisekula inayotolewa na shule hiyo.

Pia serikali ya Misri huleta nchini walimu wa dini ya Kiislamu na lugha ya Kiarabu, ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaopitia shule hiyo wanapata elimu bora ya dini ya Kiislamu, kwa kufundishwa na walimu waliobobea katika nyanja hiyo.

“Serikali ya Misri inatoa fedha zote za kuendesha shule hii na kuleta mkurugenzi mtendaji na walimu wa dini na lugha ya Kiislamu, lakini tupo chini ya BAKWATA ambayo inatoa miongozo ya mitaala ya elimu zote tunazofundisha hapa”, anasema Dk. Rashid.

Shule ya Markaz hufundisha elimu ya dini ya Kiislamu na lugha ya Kiarabu; na hutoa huduma ya elimu za msingi, kati (pre-secondary) na elimu ya sekondari, na kwamba elimu zote hutolewa bila malipo yoyote.

“Wanafunzi wetu hawalipii masomo yao, gharama zote hulipwa na Serikali ya Misri na hii ni kwa sababu nchi yetu inatambua uchumi duni wa wananchi wengi wa Tanzania,” anafafanua Dk. Rashid.

Anasema kuwa sifa kuu ya kujiunga na shule hiyo ni kuwa muumini wa dini ya Kiislamu na tabia njema kulingana na maagizo ya dini hiyo.

Kuhusu nafasi ya waumini wa dini nyingine au kwa watu wasio na dini wanaovutiwa kujifunza dini ya Kiislamu au lugha ya Kiarabu, Dk. Rashid anasema wanaruhusu lakini nje ya muda wa kawaida wa masomo (evening classes), na kwamba hawatozi malipo yoyote kama ilivyo kwa wanafunzi wengine.

“Tunapokea wanafunzi wasio Waislamu wanaotaka kujifunza dini ya Kiislamu au lugha ya Kiarabu kwa muda wa jioni na hatutozi malipo yoyote, hata ninyi waandishi wa habari tunawakaribisha mjifunze Kiarabu na Uislamu ili mfanye kazi zenu vizuri zaidi,” anaeleza na kushauri Dk. Rashid.

Dk. Rashid anasema kuwa baada ya kuhitimu elimu ya sekondari, wanafunzi 16 bora hupelekwa nchini Misri kuendelea na masomo ya juu katika vyuo vya nchi hiyo, na wengine hujiunga na shule na vyuo vya hapa nchini kwa masomo ya juu.

Anasema Watanzania wengi mmoja mmoja na jamii kwa ujumla wamenufaika na huduma za elimu za shule hiyo, kwani wengi wameajiriwa katika taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi yetu.

Ukiacha huduma ya elimu, pia Shule ya Markaz imefufua huduma ya zahanati ambayo ilisitishwa tangu mwaka 1985, ili kutoa huduma ya matibabu kwa wanafunzi wa shule hiyo na wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka shule hiyo.

“Huduma ya zahanati ilikuwepo miaka ya nyuma, lakini ilisitishwa baada ya kushindwa kukidhi viwango vilivyowekwa na serikali. Sasa tumeifufua na safari hii tumejiandaa vya kutosha kifedha na kitaalamu,” anasema Dk. Rashid.

Dk. Rashid anasema kuwa Serikali ya Misri italeta madaktari wanne, ambao watasaidiana na madaktari na wauguzi wazalendo watakaoajiriwa na kulipwa vizuri ili kuleta ufanisi.

Zahanati hiyo itakuwa chini ya Shule ya Markaz na Ubalozi wa Serikali ya Misri nchini, na itaendeshwa kwa kufuata sera ya Taifa ya Afya.

Dk. Rashid amewashauri Watanzania hususan wasio Waislamu kuuangalia Uislamu kwa jicho chanya, kuwa dini inayohimiza na kusimamia misingi ya uadilifu wa kiroho na ustawi wa kimwili kwa wanadamu wote.

Anaongeza kuwa Uislamu hauhusiani hata kidogo na vitendo vya ghasia na uhalifu dhidi ya mali na maisha ya binadamu.

“Uislamu si dini ya wahalifu na haihusiani hata kidogo na mafundisho ya kihalifu. Uislamu ni uadilifu, unahimiza na kusimamia matendo mema na ustawi wa maisha ya kimwili ya kila binadamu,” amesisitiza Dk. Rashid.

No comments: