Friday, February 8, 2008

Serikali yameguka





Lowassa akubali yaishe, aomba kujiuzulu
na Mwandishi Wetu
RIPOTI ya kamati iliyochunguza mkataba wa Richmond, iliyowasilishwa bungeni juzi, imelipua moto mkubwa wa kisiasa ambao haujapata kutokea kwa miaka mingi ndani ya nguzo hiyo muhimu ya dola.
Joto la ripoti hiyo iliyosomwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe, lilianza kuonekana mapema jana asububi, baada ya Waziri Mkuu Edward Lowassa, kutangaza kuandika barua kwa Rais Jakaya Kikwete ya kuomba kujiuzulu wadhifa huo wa juu nchini.

Moto huo wa kisiasa ulikuwa mkali zaidi wakati wa mjadala wa Bunge jana jioni pale wabunge walipoanza kuijadili ripoti hiyo.

Katika mjadala huo, takriban wabunge wote waliochangia waliiunga mkono ripoti ya kamati na wakawataka viongozi wote waliohusika katika kuipa mkataba Richmond, kuwajibika au kujiuzulu.

Hoja hizo za wabunge zilisababisha Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha watangaze dhamira yao ya kujiuzulu wakisema, walikuwa wameshawasilisha maombi yao hayo kwa Rais Kikwete asubuhi hiyo hiyo ya jana.

Mbunge wa kwanza kuchangia hoja hiyo jana jioni, alikuwa Anne Kilango Malecela (CCM), ambaye alieleza bayana kukerwa na mkataba huo, na akaahidi kwamba ugunduzi wa uchafu ndani ya Richmond ulikuwa ni mwanzo tu wa safari ya kuwasafisha viongozi wote walarushwa serikalini.

Akizungumza katika mjadala huo, Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (CHADEMA), alisema, ingekuwa ni China mafisadi kama wale walioshiriki katika Richmond wangenyongwa.

Kwa sababu hiyo basi, Ndesamburo na Willibrod Slaa walilitaka Bunge na serikali kufanya kila linalowezekana kuwachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafilisi wale wote waliohusika katika ufisadi wa Richmond.

Hata hivyo, hadi wakati mjadala huo ulipokuwa umeanza jana jioni, Rais Kikwete alikuwa hajaridhia kujiuzulu kwa waziri mkuu wake, Lowassa na mawaziri wengine wawili.

Iwapo Kikwete ataridhia uamuzi huo, basi Lowassa, anaweza akawa kiongozi wa kwanza mwenye wadhifa huo kuondoka madarakani kutokana na tuhuma zilizomhusisha yeye binafsi moja kwa moja ndani ya Bunge, tangu uhuru mwaka 1961.

Katika tamko lake hilo la kujiuzulu alilotoa jana asubuhi, Lowassa alielezea ripoti ya kamati ya Mwakyembe kuwa iliyowasilishwa kwa mbwembwe nyingi.

Lowassa katika hotuba yake hiyo, alieleza kutoridhishwa na namna kamati hiyo ilivyofanya kazi kwa kuwahoji mashahidi mbalimbali na kujumuisha vielelezo mbalimbali pasipo kumhoji yeye.

“Mheshimiwa Dk. Harrison Mwakyembe ni mwanasheria, tena daktari, alikuwa anafundisha wanafunzi chuo kikuu. Moja ya vitu alivyokuwa anafundisha ni “Natural Justice.” Mheshimiwa Spika, wewe pia ni mwanasheria unafahamu suala la natural justice.

“Kwamba kamati teule imesikiliza watu wengine wote pamoja na wanaoita minong’ono ya mitaani, wamesafiri mpaka Marekani kutafuta mashahidi, lakini mimi ambaye ni mmoja katika watuhumiwa mle, hawakunihoji hata siku moja,” alisema Lowassa alipozungumza kama mchangiaji wa kwanza.

Lowassa alieleza kusikitishwa kwake na namna Kamati ya Mwakyembe ilivyofikia hatua ya kutumia uvumi wa mitaani kuwa uthibitisho unaomhusisha yeye katika mkataba wa Richmond.

Mbali ya hilo, Lowassa katika hatua inayoweza kuibua maswali mengi, baadaye alisema alipojiuliza sababu za kamati hiyo kushindwa kumtendea ‘natural justice’ (haki ya msingi) ya kumhoji, alibaini tatizo la msingi lilikuwa ni uwaziri mkuu wake.

Kwa kutambua hilo, Lowassa alisema alikuwa tayari kuiachia nafasi hiyo kubwa ya tatu kimadaraka, na ndiyo sababu iliyosababisha aamue kumuandikia barua rais kumuomba ajiuzulu.

“Mheshimiwa Spika, lakini nimetafakari kwa makini sana jambo hili, nikajiuliza hivi, hasa kulikoni mpaka watu wazima wenye uwezo wao, watu maarufu wenye heshima zao, mpaka wafike mahali waache jambo la msingi kama hilo, kulikoni?

“Mimi nadhani ‘there is a wish which I am going to grant’, ni uwaziri mkuu. Nadhani tatizo ni uwaziri mkuu. Kwamba ionekane Waziri Mkuu ndiye amefanya haya, tumuondolee heshima au tumwajibishe,” alisema Lowassa aliyekuwa akizungumza kwa utulivu.

Alisema jambo hilo limemuumiza, kumsikitisha na kumdhalilisha sana na kuhoji: “Iwapo kama Waziri Mkuu anafanyiwa hivi, nachelea kuuliza je mtu wa chini itakuwaje?”

Tamko hilo la Lowassa liliibua mshtuko ndani ya Bunge na wabunge kadhaa wakasisimama kuchangia kusudio hilo la Waziri Mkuu kujiuzulu.

Wa kwanza kuonyesha mshtuko huo, alikuwa ni Spika wa Bunge, Samuel Sitta ambaye alisema hakutarajia kwamba Lowassa angetoa tamko hilo na hivyo akaomba maoni ya wabunge.

“Tamko hili ni zito, sikulitarajia, naomba ushauri tuendeje,” alisema Sitta.

Kauli hiyo ya Spika ilimfanya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA) kusimama na kuomba muongozo wa Spika akisema kwamba tamko la Lowassa lilikuwa likimaanisha kuwa mawaziri wote walikuwa wamejiuzulu pia.

Ingawa Zitto hakunukuu Katiba ya Jamhuri ya Muungano alichokisema kiko katika Ibara ya 17 (1) (e) kinachosema nafasi ya waziri au naibu waziri itakuwa wazi iwapo Waziri Mkuu atajiuzulu.

Hata hivyo, baada ya hoja hiyo ya Zitto, Spika wa Bunge alitoa ufafanuzi kwa kusema kuwa rais alikuwa hajamtaarifu iwapo alikuwa amekubali uamuzi huo wa Lowassa, na hivyo kumfanya aendelee kushikilia wadhifa huo hadi hapo atakapopata maelekezo mengine.

Akizungumza nje ya Bunge jana asubuhi, Lowassa alisema ameamua kuwajibika baada ya kuona kamati ikitumia maneno mengi ya kuichonganisha serikali na watu wake.

Alipotakiwa aeleze atafanya nini iwapo rais atakataa ombi lake la kujiuzulu, alisema kuwa atasubiri hadi wakati huo na kuelezea suala hilo.

Alipomaliza kusema hayo, aliondoka akiwa ameandamana na wasaidizi wake, na kuelekea katika ofisi zake bungeni kabla ya kuondoka baadaye.

Kambi ya Upinzani Bungeni, imepongeza hatua ya Lowassa, ingawa ilibainisha kuwa imesikitishwa na maneno aliyoyatumia Lowassa katika kauli yake.

Kiongozi wa kambi hiyo, Hamad Rashid Mhammed (Wawi-CUF) alisema kuwa Lowassa alipaswa kuonyesha ukomavu wake kwa kuwajibika bila kulalamika.

Alisema kuwa kulalamika kwa Lowassa kuwa ameonewa, si jambo zuri, kwani linaondoa ile dhamira yake ya kuwajibika kwa maslahi ya serikali, chama chake na nchi kama mwenyewe alivyosema.

Hamad alimtaka rais kukubali ombi la Lowassa na kwa kuwa kujiuzulu kwa Waziri Mkuu kunamaanisha kujiuzulu kwa baraza lote la mawaziri, achukue fursa hiyo kupanga upya timu yake kwa manufaa ya Watanzania kulingana na wakati na mambo yaliyojitokeza.

Mbunge wa Mtera, John Samuel Malecela, na makamu mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mstaafu, alisema kuwa anayaheshimu maamuzi yaliyofikiwa na Lowassa na kuwataka watu wengine kumpa fursa kiongozi huyo kusema kilichomo moyoni mwake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alitoa kauli fupi sana: “Ni shock (mshituko) kwangu mimi.”

Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF) alisema kuwa, alichofanya Lowassa ni kizuri kwa sababu ‘tuhuma zinapokuwa kubwa kiasi cha kuathiri personality (utu) ya mtu, jambo zuri ni kujiuzulu.’

“Alichofanya Lowassa si tu ni kizuri, bali ni ishara ya namna ya uongozi unaotakiwa kwa nchi hii na hii inawataka wale wote ambao wamekutwa na kashfa na tuhuma kama hizi, wafuate nyayo zake,” alisema.

Alisema ni vema viongozi wakajenga utamaduni wa kuwajibika kwa mambo hata wasiyoyafanya wao binafsi, kwani hata Lowassa amewajibika kutokana na yale yaliyotokea chini ya usimamizi wake.

Martha Mlata (Viti Maalum-CCM) alisema kuwa, Lowassa ameonyesha njia na kuwashauri viongozi wengine kufanya hivyo kwa maslahi ya wengi, huku akitolea mfano wa Yesu Kristo, ambaye alikubali kufa msalabani ili wengi waokoke.

Chacha Wangwe (Tarime-CHADEMA) alisema kuwa yaliyotokea ni matokeo ya ujenzi mbaya uliofanywa na CCM yenyewe.

“Hii ni things fall apart (mambo yamesambaratika),” alisema.

Phillemon Ndesamburo (Moshi Mjini-CHADEMA), naye alisema kuwa amefurahishwa na uamuzi wa Lowassa na haoni kama ameonewa kama yeye mwenyewe alivyolalamika.

“What goes around comes around,” alisema akibainisha kuwa mambo unayoyafanya leo yanaweza kukuandama baadaye.

Ulitokea utata wa kisheria na kikatiba kuhusu hatua aliyoichukua Lowassa, huku baadhi ya watu wakisema kuwa kwa mujibu wa katiba, iwapo Waziri Mkuu ataamua kujiuzulu, rais hana mamlaka ya kukataa moja kwa moja.

Mmoja wa wabunge wanasheria alisema kuwa, kwa mujibu wa Ibara ya 51(3)(c) ya katiba, mamlaka ya Waziri Mkuu yanakoma pale atakapojiuzulu na si rais atakapokubali kujiuzulu kwake.

Alisema kutokana na ibara hiyo, anachoweza kufanya rais sasa ni aidha kulirudisha tena jina la Lowassa kama Waziri Mkuu mteule akimaanisha kuwa amekataa ombi lake hilo.

No comments: