Wednesday, February 13, 2008

Mawaziri 19% wapya

na Peter Nyanje na Rahel Chizoza, DodomaRAIS Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko makubwa katika Baraza la Mawaziri akipunguza idadi ya mawaziri kutoka 61 na kufikia 47, huku mawaziri tisa na manaibu wanane waliokuwa katika baraza lililopita wakiachwa.

Akitangaza baraza hilo ambalo limekuwa likisubiriwa kwa hamu na wananchi wengi katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mjini hapa, Rais Kikwete alisema uundaji wa serikali yake hiyo mpya umezingatia majukumu ya serikali, mahitaji ya maendeleo, wakati tuliopo na ufanisi wa utekelezaji.

Katika baraza hilo jipya, ambalo linatarajiwa kuapishwa leo majira saa 7:30 mchana katika Ikulu ndogo ya Chamwino, nje kidogo ya Dodoma, mawaziri kamili ni 26 na manaibu 21 ukilinganisha na la zamani lililokuwa na mawaziri 29 (ukimtoa Waziri Mkuu) na manaibu 31.

Katika mabadiliko hayo ya jana, asilimia 81 ya mawaziri wanaounda serikali mpya ya sasa ni wale waliokuwamo katika baraza lililopita na hivyo kuwafanya wapya walioingia kuwa ni asilimia 19 tu.

Miongoni mwa wabunge walioachwa katika baraza hilo jipya yuko Zakia Hamdan Meghji, aliyekuwa Waziri wa Fedha, mwanamke aliyedumu serikalini mfululizo bila kukosa, kwa miaka mingi akiteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa naibu waziri kabla ya kupanda na kuwa waziri kamili wakati wa muhula wa kwanza wa utawala wa rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi (1985-1995).

Kuondoka kwa Meghji kunahitimisha mlolongo wa lawama zilizokuwa zikivurumishwa kwake, tangu alipopewa wizara hiyo ngumu na nyeti miaka miwili iliyopita, kwa kiwango cha kumfanya apoteze sifa yake ya miaka mingi ya ‘Mwanamke wa Chuma’ (Iron Lady), aliyopewa zama akiwa Waziri wa Afya na baadaye Waziri wa Maliasili na Utalii katika serikali zilizopita.

Mbali ya Meghji, wengine walioachwa katika baraza hilo ni pamoja na Anthony Diallo (Maendeleo ya Mifugo), Nazir Karamagi (Nishati na Madini), Dk. Ibrahim Msabaha (Afrika Mashariki), Bakari Mwapachu (Usalama wa Raia) na Basil Mramba (Viwanda, Biashara na Masoko).

Wengine ni James Mungai (Mambo ya Ndani), Juma Ngasongwa (Mipango, Uchumi na Uwezeshaji) na Kingunge Ngombale-Mwiru (Siasa na Mahusiano ya Jamii).

Rais Kikwete alisema Ngombale-Mwiru na Mungai kuwa ni wanasiasa walioachwa kutokana na wao wenyewe kuomba kupumzika baada ya kuitumikia serikali kwa miaka mingi.

Wakati kuachwa kwa Karamagi na Msabaha kunahusishwa moja kwa moja na kashfa ya Richmond iliyofumuliwa bungeni wiki iliyopita, kuwekwa kando kwa Diallo na Mramba kulikotarajiwa, kunahusishwa zaidi na msimamo wa Rais Kikwete wa kutaka kutenganishwa kwa shughuli za kibiashara na za uongozi wa kisiasa.

Mbali ya hao, waliokuwa manaibu waziri ambao nao wameingia katika kundi la walioachwa ni pamoja na Abdisallam Issa Khatib (Fedha), Zabein Mhita (Maliasili na Utalii), Rita Mlaki (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Dk. Luka Siyame (Maafa na Kampeni za Ukimwi), Ludovick Mwananzila (Elimu na Mafunzo ya Ufundi), Daniel Nsanzugwanko (Habari, Utamaduni na Michezo), Charles Mlingwa (Maendeleo ya Mifugo) na Gaudence Kayombo (Mipango, Uchumi na Uwezeshaji).

Katika mabadiliko hayo, Rais Jakaya Kikwete amewapandisha vyeo vijana wawili waliokuwa manaibu waziri na akawafanya mawaziri kamili, wote akiwaacha kuongoza wizara zile zile walizofanya kazi wakiwa manaibu kwa mfano ule ule ilivyotokea kwake yeye mwaka 1990 alipopanda kutoka kuwa Naibu Waziri wa Nishati, Maji na Madini baada ya kuwa naibu katika wizara hiyo hiyo kwa miaka miwili.

Vijana hao wawili ni William Ngeleja ambaye sasa anakuwa Waziri wa Nishati na Madini akichukua nafasi ya Karamagi aliyelazimika kujiuzulu kwa kashfa ya Richmond na Dk. Diodorus Kamala anayekuwa Waziri wa Afrika Mashariki.

Wakati vijana hao wakipanda, mwenzao, Emmanuel Nchimbi aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana na Dk. Mathayo wanaendelea kubakia manaibu waziri.

Hata hivyo, uamuzi wa Rais kumpeleka Nchimbi Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, moja ya wizara nyeti, kunaonyesha namna alivyo na imani na mwanasiasa huyo ambaye alikuwa mstari wa mbele kupigania ushindi wa Kikwete mwaka 2005.

Aidha, Uamuzi wa Rais Kikwete kuwapandisha vijana hao, umeungwa mkono kwa nguvu kubwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema).

Ukiacha hilo, sura mpya sita zilizoingia kwa mara ya kwanza katika baraza hilo zinajumuisha Kapteni (mstaafu) George Mkuchika (Newala-CCM) ambaye anakuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, ambaye ndiye mbunge pekee ambaye hakuwepo katika baraza la awali anayekuwa waziri kamili.

Kuingia kwa Mkuchika katika Baraza la Mawaziri ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, kunamfanya Kikwete aendelee kukisogeza chama katika utendaji wa karibu wa serikali kwa mfano ule wa mtangulizi wake Benjamin Mkapa.

Wapya wengine watano wanaoingia pamoja na Mkuchika japo ni katika nafasi za unaibu uwaziri ni Dk. Lucy Nkya (Viti Maalum-CCM) anayekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. James Wanyancha (Serengeti-CCM) ambaye ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Wengine ni Ezekiel Maige (Msalala-CCM) anayekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki (Bukoba Mjini-CCM) anayekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani na Adam Malima (Mkuranga-CCM) anayeshika unaibu uwaziri wa Nishati na Madini.

Baraza la Mawaziri:

Ofisi ya Rais; Utawala Bora - Sofia Simba (awali Maendeleo ya Jinsia na Watoto), Menejimenti ya Utumishi wa Umma - Hawa Ghasia (hajabadilishwa).

Ofisi ya Makamu wa Rais; Muhammed Seif Khatib, anakuwa Waziri wa Nchi masuala ya Muungano (awali Habari, Utamaduni na Michezo), Dk. Batilda Buriani - Mazingira (awali Bunge).

Ofisi ya Waziri Mkuu; Philip Marmo anakuwa Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge wakati Stephen Wassira anakuwa Waziri wa Nchi TAMISEMI, huku Celina Kombani akiwa ni naibu wake.

Wizara mpya ya Mipango na Fedha itaongozwa na Mustapha Mkullo akisaidiwa na manaibu wawili ambao ni Jeremia Sumari na Omar Yusuf Mzee.

Profesa David Mwakyusa amebakia kama Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, akiendelea kufanya kazi na aliyekuwa naibu wake wa awali, Dk. Aisha Kigoda.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itabakiwa na waziri tu ambaye ni John Chiligati akihamishwa kutoka Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, inayojumuisha elimu kuanzia ya msingi hadi ile ya juu, anakuwa Profesa Jumanne Maghembe aliyehamishwa kutoka Maliasili na Utalii na huko atasaidiwa na Gaudencia Kabaka na Mwantumu Mahiza kama manaibu mawaziri.

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Tekinolojia sasa anakuwa Dk. Jumanne Kawambwa ambaye ni Mbunge wa Bagamoyo anakotoka Rais Kikwete. Naibu Waziri wake anakuwa Dk. Maua Daftari, mmoja wa manaibu waziri waliobakia ngazi hiyo ya unaibu kwa miaka mingi sasa.

Wizara ya Miundombinu ambayo sasa inabakia kuwa na barabara, usafiri wa reli, anga na maji pekee, waziri anaendelea kuwa Andrew Chenge, mwanasiasa ambaye kubakia kwake serikalini kumezusha maneno mengi kutoka kwa wananchi mbalimbali.

Kama ilivyokuwa katika serikali iliyopita, Dk. Milton Makongoro Mahanga anabakia kuwa ni Naibu Waziri katika wizara hiyo hiyo ya Miundombinu.

Kwa upande wa Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni iliyo chini ya Mkuchika, itakuwa na naibu mmoja tu, Joel Bendera anayebakia katika wadhifa huo na wizara hiyo hiyo.

Profesa Juma Kapuya, mtu anayetajwa kuwa mmoja wa watu wa karibu wa Rais Kikwete, amehamishwa kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na sasa anakuwa Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana ambayo ndiyo aliyokuwa akiiongoza wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu.

Kapuya katika wizara yake hii, atakuwa akisaidiwa na naibu wake, Ezekia Chibulunje ambaye katika baraza la mawaziri lililopita alikuwa ni Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko.

Prof. Mark Mwandosya aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), anahamishwa kutoka wizara hiyo na kuwa waziri kamili wa Maji na Umwagiliaji akisaidiwa na Christopher Chiza.

Margaret Sitta, aliyeiongoza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mafanikio katika serikali iliyopita, sasa anakuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto akichukua nafasi ya Sofia Simba aliyepelekwa Ofisi ya Rais.

Sitta anaongoza wizara hiyo akisaidiwa na naibu waziri mpya, Dk. Lucy Nkya anayeingia serikalini kwa mara ya kwanza.

Naye Profesa Peter Msolla aliyekuwa Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, sasa anahamishiwa katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirikika akiwa waziri, huku akisaidiwa na naibu wake Dk. Mathayo David aliyekuwa naibu katika wizara hiyo hiyo.

John Magufuli, mmoja wa mawaziri ambao uchapakazi wao hauna shaka, anahamishwa kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na sasa anakuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi akisaidiwa na naibu mpya katika baraza, Dk. James Wanyancha.

Wizara ya Maliasili na Utalii sasa itakuwa chini ya Shamsa Mwangunga aliyepanda kutoka kuwa Naibu Waziri na chini yake atakuwa akisaidiwa na Ezekiel Maige.

Wizara ya Mambo ya Ndani sasa itaongozwa na Lawrence Masha aliyepandishwa kutoka kuwa naibu hadi waziri kamili, na huko atasaidiwa na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Kagasheki.

Bernard Membe, rafiki wa karibu na wa siku nyingi wa Rais Kikwete, na mtu anayetajwa kuwa na nafasi kubwa kisiasa siku zijazo, anaendelea kubakia kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akisaidiwa na naibu wake yule yule, Balozi Seif Iddi.

Wizara ya Nishati na Madini inaongozwa na Ngeleja, mmoja wa wanasiasa vijana na aliyedumu muda mfupi zaidi serikalini kuliko wengine wote, ambaye naye atasaidiwa na Mbunge wa Mkuranga na mwanasiasa machachari, Adam Malima.

Manaibu Waziri wengine waliopanda ni Mathis Chikawe ambaye sasa anakuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Dk. Hussein Mwinyi ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, ambaye anakuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akisaidiwa na Nchimbi.

Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo waziri wake anakuwa Kamala, itakuwa na naibu wake ambaye ni Mohammed Aboud. Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, sasa itaongozwa na Dk. Mary Nagu aliyehamishwa kutoka Wizara ya Sheria na Katiba na hivyo kumfanya mmoja wa mawaziri wawili wanawake (mwingine ni Mwangunga) wanaoongoza wizara nyeti. Naibu Waziri wa Nagu sasa anakuwa Dk. Cyril Chami aliyetokea Mambo ya Nje.

No comments: