Friday, February 29, 2008

Mafisadi wa BoT warudisha bilioni 50/-

Mkullo asema fedha hizo zimekusanywa kwa mwezi mmoja
*Amwambia bosi wa IMF zitakazorudishwa ni bilioni 121/-
KAMPUNI zilizohusika na ufisadi wa kuchota mabilioni ya fedha ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), zimerudisha serikalini Sh bilioni 50 hadi sasa, imefahamika.

Fedha hizo zimerejeshwa baada ya Rais Jakaya Kikwete kuamuru mwezi uliopita kampuni 22 zilizohusika na ufisadi wa Sh bilioni 133 kupitia EPA, kurudisha fedha hizo na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mustapha Mkullo, aliwaambia waandishi wa habari leo wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Dominique Strauss-Khan, kuwa fedha hizo zimepatikana ndani ya mwezi mmoja uliopita.

“Tumeweza kukusanya Sh bilioni 50 ndani ya mwezi mmoja tu na tunatarajia kukusanya fedha na mali zaidi ambazo ziliibwa BoT,” alisema Mkullo. Mkullo alisema Serikali pia imefanikiwa kukamata mali za wahusika, zikiwamo zilizofichwa nje ya nchi na wamiliki wa kampuni hizo.

Hata hivyo, hakutaka kutaja thamani ya mali na majina ya kampuni zilizorudisha mali na fedha hizo.

“Tumekamata mali nyingi tu na nyingine zilikuwa nje,” alisema Mkullo na kuongeza kuwa, lengo na matarajio ya Serikali itafanikiwa kurejesha asilimia 80 ya fedha zote zilizoibwa, yaani Sh bilioni 106.4.

Suala la ufisadi ndani ya BoT liliibuka mwaka jana baada ya Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kuonyesha upungufu katika akaunti ya EPA na hivyo Serikali kuamuru uchunguzi zaidi kufanyika kwa kutumia kampuni ya nje.

Serikali iliiteua kampuni ya Ernst & Young kufanya uchunguzi wa kasoro zilizokuwapo kwenye ulipaji wa EPA na ikagundua ubadhirifu mkubwa wa fedha ukiuhusisha uongozi wa BoT na kampuni 22.

Rais Kikwete alimfukuza kazi aliyekuwa Gavana wa BoT, Dk. Daudi Ballali na akaamuru akaunti ya EPA kufungwa. Pia aliunda kamati iliyojumuisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi na kuwashughulikia wa husika.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa IMF, Strauss-Khan, ameipongeza Serikali kwa namna ilivyoshughulikia masuala ya ufisadi wa BoT na Richmond. Strauss-Khan alisema jana kuwa nchi zote duniani zina matukio ya vitendo vya rushwa ila kitu muhimu ni kuhakikisha kwamba nchi husika zinapambana na ufisadi huo.

Bosi huyo wa IMF alitanguliwa na ujumbe mzito wa maofisa wa IMF ambao walikuwapo nchini tangu Jumanne wiki hii ambako walikutana na viongozi mbalimbali wa Serikali na taasisi akiwamo Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndulu. end annet

No comments: