Thursday, February 7, 2008

Richmond yaivua nguo serikali


na Mwandishi Wetu
KAMATI Teule ya Bunge iliyochunguza mchakato wa upatikanaji wa zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura, iliyopewa Kampuni ya Richmond Development LLC, ya Hauston Marekani, imemtaja Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kuwa alihusika kuibeba kampuni hiyo kupata zabuni hiyo.
Kutajwa kwa Lowassa kuhusika katika kashfa hiyo, kuliwashtusha wengi, wakiwemo wabunge waliokuwa wakimsikiliza Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe, Mbunge wa Kyela (CCM), wakati akisoma ripoti ya kamati yake bungeni jana, iliyowafanya wabunge kuwa katika hali ya utulivu usiokuwa wa kawaida, akiwemo Spika wa Bunge, Samuel Sitta.

Aidha, hatua ya kamati ya Dk. Mwakyembe kumpa nafasi Lowassa kupima uzito wa matokeo ya uchunguzi wa kamati hiyo yanayoweza kumtia katika kashfa ya kutumia vibaya madaraka yake iwapo atashindwa kutoa maelezo ya kuwaridhisha wabunge na wananchi inaweza kubadili kabisa mwenendo wa mambo serikalini katika siku chache zijazo.

Mbali ya Lowassa kupewa fursa hiyo ambayo inaweza ikawa ni lugha ya kistaarabu ya kumtaka mkubwa ajiwajibishe mwenyewe, Bunge ambalo leo linaanza kuijadili ripoti hiyo ya Kamati ya Mwakyembe limetakiwa kuchunguza iwapo matokeo ya uchunguzi huu hayatakuwa yameathiri hadhi na uzito wa kiongozi huyo ndani ya taasisi hiyo.

Dk. Mwakyembe katika ripoti yake, aliliambia Bunge kuwa, ushiriki wa karibu wa Lowassa katika kila hatua ya zabuni ya umeme wa dharura, si lazima uwe ushahidi kwamba kiongozi huyo wa kitaifa alihusika katika kuibeba Richmond, lakini unaweza ukawa ushahidi wa staili yake ya kawaida kabisa ya uongozi katika kufuatilia masuala yote ya kitaifa kwa karibu, ikizingatiwa kwamba taifa lilikuwa katika kipindi kigumu cha ukosefu wa umeme.

“Mheshimiwa Spika, ushiriki huu wa karibu wa Waziri Mkuu katika kila hatua ya zabuni ya umeme wa dharura, si lazima uwe ushahidi wa kwamba kiongozi huyo wa kitaifa alihusika katika kuibeba Richmond. Unaweza pia ukawa ushahidi wa staili yake ya kawaida kabisa ya uongozi katika kufuatilia masuala yote ya kitaifa kwa karibu sana, tukizingatia kwamba nchi wakati huo ilikuwa katika kipindi kigumu sana cha ukosefu wa umeme,” alisema Mwakyembe katika hatua moja ya awali ya ripoti yake.

SOMA RIPOTI KAMILI YA SERIKALI YA KIZUSHI HAPA

Baadhi ya hoja zilizotajwa na Dk. Mwakyembe kuwa ziliishawishi kamati yake kuamini kuwa Lowassa alihusika kuibeba Richmond kupata zabuni hiyo, ni barua ya Katibu wa Lowassa ya Juni 21, 2006, B. Olekuyan, ya kuitaarifu Wizara ya Nishati na Madini kuwa Waziri Mkuu Lowassa amekubali mapendekezo na ushauri wa Waziri wa Nishati na Madini kama ulivyokuwa umeletwa.

“Aidha, baadhi ya nyaraka ambazo Kamati Teule ilipata katika uchunguzi wake zilionesha kuwa maelekezo na maamuzi mengi ya msingi yalikuwa yanafanywa na Waziri Mkuu badala ya wizara. Mfano ni barua kutoka Wizara ya Nishati na Madini kwenda kwa Waziri Mkuu tuliyoinukuu ukurasa wa 31 wa taarifa hii, ikitamka wazi kuwa GNT ilifanya majadiliano na Richmond Development Company LLC tarehe 8 hadi 16 Juni 2006 “kwa kuzingatia maelekezo” ya Waziri Mkuu,” alieleza Mwakyembe.

Kwamba, baada tu ya kupokea barua hiyo, Waziri wa Nishati na Madini aliandika dokezo kwa Katibu Mkuu wake akimtaka aiagize TANESCO iingie mkataba mara moja na Richmond Development Company LLC baada ya Waziri Mkuu kuidhinisha mapendekezo ya wizara.

Dk. Mwakyembe alisema kamati yake ilibaini kuwa hisia walizokuwa nazo viongozi wa ngazi mbalimbali wa TANESCO, uongozi wa kiimla wa wizara ulikuwa ukipata nguvu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kwamba kilichoonekana ni ukiukwaji wa sheria na utaratibu mzima wa uwajibikaji, na kwamba pamoja na dharura iliyokuwa ikilikabili taifa, serikali haipaswi kuwa kinara wa kuvunja sheria za nchi.

Aidha, Dk. Mwakyembe alisema kuwa baadhi ya mashahidi, wakiwemo waandishi wa habari waliinyoshea kidole Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa msingi wa ubabe uliokithiri wa Wizara ya Nishati na Madini katika kuibeba Richmond.

Alizitaja pia baadhi ya nyaraka ambazo kamati yake ilizipata katika uchunguzi wake, zilionyesha kuwa maelekezo na maamuzi mengi ya msingi yalikuwa yakifanywa na Lowassa badala ya wizara.

Alitoa mfano wa barua kutoka Wizara ya Nishati na Madini kwenda kwa Waziri Mkuu iliyonukuliwa ukurasa wa 31 wa ripoti ya kamati ikitamka kuwa Juni 8, 2006 GNT ilifanya majadiliano na Kampuni ya Richmond kwa kuzingatia maelekezo ya Lowassa.

Dk. Mwakyembe alilieza Bunge kuwa kamati yake pia ilibaini kuwa Julai 13, 2006 Waziri wa Nishati na Madini alimwandikia Katibu Mkuu wake kumweleza kuwa kwa mara nyingine amezungumza na Lowassa juu ya bei ya mitambo ya Aggreko.

Katika mazungumzo hayo, Lowassa alibaki na msimamo ule ule ulioelezwa na waziri kuwa aliagiza Richmond iulizwe kama inaweza kuzalisha Megawati 40 za umeme kwa bei isiyozidi senti 4.99 za Marekani na kama ikipatikana, basi ichukuliwe Richmond.

Dk. Mwakyembe ambaye wakati wote wa kusoma ripoti hiyo alionekana kutamka maneno bila kumung’unya, alisema kamati yake ililazimika kuwaita kwa mara ya pili Dk. Ibrahim Msabaha aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini na Katibu Mkuu wake, Mwakapugi, kwa ajili ya kuwahoji.

Katika mahojiano hayo ya mara ya pili, wote wawili, wakiwa ndani ya kiapo, walikataa kupokea maagizo ya kuipa upendeleo Kampuni ya Richmond, kutoka kwa Lowassa.

Lakini Dk. Msabaha ambaye sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, baada ya kumaliza kuhojiwa chini ya kiapo, aliwauma sikio wajumbe wa kamati hiyo kuwa, yeye anatolewa kama kondoo wa kafara, lakini mhusika mkuu ni mkuu wake wa kazi.

Alieleza zaidi kwamba hata Balozi Fulgence Kazaura katika maelezo yake nje ya kiapo naye alisema kwamba Richmond ni mradi wa bwana mkubwa na mshiriki wake mkubwa wa kibiashara ambaye Dk. Mwakyembe alimtaja kuwa ni Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Alisema ingawa ushahidi wa ziada na nje ya kiapo wa Dk. Msabaha na Balozi Kazaura haukutoa msaada stahili kwa kumhusisha Lowassa, kwa vile Bunge halichukui maamuzi kwa minong’ono au tetesi, isipokuwa taarifa zenye uthibitisho halisi, lakini viongozi hawawezi kumtaja Waziri Mkuu Lowassa wakiwa chini ya kiapo, hata kama ni kweli anahusika, kwa sababu hatua hiyo inahitaji ujasiri mkubwa na uzalendo wa hali ya juu.

Alisisitiza kuwa, pamoja na woga uliokuwa dhahiri wa watumishi hao, ushahidi wa maandishi, wa mdomo na kimazingira ambao kamati yake iliupata kutoka kwa mashahidi mbalimbali, ulimhusisha Lowassa na mchakato wa maamuzi katika suala la Richmond.

Huku akishangiliwa na wabunge, Mwakyembe alisema uvumi kwamba Lowassa na baadhi ya washirika wake wanahusika katika suala hili la Richmond umeenea sehemu nyingi nchini.

Kwamba, ingawa uvumi huo unaweza kuwa umechangiwa na mahasimu wake kisiasa, lakini uharaka, urahisi na wepesi wa wananchi kuziamini tetesi hizo, unazua maswali mengi kuhusu imani, taswira, na heshima ambayo Lowassa amejijengea katika jamii.

Ripoti ya Dk. Mwakyembe inahitimisha uvumi wa muda mrefu uliokuwa ukisambaa kwa kasi kuhusu utata wa zabuni iliyopewa Kampuni ya Richmond kuwa baadhi ya viongozi wakuu serikalini walikuwa na mkono wao katika upatikanaji wa zabuni hiyo.

Ingawa kwa nyakati tofauti, wasaidizi wa Lowassa wamekuwa wakitoa matamko ya kukanusha uvumi huo, ripoti hiyo ya Dk. Mwakyembe inawaweka njia panda wasaidizi hao wa Lowassa na pia inampa mtihani Rais Jakaya Kikwete wa ama kuendelea na Lowassa ambaye sasa anaonekana kuwa moja ya sababu za kuporomoka kwa umaarufu wa serikali yake au kumtosa.

Mbali ya Lowassa, kamati hiyo imeitaka serikali na hususan Rais Kikwete kuwawajibisha Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Waziri Msabaha kutokana na kushiriki katika mkakati wa kuipa zabuni Richmond ambayo kimsingi imethibitika pasipo shaka kuwa ni ya kitapeli.

Chini ya mtiririko huo, Rais Kikwete ameshauriwa katika ripoti hiyo ambayo Tanzania Daima imeuchapisha muhtasari wake wote uliosomwa na Mwakyembe bungeni jana kuwa anatakiwa kufanya mabadiliko ya maofisa wote wakuu katika Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), ambao Mei mwaka jana walitoa taarifa ta kuisafisha Richmond kwa kusema hakukuwa na ushahidi wowote wa kuwapo wa vitendo vya rushwa.

Kwa mwelekeo huo, basi Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Edward Hoseah, ambaye ripoti yake ya kuisafisha Richmond ilizua malalamiko mengi kutoka kwa wadau mbalimbali hapa nchini wakiwamo wana habari.

Kamati hiyo iliundwa na Spika Sitta Novemba 15, mwaka jana na kupewa siku 30 za kukamilisha kazi ya kuchunguza mchakato wa zabuni hiyo.

Hadidu za rejea za kamati hiyo zilikuwa kubainisha Richmond Development Company LLC ni kina nani, na ni kampuni ya shughuli zipi na kupima uwezo wake kupatiwa zabuni ya kuleta na kujenga mtambo wa umeme wa gesi wa MW 100 nchini.

Pia ilitakiwa kutathmini mchakato mzima wa jinsi zabuni ilivyoshughulikiwa kuanzia kamati ya zabuni hadi kupatikana mzabuni ili kujiridhisha kuwa sheria, taratibu, miiko na maadili ya zabuni yanayotawala zabuni za aina hiyo vilifuatwa au vipi.

Kutathmini mkataba baina ya Richmond na TANESCO ili kujiridhisha kuhusu uhalali wa masharti ya mkataba kwa kuzingatia gharama na masharti mengine, ikilinganishwa na masharti yaliyomo katika mikataba ya aina hiyo iliyoafikiwa na TANESCO/Serikali.

Kubainisha huduma na misaada mbalimbali waliyopewa Richmond kama vile kufunguliwa ‘Letter of Credit’ na kupima uhalali wake.

Kuziangalia na kuzitolea maoni taarifa za TAKUKURU, PPRA na taarifa zozote nyingine zilizoangalia utaratibu wa zabuni ya Richmond na kuangalia mambo mengine yoyote yenye uhusiano na mchakato mzima wa Richmond, ili kutoa mapendekezo ya kuboresha taratibu za zabuni kwa siku zijazo, kwa masilahi ya taifa.

No comments: