Saturday, February 9, 2008

Ni Mizengo Pinda


na Peter Nyanje



RAIS Jakaya Kikwete, amemteua mmoja wa wanasiasa wanaoheshimika, Mizengo Peter Kayanza Pinda, kuwa Waziri Mkuu wa tisa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uamuzi huo wa Kikwete unakuja siku moja tu baada ya kuridhia uamuzi wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu baada ya kuhusishwa katika kashfa ya mkataba wenye utata wa Richmond.

Kuteuliwa kwa Pinda kuwa Waziri Mkuu, kunamfanya awe mwanasiasa wa 10 kushika wadhifa huo hapa nchini, ukianzia na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Aidha, Pinda anakuwa ni Waziri Mkuu wa tisa kushika wadhifa huo tangu kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964.

Mwanasiasa wa kwanza kushika wadhifa wa Waziri Mkuu tangu Tanganyika iwe Jamhuri na baadaye Tanzania, alikuwa ni Rashid Kawawa aliyeshika wadhifa huo kwa mara ya kwanza kati ya Januari 1962 hadi Desemba 1962.

Aidha, baada ya wadhifa huo kufutwa katika kipindi cha kati ya Desemba 1962 na Februari 1972, Kawawa aliyekuwa Makamu wa Pili wa Rais, alishika tena wadhifa huo katika kipindi cha kati ya 1972 na Februari 1977.

Pinda, mwanasiasa mkimya na mwenye heshima ya pekee miongoni mwa waliokuwa mawaziri katika Baraza la Mawaziri lililovunjwa juzi, anachukua wadhifa huo wa tatu wa juu kimamlaka hapa nchini akiungwa mkono na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa upinzani.

Katika kuonyesha namna uteuzi wake ulivyoungwa mkono kwa nguvu na wabunge, Pinda aliungwa mkono na wabunge 279 kati ya 282 waliopiga kura za siri bungeni mjini hapa, jana, na hivyo kumfanya apate ushindi wa asilimia 98.9.

Katika uchaguzi huo, wabunge wawili walipiga kura za kumkataa huku kura moja ikiharibika.

Kama ilivyo ada, uteuzi wa Pinda kushika wadhifa huo, ulitangazwa jana jioni bungeni mjini Dodoma na Spika wa Bunge, Samuel Sitta.

Kabla ya kufungua bahasha iliyokuwa na jina la Waziri Mkuu mteule, Sitta alisema alikabidhiwa bahasha hiyo na Rais Kikwete majira ya saa 10:00 jioni jana hiyo hiyo.

Alipolitaja jina la mwanasiasa huyo ambaye minong’ono ilikuwa imeshaanza kumtaja kabla hata ya kikao hicho cha Bunge, wabunge walilipuka na kushangilia.

Mara baada ya tukio hilo, Sitta alimuita Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika kutoa hoja ya kuwataka wabunge kuridhia uteuzi huo wa rais.

Kabla ya kazi ya kupiga kura za siri kumuidhinisha waziri mkuu mteule, wabunge kadhaa wa pande zote mbili walizungumza wakieleza kuunga mkono uteuzi wa Rais Kikwete.

Wabunge takriban wote waliozungumza walimuelezea Pinda kuwa mwanasiasa mchapakazi, mwadilifu, asiye na makuu na anayewaheshimu wabunge wa upinzani na wale wa CCM.

Miongoni mwa wabunge hao, alikuwa ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohammed.

“Namfahamu Pinda tangu mwaka 1972 baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani. Ni mtu mwadilifu wa kusimamia haki, kwa hili sote tumefarijika sana. Tunampongeza Rais Kikwete na tutampatia ushirikiano,” alisema.

Alisema kambi ya upinzani itampatia ushirikiano wote ili kuhakikisha Watanzania wanaondoka kwenye dimbwi la umasikini.

“Nawaomba wabunge wenzangu tuungane ili kumuondoa Mtanzania kwenye dimbwi la umasikimi, tofauti zetu tutaziacha pale tukiona kuna maslahi ya kitaifa,” alisema Hamad.

Akichangia mjadala huo, Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa hakusita kummwagia sifa Pinda akimwelezea kuwa ni kiongozi shupavu anayeweza kuvaa viatu vyake.

“Nimefarijika ameingia Waziri Mkuu tunayefanana naye sana. Anaingia mtu mchapakazi kweli kweli, mzoefu na mkweli, anaingia mtu ambaye ni kada wa CCM,” alisema Lowassa na kushangiliwa.

Alimwelezea Pinda kuwa mtu anayejali maslahi ya wanyonge, mwenye uzoefu mkubwa na serikali na Bunge.

Mbunge wa Ukerewe, Gertrude Mongella (CCM) hakusita kuonyesha hisia zake juu ya uteuzi huo kwa kusema Rais Kikwete ameteua mtu makini.

“Ndugu yetu Lowassa haondoki kwa sababu ana mapungufu ya utendaji kazi, ameondoka kwa kidemokrasia, huu ni mfano wa kuigwa,” alisema.

Naye Anna Abdallah (Viti Maalum - CCM), alisema Pinda hajachupia ndani ya Bunge wala CCM, na kwamba ameanzia chini hali iliyomjengea heshima na uaminifu mkubwa katika utendaji kazi wake.

“Alikuwa msaidizi wa Mwalimu Nyerere kuanzia enzi za TANU, ndani ya chama amekomaa, tumepata kada kamili,” alisema.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), alisema hatua ya kuteuliwa kwa Pinda imetokana na misingi imara ya taifa iliyowekwa na waasisi, kwani imesaidia taifa kushinda hata katika kipindi kigumu.

“Sisi kambi ya upinzani tutampatia ushirikiano wote atakaohitaji kutoka kwetu ili kujenga taifa letu,” alisema na akaongeza kueleza namna Pinda alivyotuliza mvutano kati ya chama chake na CCM katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Mbunge wa Mtera, John Malecela (CCM), alimmwagia sifa Rais Kikwete kwa kumchagua mtu shupavu.

“Kikwete ametumia hekima zake, baada ya yote ametuteulia mwenzetu ambaye sifa zake zimesomwa hapo na zinastahili kuchukua madaraka ya kuendesha nchi hii,” alisema.

Aliwataka wabunge kukumbuka kuwa nchi ndiyo yenye maslahi ya kudumu na kwamba wao wabunge wanakwenda na wengine wanakuja.

Mbunge wa Njombe Kusini, Anne Makinda (CCM), alisema: “Uteuzi huu ni wonderful (ni safi sana)… Rais Kikwete asingeweza kufanya vizuri zaidi ya hapa.”

Alisema kuwa Pinda ni muadilifu na mnyenyekevu, na kuongeza kuwa anaamini atafanya kazi vizuri kwa kuwa ni mtu sahihi.

Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (CCM), alisema uteuzi huo ni muafaka, kwani ni mtu anayejali na kuheshimu kila mtu.

“Pinda yupo hivyo akiwa kazini na hata kwenye mapumziko ana sifa hizo hizo, hivyo ataendeleza zama mpya za uwazi katika utendaji wake wa kazi,” alisema.

Mbunge wa Njombe Kaskazini, Jackson Makwetta (CCM), alisema ameridhirishwa na uteuzi huo na kuongeza kuwa, ana mtaji mkubwa kuwa ametoka TAMISEMI, ambako kumemwezesha kuifahamu nchi, hivyo ataweza kufanya kazi yake vizuri.

Kwa mujibu wa Spika Sitta, Pinda ataapishwa leo katika Ukumbi wa Chamwino, mjini hapa.

No comments: