Friday, February 29, 2008

Waislamu 'magaidi' waibana Serikali

Na Glory Mhiliwa, Arusha

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Bw. Laurence Masha, ametakiwa kuwachukulia hatua za kinidhamu maofisa wa Jeshi la Polisi kwa kuwakamata wanachama wanane wa Umoja wa Waislamu Arusha (AMU) wakati Rais George Bush wa Marekani akiwa ziarani jijini hapa.

Barua iliyoandikwa na wanachama hao kwenda kwa Waziri Masha inaeleza kuwa wanachama hao walikamatwa Februari 17 mwaka huu saa 6 mchana nyumbani kwa Katibu wa AMU, Bw. Mohamed Akida, mtaa wa Pangani kwa madai ya kutaka kuvuruga ziara ya Rais huyo.

Wanachama hao waliokamatwa walitajwa kuwa ni Alhaji Yusuf Ally, Bw. Said Larusai, Bw. Jamal Shaban, Bw. Abdalah Salim, Bw. Ahemd Kassa, Bw. Yusuf Mchinja, Bw. Akida na Bw. Mohamed Mkindi.

Katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba AMU/KD/2008/017 iliyosainiwa na Mwenyekiti Alhaj Yusuf Mkindi, chama hicho pia kinataka Jeshi hilo likiri kosa hilo hadharani na liwaombe radhi Waislamu wote kwani kitendo cha kukamatwa kwao kimewajengea taswira mbaya mbele ya wanajamii.

“Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani kupitia kwako, tunaliomba Jeshi lako likiri kosa hilo hadharani na liwajibike kutuomba msamaha sisi wanachama wa AMU,” ilisomeka barua hiyo yenye kurasa nne.

Katika barua hiyo Mwenyekiti huyo alieleza kuwa maofisa wa Polisi wakiongozwa na afisa wa ngazi ya wilaya mwenye cheo cha juu, walifika nyumbani kwa Katibu wao na kuwataka watu waliokuwa hapo waende kituo Kikuu cha Polisi kujieleza kwa kufanya kikao haramu.

“Tulimweleza ofisa huyo kuwa kikao kile kilikuwa mwendelezo wa kikao cha Februari 13 mwaka huu ambacho kiliahirishwa, kutokana na idadi ya wajumbe wanaohitajika kutofikia na tulimwonesha ajenda zake, lakini hakutaka kutusikiliza,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.

Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa walipofikishwa kituoni, waliandika maelezo na baadaye waliwekwa rumande hadi Februari 18 saa 12.30 jioni wakaachiwa wakati ziara ya Rais wa Marekani ikiwa imemalizika.

“Tukiwa kituoni tuliomba tupewe nafasi ya kuonana na viongozi wa juu wa Polisi Arusha tukakataliwa na kuelezwa kuwa sisi ni magaidi wa mtandao wa kundi hatari la Al-qaeda,” ilidai barua hiyo.

“Sisi hapa tunasema tumeonewa. Majina yetu yamepakwa matope. Kila mahali tunapopita watu wanatuona kama washari na wengine wanatukejeli kama magaidi wa kundi la Al-qaeda, hasa baada ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kukiri kwenye vyombo habari kuwa kuna watu wamekamatwa Arusha na Dar es Salaam kwa ugaidi,” iliendelea kusomeka barua hiyo.

Chama hicho kinalalamika kuwa kitendo hicho kimewadhalilisha sana kwa kuwa kiroho, magaidi wanatambulika kama watu wanaofanya vitendo vya kishetani ambavyo vinawatisha watu. “sisi tunatumia fursa hii kulitaka Jeshi la Polisi lisafishe majina yetu”.

AMU ilianzishwa miaka miwili iliyopita na kupewa hati ya usajili namba 14590 na madhumuni yake ni kuwaunganisha waumini wa dini hiyo katika masuala mbalimbali hasa ya kiroho na kijamii.

No comments: