Wednesday, February 13, 2008

Wanasiasa walonga

BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI



na Tamali Vullu



WANASIASA kadhaa nchini, wametoa maoni mbalimbali kuhusu baraza jipya la mawaziri ambalo limetangazwa jana na Rais Jakaya Kiwete.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa, alisema kuna baadhi ya maeneo anakubaliana na Rais Kikwete katika uteuzi wake na mengine wanatofautiana.

Alisema anampongeza Rais Kikwete kwa kufanya wizara inayoshughulikia elimu kuwa moja, na kusema kuwa iwapo itasimamiwa vizuri kutakuwepo na mabadiliko makubwa ya elimu nchini.

Hata hivyo, alihoji kutenganishwa kwa masuala ya teknolojia na elimu ya juu na kusema kuwa masuala hayo yanakwenda sambamba hivyo hayakupaswa kutenganishwa.

“Mara nyingi tunafanya maamuzi ya zima moto, sidhani katika hilo kama kuna utafiti uliofanyika,” alisema.

Pia alisema bado baraza hilo ni kubwa hasa ukizingatiwa hali ya nchi yetu ni maskini.

Alisema inashangaza kwa nchi maskini kama Tanzania kuwa na Baraza kubwa la Mawaziri, wakati nchi tajiri kama Uingereza, ambayo inaongoza kwa kusaidia bajeti ya Tanzania, ina baraza dogo la mawaziri.

Alisema kwa mujibu wa taratibu za Uingereza, waziri mkuu anaruhusiwa kuchagua mawaziri wasiozidi 20 na anakuwa na ruhusa ya kuchagua mmoja wa ziada iwapo atatoa hoja inayoonyesha kuwa anamuhitaji mtu wa ziada katika baraza lake.

“Baada ya hao 21, akiongeza mtu mwingine, waziri mkuu anawajibika kulipia gharama zake zote yeye mwenyewe binafsi kutoka katika fedha zake na si za ofisi yake au serikali,” alisema.

Alisema kila waziri nchini anapewa gari la milioni 60, fedha ambazo zingeweza kujengwa zahanati moja na dawa za kuanzia.

“Tunapoteza fedha nyingi kutokana na ukubwa wa baraza. Tunakurupuka katika maamuzi , tutataka kuwa na wizara katika kila eneo. Tunaweza kuwa na wizara chache ambazo kama mawaziri wangetengeneza sera wangeweza kusimamia masuala mengi katika wizara moja.

Aidha, alieleza masikitiko yake kwa kuona baadhi ya sura za mawaziri ambao wamekuwa wakilalamikiwa na wananchi kutokana na maamuzi yao mabovu. Alisema hali hiyo inapunguza imani ya wananchi kwa serikali yao.

Naye, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, alisema anampongeza rais kwa kuunganisha baadhi ya wizara pamoja na kupunguza ukubwa wa baraza.

Hata hivyo, alisema Rais Kikwete angeweza kupunguza zaidi ukubwa wa baraza hilo kwa kuunganisha wizra nyingine.

“….pamoja na pongezi hizo, nina wasiwasi na baadhi ya uteuzi wa mawaziri. Mfano Chenge alitajwa katika orodha ya mafisadi pale Mwembe Yanga na ni waziri pekee aliyetajwa katika orodha ile ambaye yupo kwenye baraza jipya.

Pia alisema kuwa na wasiwasi wa uteuzi wa Sophia Simba kuwa Waziri katika Ofisi ya Rais; Utawala Bora.

“Sofia Simba akiwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto hakuweza kuleta mabadiliko yoyote katika wizara hiyo…..sasa anapelekwa katika wizara hiyo nyeti. Sina hakika na uteuzi wake,” alisema.

Aidha, alisema nafasi ya wanawake katika baraza jipya imepungua. Baraza lililopita lilikuwa na mawaziri 16 na sasa wapo 11.

“Nafasi ya wanawake katika baraza imepungua. Baraza lililopita wanawake walipewa kuongoza wizara nyeti kama ya Mambo ya Nje, Fedha, Elimu na Sheria na Katiba, lakini sasa wizara zote hizo zimeshikwa na wanaume. “…..hii inatupa ujumbe gani? Wanawake hawakuweza?” alihoji.

Naye mwanasheria na mwanachama wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Mabere Marando, alisema ameridhika na uteuzi wa mawaziri katika baraza jipya.

“Nimeridhika, maveterani wameondolewa, imeingia damu mpya, wajaribu. Tusiwakatishe tamaa,” alisema Marando.

Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, alisema pamoja na Rais Kikwete kutangaza baraza hilo, hajaeleza mikakati ya baraza hilo katika kupambana na ufisadi.

Alisema kitu kilichosababisha kuvunjwa kwa baraza lililopita ni kashfa ya ufisadi, hivyo alipaswa kuweka wazi mikakati ya baraza hilo katika kupambana na ufisadi uliopo.

“Watu wengi tulitegemea rais baada ya kutangaza baraza hilo angeeleza mikakati ya kupambana na tatizo hilo, lakini ameeleza masuala mengine ambayo si ya msingi….tatizo bado lipo palepale,” alisema Mrema.

Mwingine, Mchungaji Christopher Mtikila, alisema analaani kitendo cha watu wanaolalamikiwa na wananchi kuhusika katika masuala ya ufisadi kurudishwa tena katika baraza hilo.

Alisema baadhi ya mawaziri walioteuliwa wana kashfa mbalimbali ambao hawakupaswa kuwepo katika baraza hilo.

“Mabadiliko yaliyofanyika ni ya kuwachezea Watanzania, kwani watu ni wale wale wanageuzwageuzwa,” alisema.

No comments: