Monday, February 11, 2008

JK kuwateua wapinzanina Mwandishi Wetu


WAKATI Rais Jakaya Kikwete, anatarajiwa kutangaza Baraza jipya la Mawaziri leo, kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo sura za wabunge kutoka vyama vya upinzani katika baraza hilo.
Habari za uhakika ambazo gazeti hili limezipata kutoka vyanzo mbalimbali vya habari, zinaeleza kuwa kwa siku kadhaa sasa hadi jana jioni Rais Kikwete, alianza kufanya mashauriano na viongozi wa juu wa vyama kadhaa vya upinzani kuhusu ushiriki wa wawakilishi wao kwenye baraza hilo jipya.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, jana jioni Rais Kikwete alimpigia simu mmoja wa wabunge wa upinzani akimwomba kuingia ndani ya baraza jipya atakalolitangaza leo, jambo ambalo halikupingwa wala kukubaliwa na mbunge huyo badala yake, alimtaka rais kuwaarifu viongozi wa juu wa chama chake.

Kutokana na hilo, Rais Kikwete amedhamiria kuwaingiza wapinzani katika baraza hilo, hali inayotoa tafsiri ya kauli yake ya Februari 5 mwaka huu wakati wa sherehe za miaka 31 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zilizofanyika visiwani Pemba ya kudumisha uhusiano wa serikali yake na kambi ya upinzani.

Aidha, mioyo ya baadhi ya waliokuwapo kwenye baraza lililopita, inakwenda kasi na kushindwa kutabiri kama watatoka au kuingia kwenye baraza hilo.

Kundi lenye hofu zaidi ni lile la mawaziri waliokuwa kwenye baraza lililopita ambao majina yao yalitajwa na Dk. Willbrod Slaa (CHADEMA) kwenye orodha ya majina 11 yanayohusishwa na ufisadi. Baadhi ya mawaziri waliotajwa ni Basil Mramba, Nazir Karamagi, Andrew Chenge na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa.

Hata hivyo, baadhi ya mawaziri wanaohofia kutoingia kwenye baraza jipya kwa sababu ama ya ufisadi au kujihusisha na biashara, suala ambalo Rais Kikwete, alisema wakati wa hotuba yake kwa taifa ya mwisho wa mwezi uliopita, wameonekana Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakiweka mambo sawa ndani ya ofisi zao, kwa vile hakuna mwenye uhakika wa kuendelea kubaki katika wadhifa huo tena katika wizara zilezile.

Zaidi ya mawaziri watano waliondoka mjini Dodoma jana asubuhi wakiwa kwenye magari binafsi huku wakiyaacha mashangingi yao ya kifahari yenye namba za uwaziri na kuelekea Dar es Salaam, yalipo makao makuu ya ofisi zao kwa lengo la ama kuhamisha au kuweka mambo yao sawa ya kiofisi, jambo linaloonyesha wazi kutojiamini kwao.

Katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete kwa ushauri wa Waziri Mkuu mpya, Mizengo Pinda, wanakusudia kupunguza idadi ya mawaziri kutoka 61 waliokuwapo kabla ya baraza hilo kuvunjwa rasmi mwishoni mwa wiki, baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kujiuzulu.

Juzi, Pinda wakati akiapishwa, alikiri kuwa Baraza la Mawaziri lililopita lilikuwa kubwa na mzigo kwa serikali na kuahidi kumshauri rais kupunguza ukubwa wa baraza hilo.

Kutokana na azima hiyo, suala la ufisadi na kasi hafifu ya utekelezaji wa majukumu ya serikali, nyuso za mawaziri wa zamani zimepoteza matumaini huku kila mmoja akikwepa kuzungumza chochote na vyombo vya habari, tofauti na ilivyokuwa awali.

Hata hivyo, baadhi ya waliokuwa mawaziri waliozungumza na Tanzania Daima baada ya kujiuzulu kwa Lowassa, Februari 7 mwaka huu, walisema hawana imani kiasi cha kutabiri tabia ya Rais Kikwete, hivyo kukosa uhakika wa kuendelea na vibarua vyao.

Sababu nyingine inayowafanya mawaziri hao kutokuwa na imani ya kurejea kwenye nyadhifa zao ni kauli, matukio na ushauri kutoka sehemu mbalimbali anaoupata Rais Kikwete kuhusu mzigo mkubwa wa Baraza lake la Mawaziri na mwenendo halisi wa uchumi wa nchi kwa siku za karibuni.

Malalamiko ya ufisadi, kuporomoka kwa umaarufu wa serikali yake na utendaji duni wa baraza hilo ni sababu zinazoweza kufanya uwepo wa baraza dogo la mawaziri wanaotarajia kujumuisha wachapakazi wengi.

Kwa kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne, imeelezwa kuwa kiwango cha kashfa za ubadhirifu wa fedha za umma na ongezeko la pengo kati ya maskini na matajiri ni miongoni mwa mambo yanayomfanya rais kuchukua maamuzi magumu yanayoweza kuwashangaza watu wake wa karibu.

Rais Kikwete alivunja Baraza lake la Mawziri Februari 7, mwaka huu baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa, kuomba kujiuzulu kutokana na kashfa ya utoaji wa zabuni kwa Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond.

Kutokana na kashfa hiyo, Bunge liliunda kamati teule Novemba 13 mwaka jana, kuchunguza mchakato wa zabuni ya Richmond, ambapo ripoti yake ilimhusisha moja kwa moja Lowassa. Mawaziri wengine waliotajwa kuhusika ni Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.

Mkataba huo wa sh bilioni 172.9 uliosainiwa na Serikali kupitia Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), umelisababishia taifa hasara ya mabilioni ya fedha, ambapo hivi sasa taifa linalazimika kulipa sh milioni 152 kila siku kwa Kampuni ya Dowans iliyorithi mkataba huo kutoka kwa Richmond.

No comments: