Monday, February 11, 2008

Mwanyika: Sihusiki kashfa ya Richmond

na Mwandishi Wetu



MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, amesema hana tatizo licha ya kutakiwa kujiuzulu na Kamati Teule ya Bunge, iliyopewa kazi ya kuchunguza mchakato wa zabuni ya Kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond.
Aidha, Mwanyika alishindwa kuweka wazi dhamira yake ya ama kujiuzulu au kusubiri hatua za kinidhamu kutoka serikalini baada ya taarifa ya kamati hiyo iliyosomwa bungeni Jumatano wiki iliyopita kuanza kufanyiwa kazi.

Akizungumza kwa njia ya simu yake ya mkononi na Tanzania Daima jana, mwanasheria huyo alishindwa kabisa kusema dhamira yake. “Eeeh, ‘No comment’…unajingine?” aliuliza Mwanyika kabla ya kuhitimisha mazungumzo yake na gazeti hili.

Lengo la mwandishi wa habari hizi kumtafuta Mwanyika ni kujua hasa nia ya ama kujiuzulu au la, ya mwanasheria huyo anayetajwa kuhusika kwenye sakata la mkataba wa sh bilioni 172.9 kati ya serikali kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na Kampuni hewa ya Richmond.

Hata baada ya kumaliza mazungumzo na gazeti hili saa moja usiku, Mwanyika alituma ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu yake wenye maelezo kuwa vyombo vya habari vinamfuata, lakini hana tatizo lolote na Mungu ndiye anayejua, hivyo anamwomba awasamehe wote.

Ujumbe huo ulisema: “Mnanitafuta lakini mjue kwamba mimi sina tatizo lolote. Mungu ndiye anayejua yote. Mimi namwomba awasemehe kwa hayo yote. Amen.” Hata hivyo, juhudi za gazeti hili kumpigia simu ziligonga mwamba baada ya mwanasheria huyo kutopokea simu iliyotaka kufahamu nia ya Mwanyika kutuma ujumbe huo.

Aidha, taarifa ya kamati hiyo teule iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela Dk. Harrison Mwakyembe (CCM), ilisema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeshindwa kuiwakilisha vema serikali kabla ya kuingia kwa mkataba huo.

Taarifa hiyo ilibaini makosa mengi ya kisheria yaliyosheheni ndani ya mkataba huo, hali iliyoashiria udhaifu mkubwa wa kitaalamu, ukosefu wa umakini ama ubinafsi kwa kushindwa kutambua ukosefu wa sifa za kikampuni zilizopo ndani ya Kampuni ya Richmond Development.

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu pia imeshindwa kuishauri serikali kuifanyia kampuni hiyo ukaguzi wa awali au ukaguzi, baada ya uteuzi na kushindwa kuona dosari za kisheria na kuona tofauti kisheria kati ya Kampuni ya Richmond, RDEVCO, RDVECO na RDC, majina ambayo wamiliki wa Richmond waliyatumia wakibadilisha badilisha kwa makusudi.

Pia taarifa ya Dk. Mwakyembe, iligundua kushindwa kwa Ofisi ya Mwanasheria huyo kuwashauri wajumbe wa Kamati ya Serikali ya Majadiliano (GNT) kuwa kadi ya biashara (business card) si mbadala wa hati mahususi kisheria na kushindwa kuishauri serikali kuhakikisha kuwa muhtasari wa majadiliano kati ya GNT na Richmond, ulizingatia baadhi ya masilahi ya nchi.

Mwanyika kupitia ofisi, na mwakilishi wake aliyetajwa kwa jina la Donald Chidowu, walishindwa kuishauri serikali kutumia fursa ya wazi ya kuvunja mkataba baada ya Kampuni ya Richmond kushindwa kutekeleza sehemu yake ya mkataba wake na kushindwa kuhudhuria idadi kubwa ya vikao muhimu vya majadiliano.

Kwa mujibu wa taraifa hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika majadiliano yake na kamati hiyo, alionyesha kutoelewa kabisa kilichokuwa kinatendwa na wasaidizi wake.

Kwa maelezo hayo, kamati hiyo teule ilimtaka Mwanasheria Mkuu na Mwakilishi wake kuwajibishwa kinidhamu, kwa kuwa ushiriki wake kwenye GNT haukuwa na tija, hali iliyochangia kuliingiza taifa katika mkataba huu wa aibu uliogharimu sh bilioni 172.9.

Baada ya kusomwa kwa taarifa ya kamati hiyo iliyofanya kazi kwa siku 45 chini ya uenyekiti wa Dk. Mwakyembe, aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, alijiuzulu kwa tuhuma za kushinikiza ushindi wa zabuni ya kampuni hiyo na kusababisha Rais Jakaya Kikwete, kuvunja Baraza la Mawaziri.

Pamoja na Lowassa, mawaziri wengine walioguswa kwa tuhuma za kuiingiza nchi kwenye mkataba huo wa aibu na hasara ambao nao walijiuzulu ni Nazir Karamagi, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini. Waziri huyu anatuhumiwa kushabikia mkataba huu huku akijua fika kuwa na hasara kwa taifa.

Naye aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo Dk. Ibrahim Msabaha, alijiuzulu baada ya kutakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kuliingiza taifa kwa makusudi kwenye mkataba na kampuni ya mfukoni, uliosababisha hasara, ambapo sasa Kampuni ya Dowans, iliyorithi mkataba wa Richmond kulipwa sh milioni 152 kila siku kwa miaka miwili.

No comments: