Monday, February 11, 2008

Pinda aanza kuonyesha makucha
na Kulwa Karedia


SERIKALI imeandaa rungu la kuwadhibiti wakurugenzi wa halmashauri nchini kutokana na matumizi mabaya ya fedha zinazotumwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo kwenye halmashauri zao.
Akizungumza kupitia Televisheni ya Taifa (TvT) juzi usiku, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema serikali imejipanga vya kutosha kuwabana viongozi hao ambao wamekuwa wakitumia fedha za serikali kinyume cha utaratibu uliopo.

“Halmashauri nyingi nchini kupitia kwa wakurugenzi wake zimekuwa na matumizi mabaya ya fedha za serikali kwa kipindi kirefu, sasa utaratibu unaandaliwa wa kuwabana viongozi hawa,” alisema Pinda.

Alisema hali hiyo imesababisha malengo mengi ya serikali kushindwa kutimia au kutekelezwa kutokana na viongozi wachache wasiokuwa waaminifu kutumia fedha hizo kwa manufaa yao.

“Nimekuwa kwenye Wizara ya Tawala za Mikoa (TAMISEMI) kwa kipindi kirefu, naelewa vema matatizo yaliyopo, sisi kama serikali tunajipanga vizuri, ili kuhakikisha tabia hii inakomeshwa,” alisema Waziri Mkuu Pinda.

Kuhusu mikatati ya serikali katika sekta ya afya, Waziri Pinda alisema tayari imejiandaa vya kutosha, kwani hivi sasa iko kwenye hatua za mwisho za kuhakikisha kila kijiji kinajenga zahanati, ili kupunguza matatizo ya matibabu kwa wananchi.

“Kabla sijateuliwa kushika wadhifa huu, tayari serikali ilikuwa imekwishatangaza kuanza kazi ya ujenzi wa zahanati kwa kila kata nchi nzima, hatua hii ni nzuri, itasaidia kupunguza vifo, hasa kwa watoto wadogo mpaka wale wenye umri wa miaka mitano,” alisema.

Kuhusu kilimo, alisema hatua za makusudi zimechukuliwa na serikali na kuanzia mwakani, itatoa pikipiki kwa kila mtaalamu wa kilimo nchini, ili kurahisisha utendaji kazi wao.

“Tumejipanga vema, kuanzia mwakani wataalamu wetu wa kilimo, hasa wale walioko kwenye kata na tarafa, tutawapatia pikipiki, ili kuwafikia wananchi kwenye maeneo yao,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Pinda alisema kuwa anaandaa siku ya kukutana na vyombo vyote vya habari, ili kuzungumza navyo kwa lengo la kujua matatizo na changamoto ambazo zinamkabili.

“Baada ya kuingia hapa, naandaa siku ya kukutana na vyombo vyote vya habari kwa lengo la kubadilishana mawazo juu ya majukumu yanayotukabili… siku zote nimekuwa navyo karibu mno, lazima tukutane,” alisema Waziri Pinda.

No comments: